Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki nchini Ndugu Filbert Bayi alikaririwa na vyombo vya habari kuhusu kushiriki kwa Tanzania katika mashindano hayo makubwa Duniani ambayo kwa mara ya kwanza yatashirikisha vijana kati ya umri wa miaka 14 hadi 18. Labda kwa wengi wasiofahamu, mashindano haya ya aina yake ni mawazo ya Rais wa Kamati ya Olimpiki Duniani Mbelgjji Jacques Rogge ambayo yalikubaliwa na kupitishwa kwa kauli moja na wajumbe wote wa Kamati hiyo July 05, 2007 kule mjini Guatemela City. Mji wa Singapore ambao ndio utakuwa mwenyeji wa michezo hiyo kwa mara ya kwanza na ulitangazwa rasmi mapema mwaka 2008. Takribani miaka miwili sasa , je Tanzania tumejitayarisha vipi na michezo hiyo? Kufuatana na kauli ya Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki nchini Tanzania inataraji kutuma timu ya watu wane ikiwemo ya Riadha na Kuogelea Sio vibaya kuelewa lengo na madhumuni ya Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa- International Olympic Committee kuendesha mashindano ya Olimpiki ya vijana Duniani.Kama mdau naona malengo makuu ya kuendesha mashino haya ni (1) – Kuwakutanisha wanamichezo vijana hodari pamoja. (2) – Kuwapa ufahamu mkubwa katika masuala ya Olimpism (3) – Kuwapa fursa ya kujadili na kuelewa umuhimu wa Olimpisim katika jamii. (4) – Kushirikiana katika tamaduni mbalimbali Duniani (5) – Kuwafikia vijana kote Duniani kupitia itikadi za Olimpisim (6) -Kuinua mwamko wa vijana kimichezo (7) – Michezo hii kufanywa jukwaa kwa vijana kusambaza maadili ya Olimpism (8) – Muendelezo wa michezo inayotayarishwa kwa hali ya juu. Michezo hiyo inatarajiwa kuwashirikisha wanamichezo 3,600 na viongozi wasiopungua 800. Kamati zote za Olimpiki toka nchi 205 zinataraji kushiriki michezo hiyo ya kwanza Duniani kufanyika. Kila nchi imepatiwa nafasi nne hata kama wanamichezo wako wameshindwa kufikia viwango walivyoweka. Kwa maana hiyo mashindano hayo utakuwa mkusanyiko mkubwa sana kwani kila nchi itakuwepo Singapore kuanzia August 14 hadi August 26 2010. Pamoja na ukweli michezo hii itaendeshwa chini ya sheria na kanuni za Olympic Charter bado wadau wengi wanadai kuwa michezo hii inaweza kuwajenga au kuwabomoa vijana wetu. Binafsi nilihudhuria kongamano la uendeshaji wa michezo hiyo mjini Olimpia Greece hivi karibuni. Wajumbe wengi walitaka World Anti Doping Code isitumike kwa hawa vijana kwani inaweza kuwakatisha tamaa katika maisha yao yote. Baadhi ya wajumbe walidiriki kudai hata nyimbo zao za Taifa zisipigwe kwa washindi bali Olympic National Anthem itumike wakati wote wa kutoa zawadi kwa washindi. Nini sababu za kudai hivyo. Baadhi ya wadau walidai kuwa vijana ni rahisi kusononeka au kuwa na msongo mkubwa pale aonapo nchi yake imeshindwa vibaya Kwa upande wa matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu baadhi ya wajumbe walidai bado kuna haja ya kufanya hivyo kutokana na ukweli kuwa baadhi ya makocha wanaweza kutumia fursa hiyo kwa kuongeza nguvu vijana kwa madawa tofauti wasiyoyaelewa. Hata hivyo michezo hiyo kidogo itakuwa tofauti kidogo ili kutoa ushindani mkubwa . Mathalani kwa mfano katika mpira wa kikapu – Basketball michezo hiyo itashirikisha wachezaji watatu watatu katika nusu ya uwanja wa kawaida wa mchezo huo. Katika baadhi ya michezo wachezaji wa jinsia tofauti watashirikishwa pamoja. Mfano wa michezo hiyo ni kama kuogelea (relay), table tennis na tennis. Kuhusu umri , michezo hiyo itashirikisha wanamichezo walio katika umri wa miaka 15,16,17na 18 tu hadi ifikapo December 2010 Wanamichezo pia watapangwa kufuatana na umri wao ili kutoa nafasi nzuri ya ushindani. Kama nilivyosema hapo awali kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazoshiriki michezo hiyo Je tumejiandaa vipi? Hivi karibuni wakati Rais Jakaya Kikwete akipokea kifimbo cha Malkia Queens Relay Baton katika viwanja vya Ikulu aliwaasa viongozi wa michezo kuwa wakati wa visingizio kushindwa kwa timu zetu umekwisha. Ukweli ni kauli nzito toka kwa Kiongozi wa nchi. Bado naamini hatujachelewa kuandaa vijana wetu ukuitilia maanani wengi wao wako katika mazoezi mazito hivi ndani na nje ya nchi. Hata hivyo bado watahitaji mafunzo maalum ya wataalamu wa saiklojia ili wafanye vizuri zaidi Kutokana na ukweli kuwa nchi nyingi zitashiriki kutokana na nafasi nne za upendeleo kama sisi basi kuna uwezekano mkubwa wa sisi kufanya vizuri kama tutajiandaa vyema Kufanikiwa medali yoyote katika michezo hiyo basi ni ishara njema kwa timu zetu katika michezo ya Jumuia ya Madola – Commonwealth Games October mwaka huu kule New Delhi India. Na hata Olympic Games kule London 2012 kule London Uingereza. ..
Mchume muharam [mchumem@yahoo.com]