UONGOZI wa klabu ya Manchester United umetangaza Ruben Amourin kutoka Sporting Lisboa ya Ureno. Najua unashangaa kwanini nimeandika ‘Sporting Lisboa’, hilo ni jina lao, lakini kwa kiingereza unaweza kutamka Lisbon, yaani Sporting Lisbon. Ni kocha kijana mwenye umri wa miaka 38 tu anachukua jukumu kubwa la kuinoa Manchester United.
Huyu ni kati ya kizazi kipya cha makocha ambao wamejitosa katika kazi hiyo ambayo ni ngumu sana. katika makala haya nitachumbua maeneo matano ambayo kocha huyo yanayomkabili kocha huyo ambaye anatarajiwa kuanza kibarua chake Novemba 11 na mechi yake ya kwanza itakuwa Novemba 24 dhidi ya Ipswich town mwaka huu. Wakati huu Man United ipo chini ya kocha wa muda Ruud van Nistelrooy. Je ni mambo gani ambayo kocha mpya Ruben Amourin
Ari ya ushindi
Manchester United imezoeleka kuwa timu yenye kusaka ushindi kila inapokwenda kucheza. Lakini miaka ya karibuni klabu hiyo imekuwa ikukutana na vipigo isivyo kawaida, huku ari ya wachezaji wake ikiwa si kubwa sana. Kwa hali ya sasa ya Man United kocha mpya anatakiwa kuwasuka kisaikolojia wachezaji hao na kurudisha nyakati za ushindi za timu hiyo.
Wafumania nyavu
Safu ya ushambuliaji ya Manchester United ni nyanya au tuseme ni laini mno au butu isiyoweza kupachika mabao hata matatu katika mechi tatu mfululizo. Ushindi wa Manchester United dhidi ya Leicester City kwenye kombe la Carabao wa hivi karibuni mabao mawili yalitoka kwa kiungo mkabaji Carlos Casemiro. Washambuliaji wa Man United sio wakali, sio tishio na hawawezi kuifanya timu hiyo iwe gumzo kwa upachikaji wa mabao. Pengine mbinu za kocha zilikuwa zinawarudisha nyuma lakini bado wana safari ndefu yenye milima mingi ili kuwa washambuliaji wa kutajika. Washambuliaji waliopo sasa hawana uwezo wa kupachika mabao 20 kwa msimu mmoja. Kocha mpya anatakiwa kusuka safu ya ushambuliaji iweze kumletea mabao ya kutosha.
Safu ya ulinzi
Uamuzi wa kumrudisha Johnny Evans katika safu ya ulinzi ya Man United ulikuwa ujumbe hali si shwari eneo hilo. Tayari Raphael Varane alishaondoka klabuni hapo na kutoa nafasi kwa Urgate na De Ligt kulinda ngome yao. Man United imekuwa ikiambulia vichapo vingi kwa sababu ya safu ya ulinzi kuwa dhaifu na kuinyima ushindi. Jukumu la kocha sasa ni kuhakikisha anaisuka safu hii ili iweze kutumika kama nyenzo ya ushindi na kulinda kila mechi. Kama timu haifungi mabao maana yake inajweka kwenye shinikizo, na kusababisha hali ya kukosa utulivu kwa mabeki wake.
Ligi ya Mabingwa
Jambo moja la aibu alilokuwa akilifanya Eric Ten Hag ni kujenga mazingira ya kuiona Man United haipo katika anga za Ligi ya Mabingwa. Lakini historia inaonesha kuwa Man United imewahi kutwaa ubingwa mara kadhaa na kuwa vigogo wa soka barani ulaya. Kwa maana hiyo Man United inapaswa kuzungumzia namna ya kufuzu Ligi ya Mabingwa na kocha anatakiwa kuwa na kauli elekezi kwenda kwa wachezaji. Wengi wachezaji wao wa sasa hawajui utamu wa mataji ya Ligi ya Mabingwa ukiondoa Casemiro. Vijana wengi walioko kikosini wanahitaji akili za kushiriki ya Mabingwa kuliko kila msimu kuishia kucheza na Crystal Palace, Brighton na kadhalika.
Zimwi la kushindwa mafanikio
Kwa muda mrefu klabu hii imekuwa kwenye kipindi kigumu tangu alipoondoka Sir Alex Ferguson. Ubingwa pekee waliochukua chini ya Eric Ten Hag ni mataji mawili ya FA. Katika misimu miwili na nusu amefanikiwa kuchukua ubingwa huo lakini takwimu zinaonesha makocha wote waliopita baada ya Ferguson wamekuwa na wakati mgumu na kuandamwa na zimwi la kufeli.
Uhaba wa mafanikio ni kitu ambacho kimewafanya mashabiki wawe wanalalamika kuhusiana na wamiliki wa timu hiyo kushindwa kuendesha mambo na kushindana na majirani zao Man City. Hali ya kukosa mafanikio imewayumbisha mno Man United na kuonekana kuwa timu ya kawaida kwenye kandanda. Wameshiriki ya Ligi ya Mabingwa bila kuwa na kitu cha kujivunia. Hali kadhalika kwenye Europa League nako mamgo hayakuwa mazuri hivyo kuifanya timu iwe inachechemea kila msimu. Kocha mpya anatakiwa kuonesha kuwa Man United wanaweza na anahitaji kuimarisha zaidi ili kwenda kwenye safari ya mafanikio.