Si kitu rahisi kutokea tangu yalipoanzishwa mashindano hayo. Lakini kwa sasa nakiri kuwa mashindano ya Jumuiya ya Madola yameshuka thamani kubwa kuliko awali. Ingawa kila mmoja ana mtazamo wake, lakini nina ushahidi mkubwa mno.
Kwanza nilianza kuona kwenye mashindano ya Diamond League ya England ambapo wanariadha wakiongozwa na Usain Bolt walikataa kushiriki ikiwa ni siku chache kabla ya kumalizika kwa mashindano ya Diamond League ya Paris, Ufaransa.
Bolt alisema wazi kutokana na makato makubwa ya kodi hakutaka kushiriki mashindano ya Diamond League ya England. Bahati nzuri michezo ya Jumuiya ya Madola imefanywa katika taifa la Uskochi(Scotland) ambalo ni sehemu ya Muungano wa Uingereza.
Kwa vyovyote vile mashindano haya nilitarajia yangelikuwa na umashuhuri ule wa awali, lakini hali imekuwa tofauti mno. Leo naandika nikiwa baada ya kutazama ufunguzi wake, na napokea kwa masikitiko kujitoa kwa Mo Farah.
Sababu alizotoa ni moja tu imekuwa muhimu, kujiandaa na mashindano ya Ulaya. Lakini ile sababu ya kiafya nadhani ni kushamirisha hoja yake ya kufanya maandalizi ya mashindano ya riadha ya Ulaya kuliko Jumuiya ya Madola.
Wanariadha wengine mashuhuri waliojitoa ni Tohan Blake, Usain Bolt ambao ni marafiki hawa na wamekuwa wakichukua uamuzi wa pamoja. Walipojitoa mashindano ya Diamond League ya England wakasubiri Diamond League ya Stockholm kule Sweden.
Yohan Blake alishiriki, lakini Usain Bolt alikuwa majeruhi. Katika mashindano ya Daegu tuliona wote hawa walishiriki na Usain Bolt alisononeshwa kutolewa kwa kadi nyekundu.
Mwanariadha wa kike na hodari Shelly-Ann Fraser-Pryce ameyakacha mashindano ya Jumuiya ya Madola, ikiwa na maana ameugana na kaka zake Blake na Bolt wote kutoka Jamaica.
Yohan Blake amesema wazi anajiandaa mashindano ya Olimpiki mwaka 2016, hii ikiwa na maana haoni umuhimu wa michuano ya Madola. Blake anao mwaka mzima wa kujiandaa wa 2015, lakini kwake Olimpiki ni muhimu zaidi kuliko Madola.
Ni ujumbe tosha. Jambo la mwisho ni kwamba michuano ya Jumuiya ya Madola inaelekea haina fedha. Haishawishi wanamichezo nguli, matokeo yake imekuwa michuano ya chipukizi na wachezaji wanaoichukulia kama sehemu ya ushindani.
Mvuto wa mashindano hayo umeshuka kwa kasi sana. Labda hakuna fedha za maana, hilo naliona bayana.