Bondia aliyeisisimua dunia kwa kutopoteza pambano lake hadi sasa, Floyd Mayweather ameichana Afrika, akisema hana sababu ya kulisaidia bara hilo wala watu wake.
Mmarekani huyo aliyemshinda Manny Pacuioaco wa Ufilipino Jumapili kwa pointi kwenye shindano lililozalisha fedha nyingi zaidi duniani, ameonesha kukerwa na kidomodomo cha watu.
Mayweather, bondia mweusi, anadai ana roho nzuri lakini hajihisi kwamba ana wajibu wa kutoa sadaka kwa wakfu au wahitaji, hasa Afrika.
“Watu wanasema eti ana fedha zote hizi, kwa nini hazitoi kwa ajili ya Afrika? Lakini tujiulize, Afrika imetupa nini? Afrika imekuja lini na kuwapa chochote watoto na familia yangu? Mambo ni kula na kulipa,” anasema Mayweather.
Bondia huyo ambaye ndiye mchezaji mwenye utajiri mkubwa kuliko wengine wote katika kada mbalimbali ikiwamo soka, tenisi na michezo mingineyo anasema kutoa sadaka kuna hatari zake.
“Kila mara kila mtu anazungumzia juu ya kutoa tu, kutoa tu, kutoa tu. Hilo ndilo tatizo. Watu wanatoa sana lakini hatimaye wanaishia kubaki kapuku.
“Baada ya hapo wale wale waliokuwa wanamtaka atoe sadaka wanaanza kuuliza ‘kwa nini huyu alitoa kwa mtu yule wakati alitakiwa kuweka katika hazina,” anaseama bondia huyo anayejua kutanua kwa fedha nyingi katika maisha ya kifahari.
Mayweather anadai kwamba anatakiwa aachwe ili aweze kufanya kila anachokitaka kwa maato yake, kama vile kujinunulia bidhaa na huduma anazotaka yeye pamoja na familia yake.
“Sikuingia kwenye mchezo wa makonde kwa sababu eti nije kupigana, nipate mamia ya mamilioni ya dola kwa ajili ya kutoa yote msaada kwa watu.
“Kama ni kuchezea fedha zangu basi nitazitumia mwenyewe. Nitazifanyia ninachotaka maana ni zangu. Unasikia watu wakisema eti ‘alitakiwa kutoa msaada kwa huyu au yule. si sawa, natakiwa kutoa kwa Floyd Mayweather, kutoa kwa ajili ya familia ya Floyd Mayweather kwa sababu ndio inawahusu,” anasisitiza.
Mayweather (38) ana utajiri wa fedha taslimu wa dola takriban milioni 330.
Hata hivyo, ana wakfu iitwayo ‘The Floyd Mayweather Jr. Foundation’ inayosaidia vijana walio katika mazingira magumu huko Las Vegas, Nevada anakoishi.