*Drogba, Toure, Mo Farah walifanya makubwa*David Rudisha, Chipolopolo waliweka rekodi*Cameroon, Misri zaaibika kwenye kandandaMwaka 2012 umetutupa mkono, tumeingia 2013, na ni jambo la shukurani kwa Mwenyezi.
Njia bora ya kuanza jambo jipya ni kutazama tulipotoka, tulipo ili kupata njia na mikakati ya kusonga mbele. Januari mosi hii na siku chache zijazo, bado tutakuwa na kigugumizi cha kuutamka mwaka huu 2013, lakini hebu turejee machache makubwa kwenye michezo ya mwaka jana. Baadhi ya hayo ni mafanikio ya mwanasoka Didier Drogba, mwanariadha mlemavu Oscar Pistorius; Chipolopolo ya Zambia na baadhi ya weusi kutamba kwenye Michezo ya 30 ya Olimpiki iliyofanyika London, Uingereza.
Mo Farah na Medali Mbili za Dhahabu Olimpiki
Hili la mwisho linatufungulia ukurasa, kwa kumtazama Mo Farah aliyetwaa medali mbili za dhahabu kwenye michuano hiyo. Huyu ni Mwingereza kwa uraia aliochukua, lakini ni mzaliwa na Somalia na damu ya Kiafrika ingali ikizunguka mwilini mwake. Farah alitwaa medali katika mbio za urefu wa mita 5,000 na 10,000, na mwenyewe alishangazwa na kushinda zile za mita 5,000. Aliwaambia hivi waandishi wa habari baada ya kushinda: “Loh, medali mbili za dhahabu za Olimpiki, nani angeweza kuwaza hili?” Si wengi, lakini ni wazi Afrika inajivunia miguu na moyo wake.
Cameroon, Misri Zakwama AFCON
Wakati mwaka 2012 ulikuwa mzuri kwa timu mbalimbali za soka, hali haikuwa hivyo kwa timu za mataifa ya Cameroon na Misri. Hata majina yao makubwa ya Simba Wasiofugika kwa Cameroon na Mafarao kwa Misri hayakuwasaidia kufurukuta, bali walikabwa vilivyo na nchi zilizoingiza timu chipukizi. Hiyo ilimaanisha kwamba Misri waliokuwa katika kimuhemuhe cha vuguvugu la mapinduzi ya Kiarabu katika siasa walishindwa kutetea ubingwa wao kwenye fainali zilizofanyika Gabon na Guinea ya Ikweta. Kana kwamba hiyo haitoshi, walishindwa pia kufuzu kwa ajili ya fainali za mwaka huu zinazofanyika nchini Afrika Kusini. Cameroon wanajiuguza maumivu sampuli hiyo hiyo, kwani hawakufika fainali za mwaka jana na walipigwa kumbo na Cape Verde na kutupwa nje ya fainali za mwaka huu.
Oscar Pistorius Aweka Historia
Mwanariadha Oscar Pistorius wa Afrika Kusini ameweka historia kwa kuwa mwanariadha wa kwanza aliyekatwa miguu (ana miguu bandia lakini) kushiriki michuano ya Olimpiki kwenye mashindano ya wasio na ulemavu wowote. Baada ya kupelekeshana na Shirikisho la Riadha la Kimataifa na vyama vingine, hatimaye mwaka 2008 alipumua baada ya Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) kusema anastahili kushindana na hao wenye viungo kamili. Hata hivyo, hakushiriki mwaka huo kwa sababu hakufuzu kwenye mchujo wa kawaida, lakini hakukata tamaa, akaendeleza mazoezi na mwaka jana akaingia kwenye fainali za London, katika mbio za mita 400. Alisifiwa na kuelezewa kuwa moja ya watu waliofikia mafanukio makubwa katika michuano hiyo ya Olimpiki, akawa eneo la marejeo ya mafanikio kwa watu wengi kote duniani. Mkenya Rudisha Aweka Rekodi ya Dunia
Tukiwa bado kwenye Michezo ya 30 ya Olimpiki, mwanariadha wa Kenya, David Rudisha ‘King’ aliendelea kutawala katika mbio za urefu wa mita 800. Safari hii, si kwamba alishinda medali ya dhahabu tu, bali pia alisonga mbele na kuweka rekodi ya kasi zaidi katika mbio hizo, akitangulia wanariadha wengine wenye sifa kubwa. Kwa ubora wa viwango vyao, aliyeshika nafasi ya nane mwaka jana, Mwingereza Andrew Osagie mwenye asili ya Nigeria angeweza kutangazwa mshindi michuano ya Olimpiki ya mwaka 2000. Ni mafanikio haya yaliyosababisha Rudisha kutunukiwa taji la Mwanamichezo wa Mwaka wa Kenya, katika hafla iliyofanyika mapema Desemba mwaka jana jijini Nairobi.
Wanawake Guinea ya Ikweta Malkia Wapya
Mwaka 2012 ulishuhudia Afrika wakipata malkia wapya wa soka katika soka. Timu ya soka ya wanawake iitwayo Nzalang ilitwaa ubingwa wa Mashindano ya Ubingwa wa Wanawake baada ya kuwakung’uta Afrika Kusini mabao 4-0. Waliokuwa wakishikilia kombe hilo ni Super Falcons wa Nigeria. Kwa ushindi huo, mchezaji wao nyota, Genovova Anonma alichaguliwa kuwa mchezaji bora kwa Afrika.
