By Faustine Feliciane
Mataifa saba yamethibitisha kushiriki mashindano ya riadha ya Kanda ya Tano ya Afrika, yaliyopangwa kufanyika Februari 23.
Katibu Msaidizi wa Riadha Tanzania (RT), Julius Musomi, alisema jana kuwa mashindano hayo ambayo yatashirikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati, yatatimua vumbi mjini Moshi.
Musomi alizitaja nchi zilizothibitisha kuwa ni Kenya, Somalia, Uganda, Ethiopia, Zanzibar, Sudan na wenyeji Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Musomi, kila nchi itawakilishwa na wanariadha sita ambao watashiriki katika michezo ya kurusha visahani, kurusha tufe, mbio za kuruka chini na zile za vipimo vya mita.
Aidha, Musomi alisema kabla ya mashindano hayo kufanyika kutakuwa na mashindano ya taifa ya mbio za nyika yatakayofanyika Jumapili mjini Arusha kwa kushirikisha timu za mikoa ya Tanzania Bara.
Wakati huo huo, wanariadha Fabiola William na Paul Sumaye, waliondoka nchini jana kwenda China kushiriki mashindano ya kimataifa yanayodhaminiwa na Benki ya Standard Chartered yajulikanayo kama `The Greatest Race on Earth` yatakayofanyika keshokutwa jijini Hong Kong.