Menu
in , ,

Mashindano ya Olimpiki yanatuumbua watanzania

Timu ya Tanzania katika michezo ya kimataifa

Mtu mwingine atajiuliza ni kwanini tuendelee kujifunza bila kuhitimu?

MASHINDANO ya kimataifa ya Olimpiki yanaendelea nchini Brazil na kushirikisha mataifa mbalimbali kote duniani bila kujali rangi, kabila, nguvu za uchumi na kadhalika. Mashindano hayo yamekuwa na mvuto wa kipekee karibu kila mwaka.

Kwanza hushirikisha michezo mbalimbai ikiwemo soka, kikapu, riadha, kurusha tufe, kurusha mkuki, mpira wa pete, kuruka vihunzi, kuruka juu na chini. Michezo inayoshirikisha inakuwa mingi mno kiasi kwamba watanzania wanaweza kuchagua mchezo wa kushiriki.

Mashindano hayo yameshuhudia mastaa wa soka kama vile Neymar Junior wa Brazil ambaye anaongoza kikosi cha nchi yake katika mchezo wa soka kwa wanaume.

Aidha mashindano hayo hushirikisha mpira wa miguu kwa wanawake ambao wameongeza mvuto mkubwa duniani kuliko miaka ya nyuma.

Mashindano ya mwaka huu yamefanyika katikati ya maandamano ya kisiasa, ambapo raia kadhaa wa Brazil waliandamana.

Pamoja na mambo mengine mashindano haya kama livyo desturi yamekuwa somo jingine kwetu. Somo hili linazidi kuota mizizi kiasi kwamba watanzania tumekuwa watu wa kujifunza kila wakati.

Mtu mwingine atajiuliza ni kwanini tuendelee kujifunza bila kuhitimu? Kwamba watanzania tunatumia muda mwingi kujifunza kuliko kuhitimu na kuonyesha uwezo wetu mbele ya dunia.

Mashindano ya mwaka huu yamenikumbusha yale ya Ubingwa wa dunia ya IAAF chini ya miaka 20 yaliyofanyika nchini Poland.

Kwenye mbio za mita 5, 000 zilinishangaza mno nilipoona mshindi wa pili akiwa ni Djamal A. Direh raia wa Djibouti. Mshindi wa kwanza wa mbio hizo alikuwa Seleman Barega kutoka Ethiopia, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Wesley Ladema raia wa Kenya.

Kwa upande wao Kenya na Ethiopia tumezoea kuwa wao ni washindani wa siku nyingi kwenye mashindano mbalimbali. Wamekuwa wakitamba kwenye riadha katika mashindano ya kimataifa iwe IAAF au Diamond League za Paris, London, Stockholm na kwengineko.

Djamal A. Direh ndiye mwanariadha aliyenivutia. Kwanza anatoka nchi ambayo haina sifa ya amani na utulivu. Djibouti ni nchi inayosifika kwa ukame, ukosefu wa amani, ukosefu wa demokrasia na haina uchumi mzuri kuizidi Tanzania.

Kimsingi Tanzania inaizidi mambo mengi sana nchi ya Djibouti. Lakini Djibouti safari hii imeibua mshindi ambaye anazidi kutuletea somo.

Twende kwenye mashindano ya Olimpiki ya mwaka huu nchini Brazil hususani katika jiji la Rio De Janeiro kuna vipaji vingi sana chipukizi na wachache ni wakongwe.

Kwenye soka la wanaume sheria inasema washiriki wawe na umri wa chini ya miaka 23, kisha wanaongezwa wakongwe wasiozidi watatu.

Katika mashindano hayo hata kwenye riadha tumeshuhudia vijana wengi chipukizi wakipewa nafasi yao ya kushindana.

Swali tunalotakiwa kujiuliza ni moja; hivi tunachokifanya kweye michezo ni kipi? Kwasababu hata mashindano ya nyumbani tumekuwa wavivu na hatuna ufanisi tangu kuondoka kwa kizazi cha akina Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na wengineo.

Mashindano ya mwaka huu pia tumeona taifa la Jamaica linatumia kama fursa kutangaza vipaji vyao vipya. Jamaica hawamtegemei Usain Bolt au Yohane Blake peke yao bali kuna vipaji vingi mno amnavyo vinawaletea sifa na kukuza uchumi.

Kwenye mashindano ta riadha ya kupokezana vijiti pia hatukuwepo kabisa. Mtu unabaki unajiuliza katika nchi yetu tumefanikiwa kitu gani haswa kwenye upande wa michezo?

Kwenye Olimpiki hatushiriki Long Jump, High Jump, kurusha tufe, mbio za mita 100, 200, 400, wala 800. Tumejipa jukumu la kutegemea mbio ndefu kama mita 1500, 3,000, 5,000 na 10,000, lakini bado hatujawa tishio.

Hatupo kwenye riadha ya mita 100 kupokezana vijiti, wala mita 200 au 400 za vijiti. Olimpiki imetuonyesha vipaji vingi vipya na washiriki baadhi yao ni makinda. Lakini sisi hadi leo hatuna makinda waliotayarishwa kuanzia ngazi za chini hadi juu.

Tumeishia kukumbatia migogoro. Tumekumbatia siasa na blah blah saa 24 za siku kwa wiki. Hakuna chama cha siasa chenye kutengeneza programu ya kuibua vipaji kwenye michezo.

Tumebaki na blah blah za kutegemea Ilani za uchaguzi ambao ni soga za kila baada ya miaka mitano. Tumekuwa taifa la ajabu sana, maneno mengi utekelezaji sifuri. Na hata tukitaka kutekeleza tumeweka utitiri wa ‘vikwazo’ usio na tija kwa nchi ilimradi tunakomoa tu. Nchi inaumwa hii, huwezi kusitisha michezo kwa kisingizio kuwa ‘watoto watasoma saa ngapi’. Ufinyu wa fikra na kutotambua faida za kiuchumi zitakanazo na michezo.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version