Menu
in , , ,

MATUMAINI YA SAFARI YA ENGLAND KOMBE LA DUNIA YAPO HAPA!

Tanzania Sports

June 30 mwaka 1966 ilikuwa siku ambayo iliacha alama kwa England, alama ambayo ilishuhudiwa ikiwekwa katika uwanja wa Wembley. Furaha, shangwe, kelele zilitawala pale nahodha Bobby Moore alipokabidhiwa kombe la dunia na kulinyanyua juu kama ishara ya kwamba ni mali ya England rasmi mbele ya Malikia Elizabeth wa pili.

Rasmi England ikaingia kwenye orodha ya mataifa ambayo yamefanikiwa kuchukua kombe la dunia ambapo mpaka sasa ni mataifa nane pekee ambayo yamefanikiwa kuchukua kombe la dunia.

Ilikuwa siku  ya furaha kwa  England kuchukua kombe la dunia, kila mtaa ulitawaliwa na furaha hakukuwepo na kificho kuhusiana na hili. Swali kubwa lilibaki England ataendeleza kitu alichokifanya katika uwanja wa Wembley mwaka 1966?, lilikuwa swali gumu ambalo jibu lake lilipatikana uwanjani kutokana na England kushindwa tena kufanya vizuri kama walivyofanya mwaka 1966.

Hakukuwepo na muendelezo wa mafanikio tena kwa England kwenye michuano hii ya kombe la dunia mpaka pale Italy ilipopewa nafasi ya kuandaa michuano ya kombe la dunia la mwaka 1990, michuano ambayo ilishuhudia fainali ya mwaka 1966 ikirudiwa katika ngazi ya nusu fainali ambapo England safari hii alifungwa na Ujerumani Magharibi katika hatua ya nusu fainali.

Ndoto za England kuchukua kombe la dunia tena kwa mara ya kwanza baada ya miaka miaka ishirini na nne (24) ikawa imekatika, ndoto ambayo ilikuwa imejengwa vichwani mwa watu wengi kwa sababu Sir Boby Robson alikuwa ametengeneza timu ambayo ilionekana inaweza ikafika mbali.

Gary Lineker aliwahi kukiri England ya Sir Boby Robson ilikuwa England imara, uimara ambao ulikuwa ukiwapa matumaini ya kuchukua kombe la dunia lakini mwisho wa siku wakawa nje ya mategemeo yao, nafasi ya nne ikawa sahihi kwao.

Hawajawahi kufika tena hatua kubwa kwenye michuano hii tangu 1990 zaidi ya kufika robo fainali tu. Wanaenda tena Russia, safari hii wakiwa hawana mategemeo makubwa kama michuano mingine ambayo waliwahi kwenda.

Hawana kikosi cha kuwafanya wapate nguvu ya kusema kuwa wanauwezo wa kuchukua kombe hili la dunia na kibaya zaidi hawamwamini kocha wao Gareth Southgate, lakini mwanga wa England kufanya vizuri kwenye michuano hii iko maeneo yafuatayo;

Kocha wa England  amebadilisha mfumo wa kiuchezaji katika timu, kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Nigeria aliamua kutumia mfumo wa 3-5-2 ambapo Trippier pamoja na Ashley Young wakicheza Wingback na kumfanya Eric Dier acheze eneo la kiungo wa kuzuia huku mbele yake wakicheza Jesse Lingard pamoja na Delle Ali ambao waliwapa nafasi Harry Kane na Raheem Sterling kucheza kama washambuliaji wawili wa mbele. 

Mfumo huu unawapa nafasi wachezaji wa England kufanya vizuri kwa sababu umri wao unaendana na kasi ya mfumo huu, pia mfumo huu una wachezaji wengi wa kucheza, mfano katika ya nafasi ya Wingbacks anaweza kuwatumia pia kina Kyle Walker upande wa kulia na Danny Rose upande wa kushoto.

Kitu hiki kinaweza kikawapa tumaini la wao kufika mbali kwa sababu Gareth Southgate atakuwa na nafasi kubwa ya kuwa na wachezaji mbadala na kitu kizuri kwao wapo kundi ambalo siyo gumu kwao wakiwa na timu za Belgium, Panama na Tunisia. Na kama wakifanikiwa kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi lao watakutana na mshi ndi wa pili wa kundi H lenye timu za Colombia, Japan, Poland na Senegal.

Hii inaonesha timu zote ambazo England anakutana nazo kuanzia katika hatua ya makundi mpaka hatua ya kumi na sita bora kuna mwanga ambao unaonesha anaweza kufika katika hatua ya robo fainali kama asipodharau timu kwa sababu kuanzia hatua ya makundi mpaka hatua ya kumi na sita bora (16) hawatokutana na timu ambazo zinauzito mkubwa.

Changamoto kubwa ni timu kuonekana imejengwa kupitia Harry Kane, huyu ndiye mchezaji anayeonekana ana kiwango kikubwa cha dunia katika kikosi cha England , ingawa kuna vijana ambao wanaweza wakaleta mabadiliko ndani ya mchezo kama Marcus Rashford.

Hazina ya wachezaji vijana waliopo katika kikosi cha England kuanzia katika safu ya ulinzi kuanzia kwa Pickford aliyechukua nafasi ya mkongwe Joe Hart mpaka safu ya ushambuliaji, hii ni silaha ambayo ikitumika vizuri inaweza ikawa faida kwa England kwa sababu vijana hawa wataendana na kasi ya mpira wa sasa.

Gareth Southgate anatakiwa awajenge vijana wake katika hali ya kupigana zaidi na kuwakumbusha kuwa umri waliopo ndiyo umri wa kwao kupigania taifa lao na mafanikio yao kwa ujumla.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version