Menu
in , , ,

MATOKEO LIGI KUU BARA

 

YANGA YALIPA KISASI DHIDI YA MTIBWA

 

Mabingwa watetezi na vinara wa Ligi Kuu Bara, Dar-es-salaam Young Africans hapo jana waliwatandika Mtibwa Sugar mabao mawili kwa sifuri katika mchezo uliopigwa ndani ya uwanja wa Jamuhuri Morogoro.

Yanga waliingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao mawili bila majibu waliyofungwa msimu uliopita dhidi wenyeji wao hao na hatimaye hapo jana walilipa kisasi kupitia mabao yaliyowekwa wavuni na Malimi Busungu na Donald Ngoma katika kipindi cha pili cha mchezo.

Kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo huo kila timu ilijaribu kushambulia lango la wapinzani lakini hakukuwa na shambulizi kali lolote na hatimaye kipenga cha mapumziko kikapulizwa kila timu ikiwa haijaaandika bao.

Dakika saba baada ya kuanza kwa kipindi cha pili mshambuliaji Malimi Busungu akawaandikia Yanga bao la kwanza baada ya walinzi wa Mtibwa kufanya makosa na kumchanganya golikipa wao Said Mohammed wakijaribu kumzuia Donald Ngoma asifanye madhara ndani ya eneo la hatari.

Mtibwa Sugar walionekana kucheza mchezo wa kasi na kupeleka mashambulizi mengi langoni wakijaribu kusawazisha bao walilofungwa lakini juhudi zao hazikuzaa matunda mbaka kufikia dakika ya 90 ya mchezo ambapo Donald Ngoma alimaliza mchezo kwa kuifungia Yanga bao la pili.

Kwa matokeo haya Yanga ambao sasa wana alama 15 wanaendelea kujiweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na rekodi ya kushinda michezo yote mitano waliyocheza mbaka sasa ndani ya msimu huu.

 

SIMBA YAPATA USHINDI MWEMBAMBA

 

 

Baadhi ya wachezaji wa timu ya SSC
Baadhi ya wachezaji wa timu ya SSC

Baada ya kupoteza mchezo wa wiki iliyopita dhidi ya Yanga, hapo jana Simba Sports Club walijirejesha kwenye njia za ushindi kwa kuwafunga Stand United bao moja kwa sifuri katika mchezo uliopigwa ndani ya dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam.

Bao pekee la mchezo huo liliwekwa wavuni na mshambuliaji chipukizi Joseph Kimwaga anayekipiga kwa mkopo akitokea Azam FC. Simba waliutawala mno mchezo huo kwenye kipindi cha kwanza kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na viungo wao wakiongozwa na David Mwalyanzi kwenye eneo la katikati.

Hata hivyo Wekundu hao walilazimika kusubiri mbaka kipindi cha pili cha mchezo ambapo Joseph Kimwaga dakika chache baada ya kuingia uwanjani akichukua nafasi ya Said Ndemla aliwafungia bao lao pekee na la ushindi. Chipukizi huyo alifunga bao hilo kwa ufundi baada ya kumchambua mlinzi wa Stand United na kuweka mpira wavuni bila papara.

Ushindi huu unaiweka Simba kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara nyuma ya Azam FC wanaoshika nafasi ya pili baada ya hapo jana kuwatandika Coastal Union mabao mawili kwa sifuri yaliyofungwa na Shomari Kapombe na Kipre Tcheche.

Written by Kassim

Exit mobile version