Menu
in , , ,

Matheus Cunha amegeuka lulu EPL

Tanzania Sports

DIRISHA la usajili wa majira ya baridi linaelekea ukingoni mwezi huu. Katika dirisha hili majina kadhaa yamekuwa maarufu kwenye vyombo vya habari kutokana na kuwindwa na timu mbalimbali. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City wanawinda wachezaji wapya huku wakionekana kukata tamaa katika mbio z akuwania taji hilo msimu huu. 

Liverpool wao wapo kileleni, hawaonekani kuhusika katika usajili wa wachezaji wapya huku baadhi ya makinda wao wakiibuka taratibu kwenye kikosi cha kwanza, wengi wao wakiwa katika nafasi ya beki na kiungo. Arsenal wanatajwa kuwania saini ya mshambuliaji ili kuongeza mabao katika kikosi chao ambacho sasa hakuna uhakika wa miongoni mwao kupachika mabao 20 msimu huu. Jina la Matheus Cunha ndilo linalotaradadi zaidi kwenye mada nyingi za michezo EPL. 

Takribani timu 6 zinatajwa kuwania saini ya mshambuliaji wa Wolves, Matheus Cunha. Viongozi waandamizi wa Wolves wanaamini kuwa staa wao atabakia klabuni na kwamba hawapo tayari kumpoteza nyota huyo. Cunha amekuwa mchezaji wa kutumainiwa katika kikosi cha Wolves ambapo alifunga mabao mawili katika ushindi w a 4-1 dhidi ya Fulham. Kwenye mchezo huo Cunha alikuwa na siku nzuri kazini, na huenda ndiyo ilikuwa nzuri zaidi tangu alipoanza kuvaa jezi za Wolves. 

Kana kwamba haitoshi Cunha alikuwa nyota wa mchezo wakati klabu yake ilipomenyana na Chelsea msimu ulopita ambako alipachika mabao matatu, kisha akaonesha thamani yake zaidi katika mchezo dhidi ya Southampton kuwa yeye ni mshambuliaji anayejua kumalizia kazi nzuri na kuwapa furaha mashabiki wa klabu yao. ukiangalia au kusoma taarifa nyingi za usajili utaona jina la Cunha linaongoza kwenye chati ambayo inampa nafasi ya kinara kati ya wachezaji wanaowindwa. Cunha amekuwa lulu katika Ligi Kuu England na kinara wa kupigania kubaki Ligi kuu kati ya timu zinazoweza kushuka daraja msimu huu. 

Je kuna timu inayoweza kumsajili mshambuliaji huyo? Kwanza si wachezaji wote walioko kwenye timu zinazopambana kubaki Ligi Kuu wakawindwa na timu kubwa, lakini ukifanya tathmini na ulinganifu kati yake na washambuliaji walioko kwenye timu za juu za EPL utaona Cunha ana kitu cha ziada na ameonesha anaweza kuwazidi maarifa nyota wenzake. 

Katika hali ya kustaajabisha, Cunha ameibuka kattika medani ya ubashiri kuwa ni mshambuliaji ambaye ataihama Wolves na kujiunga na timu kubwa. Si timu kubwa pekee hata zile ambazo zipo kwenye msimu mzuri kama vile Nottingham Forest imemfanya Matheus Cunha kuwa chaguo lao namba moja katika usajili wa kuimarisha kikosi chao. Timu nyingine ambazo zinatajwa kuwania saini ya Cunha ni pamoja na Arsenal ya Mikel Arteta, Chelsea ya Enzo Moresca, Manchester United ya Ruben Amorim, Newcastle United ya Eddie Howe pamoja na Tottenham Hostpurs ya Daniel Levy. 

Wakati huo huo klabu ya Wolves ambayo imejikuta katika shinikizo la kumbakiza nyota huyo tegemeo inatarajiwa kuendelea kumshawishi ili asalie klabuni. Lakini kumbakiza Cunha katika klabu hiyo ni sawa na kujaribu kuzuia miguu yake isiguse mpira ppale anapokaribia langoni mwa adui. Cunha ni mshambuliaji wa ndoto ya kila kocha. Ni aina ya mchezaji ambaye kila wakati anaangalia nafasi muhimu na mianya ya kupachika mabao. Kwa mujibu wa mtandao wa takwimu wa Opta wanasema Matheus Cunha ndiye mshambuliaji mwenye mgoli mengi katika kikosi cha Wolves. 

Ndiye mchezaji aliyechangia mabao mengi, ndiye mwenye kupiga chenga nyingi (39),ndiye mchezaji anayeingia kwenye eneo la adui mara nyingi zaidi (90), na ndiye anayeshinda vita vya kuwania mpira kwenye hatua za mwisho kabla ya kufunga mabao (ameshinda mpira mara 16). Kimsingi takwimu zake ni za kiwango cha juu na ameonesha hilo katika msimu mzima akiwa Wolves. Ni wachezaji saba pekee ambao wamefunga mabao kuliko Cunha. Matheus Cunha yuko katika kiwango sawa na Ollie Watkins na Justin Kluivert, ambapo nyota wote hao wanashindana katika Ligi maarufu zaidi barani Ulaya.

Kama Wolves wanataka kuishi kwa amani katika Ligi ya EPL ni lazima wakubali kumuuza ama kuhakikisha timu inaonesha kila namna ya kubaki Ligi Kuu pamoja na kuongeza mishahara ya nyota huyo. Timu kama Arsenal, Chelsea, Manchester United au Man City zinapoingia sokoni kuwinda mchezaji maana yake zimejiridhisha kuwa anakwenda kuwapa kitu cha ziada na ambacho mwenyewe atanufaishwa nacho. Matheus Cunha pamoja na kucheza vizuri akiwa Wolves anakosa ladha ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Chelsea, Arsenal na Man City zina uhakika wa kufuzu msimu ujao. 

Changamoto pekee itakuwa Man United ambao wanahaha kumaliza msimu wakiwa salama, lakini pia Cunha anaweza kujiunga na timu hii kama njia ya kujihakikishia namba kikosi cha kwanza. Katika kikosi cha Man City Cunha atapata changamoto kutoka kwa Erlin Haaland katika kuongoza safu ya ushambuliaji, kwahiyo anaweza kugeukia macho yake kwenye timu nyingine ilia pate nafasi ya kucheza. 

Hata hivyo sehemu ya mwisho ambayo anaweza kunufaika nayo ni ofa itakayotolewa na klabu itakayomhitaji huku akiombea waajiri wake wa sasa Wolves wawe na moyo wa kumwachia ili aende kutafuta changamoto nyingine.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version