Nawasikitikia sana wanasoka wa kulipwa kwa sababu Michezo ya 30 ya Olimpiki imewaumbua.
Mashujaa waliopigana kufa na kupona kwenye Olimpiki hii wamewavua nguo, kuwaanika na kuwatia aibu isiyo kifani jamaa hao.
Kiburi cha wachezaji hao wa kulipwa ambao wanajidai kwamba ndio nguvu na nguzo zetu nyakati hizi, hakijapata kutikiswa kama sasa.
Mashujaa wa Olimpiki wameonesha nini maana ya uzalendo kwa jinsi walivyoonesha nidhamu ya hali ya juu pasipo kuwaiga wajeuri hawa wa soka.
Hawakuringa kukubali kuziwakilisha nchi zao, hawakujifaragua wala kudai walipwe kwa mamilioni ya pesa kabla wala baada ya kucheza.
Waliingia kambini kama walivyoagizwa, wakawa chini ya wakuu wa misafara, wakafuata ratiba, wakapeperusha bendera za nchi zao kwa kadiri walivyoweza pasipo unafiki.
Hii imekuwa tofauti kabisa na hawa wanaojiita wanasoka wa kulipwa ambao sasa wanajivuta vuta kwa ajili ya kujiandaa kwa msimu mpya.
Ama kweli, maumivu wanayopata kutokana na unyenyekevu wa wenzao wa ridhaa wanaoshiriki Olimpiki na kuzing’arisha nchi zao hayasemeki.
Wataweza tena kunyanyua vichwa vyao kwa kiburi na kujidai, wakilinganishwa na mashujaa wetu wa Olimpiki?
Sie mashabiki wa soka, tunaonyonywa na kutiwa ulevi na Ligi Kuu, tumechanganyikiwa na kuijiongoza kuamini kwamba ‘mashujaa’ wetu wa soka wamefanya kazi kubwa.
Ukweli ni kwamba tunajua mambo machafu, kama si ya aibu yanayowahusu watu hawa, ambapo kila siku lazima watambe na magari yao ya kifahari, wakiyatembeza huku na kule.
Kwa siku wanazotakiwa kwenda mazoezi, hadi kila mmoja aingie kwenye gari lake la kutesea kwa kushindana bei na aina, inakuwa imeshatinga saa 3.30 asubuhi.
Hapo mmoja mmoja, mpaka ajisogeze hadi kufika uwanja wa mazoezi inakuwa kwenye saa 4 tayari.
Basi wakishafika kwenye maeneo ya uwanja, watajidai na ndala zao kama zile za flip-flops halafu wapate kifungua kinywa.
Baada ya hapo watapiga soga zisizo na nyuma wala mbele na wenzao, wawapigie simu na kuongea na mawakala wao, kabla ya kupanga jinsi ya kutoka jioni na mambo ya ngono.
Baada ya hapo eti ndio wanashuka kwenda kwenye mazoezi ya kama saa mbili tu, na wakati mwingine eti huwa wanatoka hata jasho!
Ajabu ni huo muda wa mazoezi, kwani ikifika saa saba wameshamaliza. Hapo kila kitu kimeisha, siku yote iliyobaki wanajiamulia wenyewe cha kufanya.
Ukiacha hayo, kuna simulizi walizozoea kutoa kuhusu jinsi walivyo kwenye shinikizo nyingi.
Ikiwa wapo kwenye mashindano ya kimataifa kuwakilisha nchi zao, hapo tena ndio usiseme.
Umma unakuwa na imani kwamba wanasoka wao hawa wa kulipwa watajitolea kweli kweli kwa ajili ya nchi, lakini ukweli sivyo, hawatendi haki.
Wapo wanaokataa kabisa kuwakilisha nchi zao mpaka wabembelezwe au wajazwe kitita cha pesa na wapo wanaoingia kwenye kambi na hata kucheza lakini hawafanyi chochote.
Nawajua wale ambao hujidai kuwa na hofu ya kuumia wakiwa na timu za taifa, eti watakosa mechi ‘muhimu’ na klabu zao.
Kana kwamba hiyo haitoshi, licha ya kuwa ni wenye kusifika kila kona ya dunia na kwa vipaji walivyo navyo, wamekuwa katika wakati mgumu hata kupiga vyema penati, kufanya mahojiano au hata kuwa wachangamfu kwa washabiki wa nchi zao.
Haishangazi basi kuona jinsi wanavyogawanyika, kama si kusambaratika na kuishia kuapa na kuapiza kila wakati. Ooh, jinsi ilivyo ngumu kuwa mchezaji wa kulipwa!
Sisi washabiki tumezoeshwa kuona tabia hiyo ni ya kawaida, huku ‘mashujaa’ wetu wakiona ni kitu cha kawaida kutia mfukoni kiasi cha Pauni 150,000 kwa wiki.
Tunawaheshimu, kitu ambacho wanakipenda sana, tena wengine wanadai, wakidhani kwamba ni haki yao.
Bahati mbaya sana ni kwamba, baada ya yote haya, baadhi yetu tumeishia kuwachukulia kama mfano wa kuigwa.
Ee Mungu, tungedanganywaje namna hiyo? Lakini sasa, tunaishukuru Olimpiki, kwa sababu sasa macho yetu yamefunguka.
Wavulana na wasichana watanashati hawa wanyenyekevu, wasio na uchu wala uchoyo wametuonesha jinsi gani wanamichezo wanavyotakiwa na wanavyoweza kuwa.
Kwa miaka minne, wengi wao wamekuwa wakiamka saa 11 alfajiri, wakitoka nje na kukumbana na giza na baridi.
Mara nyingi wanajihimu hivyo wakiwa peke yao, bila kishawishi cha fedha, bila kutiwa moyo sana, bila umaarufu, bila washabiki, bila makundi wala kuwekewa usalama.
Na bado, ni wanyenyekevu hawa walioonesha uzalendo ambao wameishia kwa uzuri, wakiwa wanadamu wenye kuhusudiwa, lakini pia wenye mafanikio zaidi.