Menu
in , ,

Mayweather ampopoa Pacquiao

 

 

Bondia Mmarekani, Floyd Mayweather ameendeleza ubabe kwa kuwa bondia ambaye hajapigwa hata pambano moja, baada ya kuibuka mshindi alipopigana na Mfilipino Manny Pacquiao.

 

Ilikuwa kazi ngumu katika ukumbi wa MGM Grand Garden Arena, Las Vegas, Marekani baina ya wakali hao wawili, ambapo hatimaye Mayweather alitangazwa na majaji kuwa mshindi kwa pointi.

 

Mayweather (38) ameibuka mshindi kwenye pambano aghali zaidi katika historia ya ngumi duniani, ambapo aliweza kujilinda dhidi ya mpinzani wake katika shindano la uzani wa Welterweight wa WBO na kujiongezea mkanda huo kwenye ile ya WBC na WBA anayoishikilia kwa sasa.

 

Majaji watatu walimpa Mayweather ushindi kwa kumtangulia mwenzake kwa pointi 118-110, 116-112 na 116-112. Hadi sasa, katika mapambano yake 48 ya kulipwa, Mmarekani huyu hajapigwa hata pambano moja katika miaka 19 aliyokaa ulingoni.

 

Pacquiao ambaye ni mbunge wa Ufilipino anayeheshimiwa sana ameshinda mapambano 57, kushindwa sita na kwenda sare mawili, lakini amesema kwamba amepoteza hili kwa sababu ya jeraha alilokuwa nalo begani.

 

Mapato ya pambano hili yanakadiriwa kuwa pauni milioni 265, ambapo mabondia wanagawana kati yao pauni milioni 150, kiwango ambacho hakijapata kutokea katika historia ya ngumi duniani.

 

Hili ni pambano lililopewa jina la ‘Pambano la Karne’ ambapo washabiki wa Amerika walikamuliwa karibu pauni 66 kulitazama kwenye televisheni, na mamilioni wengine wakilifuatilia pia kwenye televisheni kwingineko duniani.

 

Pacquiao (36) alikuwa akipewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda kutokana na washabiki na wadau waliotoa maoni kabla, na aliingia ulingoni huku ukipigwa wimbo aliorekodi rasmi kwa ajili hiyo.

 

Kwa upande mwingine, Mayweather, ambaye ni mkazi wa eneo la karibu na ukumbi huo, alizomewa wakati wa kuingia na kulikuwa na wasiwasi katika kambi yake.

 

Baada ya kushinda, Mayweather amesema kwamba yupo hatua 10 mbele ya wenzake. Alicheza vyema ambapo licha ya wote kujaribu kujiachia kwa mbali, aliweza kusukumiza ngumi za mkono wa kulia kwa mpinzani wake.

 

Mayweather kwa ujumla alionekana mkubwa kuliko mwenzake, lakini pia alikuwa akicheza haraka kuliko mwenzake, na hata alipokaribiwa alimbana na kumbana.

 

Katika hatua nyingine, bondia wa Uingereza, Amir Khan, amedai kwamba Mayweather anataka kupambana naye baada ya kuibuka na ushindi huo.

 

Khan amedai kwamba alifuatwa na meneja wa Mayweather, Len Ellerbe kabla ya pambano la Jumamosi na kumweleza kwamba sasa wanamtaka, maana wanajua litakuwa pambano kubwa.

 

Siku zilizopita Mayweather alinukuliwa akidai kwamba baada ya kucheza na Pacquiao angestaafu na baba yake Mayweather mwenye jina hilo hilo alikuwa akieleza wasiwasi kwamba mwanawe angeweza kufilisika.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version