Milima na Mabonde kwa Afrika Olimpiki
Michezo ya 30 ya Olimpiki ilikuwa na mchanganyiko wa hisia kwa timu za Afrika. Ilikuwa mara ya kwanza timu za bara hilo kuwa eneo moja katika kijiji cha Afrika. Humo kulikuwa na klabu, makumbusho na biashara, lakini furaha iliishia njiani kwa kufungwa kutokana na kushindwa kukidhi matakwa ya mkataba. Ama kwa upande wa michezo, nchi za Afrika Kusini na Ethiopia zilipata medali tatu kila moja; Kenya ilipata mbili za dhahabu na Gabon na Uganda zikaambulia moja moja. Nchi za Cameroon, Ghana, Nigeria, Tanzania na nyinginezo zilifanya vibaya na kuwasikitisha raia wao waliokuwa London na nyumbani, kwani wanamichezo wake hawakupata medali hata moja. Nyota ya Yaya Toure Yang’aa Kote
Yaya Toure, kiungo wa mabingwa wa soka wa England, Manchester City alikuwa na mwaka mzuri kwa ujumla. Pamoja na kufanikiwa kuiongoza klabu yake kutwaa ubingwa wa nchi kwa mara ya kwanza katika miaka 44, amechaguliwa kuwa mwanasoka bora wa Afrika kwa 2012. Mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona alikuwa injini muhimu ya kuisukuma City kutwaa ubingwa mwaka jana. Ubingwa huo haukupatikana kirahisi, kwani ilibidi wasubiri hadi mechi ya mwisho, ambapo walitakiwa kushinda, na hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika walihitaji mabao mawili, na walipigana kufa na kupona hadi kuyapata. Toure mwenye umri wa miaka 27, na Didier Drogba wamekuwa mmoja wa nguzo muhimu ya timu yao ya taifa ya Ivory Coast iliyokosa ubingwa wa mwaka jana kwenye tundu la sindano.
Al-Ahly Na Kombe la Saba la CAF
Klabu ya soka yenye mafanikio zaidi Afrika, Al-Ahly ya Misri imefanikiwa kutwaa kwa mara ya saba kombe la Klabu Bingwa ya Afrika chini ya CAF. Hata hivyo, mwaka ulianza kwa machungu kwao, kwani washabiki wake walishambuliwa baada ya mechi iliyofanyika Uwanja wa Port Said Februari mwaka jana na kusababisha vifo vya watu 74. Hali hiyo ilisababisha taharuki kubwa, kiasi cha kupelekea kusimamishwa kwa ligi ya Misri. Hata hivyo, Al-Ahly walisahau yote hayo, wakaweka jitihada na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Esperance ya Tunisia kwenye mechi ya marudiano.
Drogba Alivyowavika Chelsea Ubingwa
Mwana mwingine wa Afrika aliyeng’ara mwaka 2012 ni Didier Drogba. Baada ya miaka minane yenye mafanikio makubwa Chelsea, Drogba alimalizia muda wake Stamford Bridge kwa mkwaju wa mwisho wa penati uliozaa bao na kuwatawaza Chelsea kuwa mabingwa wa Ulaya. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza wa Chelsea katika historia kutwaa taji hilo, Drogba akimaliza kwa furaha kuu mbele ya mmiliki wa klabu, bilionea wa Kirusi, Roman Abramovic. Mafanikio ya klabu hiyo yasingepatikana bila mchango wa Drogba kwenye mechi hiyo nchini Ujerumani na zilizotangulia. Bao lake dhidi ya Napoli ya Italia wakati wa marudiano ndilo liliwarejesha Chelsea kwenye ushindani. Baada ya hapo, Drogba alifunga bao dhidi ya Barcelona kwenye mchezo wa awali wa nusu fainali. Katika fainali kwenye uwanja wa wapinzani wao, Bayern Munich walibakisha dakika mbili watawazwe mabingwa. Alikuwa Drogba aliyegeuza furaha yao kuwa kiwewe kwa kupachika bao la kusawazisha. Katika muda wa ziada, timu zilitoshana kwa bao 1-0 hivyo kuingia kwenye penati , Drogba akafunga ya mwisho iliyowatawaza Chelsea wafalme wa Ulaya, japo kwa mwaka jana tu.
Chipolopolo Wafuta Machozi kwa Ubingwa
Timu ya Taifa ya Zambia – Chipolopolo walifanikiwa mwaka jana kutwaa ubingwa wa Afrika, wakifuta machozi ya kupoteza timu nzima mwaka 1993. Walicheza katika nchi ya Gabon ajali ya ndege ilikotokea, na kabla ya kuondoka Zambia, Rais Michael Satta aliwakumbusha jambo hilo, nao wakaahidi kurudi na kombe. Awali ilionekana kama siasa tu, lakini kadiri muda ulivyokwenda, wachezaji wa kizazi kipya wa Chipolopolo waliishangaza dunia kwa kuonesha soka ya hali ya juu na kuwatoa kamasi waliopewa nafasi, Ivory Coast. Zambia walivishwa ufalme wa Afrika baada ya kufunga penati 8-7 chini ya kocha Harve Renard aliyesema ndoto yake ilikuwa hiyo. Mengi yanasubiriwa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na Manchester City kutetea ubingwa wao katika Ligi Kuu ya England. Hata hivyo, wameingia mwaka mpya wakitanguliwa na mahasimu na jirani zao, Manchester United kwa pointi saba. Timu zinazofuata ni Chelsea, Tottenham Hotspurs na Arsenal. Timu tatu zilizokuwa mkiani wakati mwaka 2012 ukimalizika ni Queen Park Rangers (QPR), Reading, Southampton, Aston Villa na Wigan. |