EPL na EFL
Nimesoma ripoti za vyombo vya habari mbalimbali hadi jumanne wiki hii ilieleza jumla ya watu 1,937 wamefariki dunia kati ya Oktoba 31 hadi Novemba 6 kutokana na kuugua ugonjwa wa corona nchini England, lakini taarifa nyingine zimebainisha kuwa upo mpango wa kuruhusu mashabiki kuingia viwanjani kabla ya sherehe za krismasi. Kwamba matumiani ya mashabiki kuingia viwanjani msimu huu yangalipo, licha ya wasiwasi kuwa huenda ungeisha bila kuwaona wakitamba viwanjani.
Imeelezwa kuwa serikali ya England imepokea mapendekezo kutoka kwa wataalamu wa michezo kutengeneza utaratibu maalumu ambao utawezesha mashabiki kuingia viwanjani kushuhudia timu zao zikicheza.
Mpango huo umewasilishwa serikalini kupitia wizara ya habari,utamaduni na michezo huku kukiwa na matumaini waziri mkuu Boris Johnson atakubaliana na muundo mpya baada ya kuzuia mashabiki kuingia viwanjani tangu mwezi machi mwaka huu.
Kwamba kutakuwa na maeneo mawili; mashabiki wanatakiwa kutengewa maeneo maalumu ya pande mbili ambapo watakaa bila kukaribiana. Hata hivyo upo uwezekano pia baadhi ya viwanja vikakosa mashabiki kutokana na mapendekezo yaliyowasilishwa ikiwa majukwaa yatabaki kama yalivyo sasa.
Wizara hiyo imekuwa ikikosolewa kwa muda mrefu kutokana na kushikilia msimamo wake kuzuia mikusanyiko mitaani na viwanjani hali ambayo imevinyima vilabu vingi mapato kwakuwa mashabiki hawakuruhusiwa kuingia viwanjani.
Utaratibu wa umbali wa kukaa kati ya shabiki mmoja na mwingine na kudhibiti idadi ya mashabiki wa kuingia uwanjani ni miongoni mwa vigezo vinavyozingatiwa. Utaratibu huo ulifanyiwa majaribio mwezi Agosti mwaka huu na klabu ya Brighton ilipomenyana na Chelsea kwenye uwanja wa Amex.
Inasemekana wizara imetoa muongozo mpya kuwa ukaaji wa mashabiki uwanjani lazima uzingatia hatua moja au mbili na wanatakiwa kvaa barakoa.
Hata hivyo haijajulikana kwa njia ipi itatumika kuingiza mashabiki wachache uwanjani. Mkanganyiko mwingine ni pale mashabiki watakaporuhusiwa kuingia kumbi zilizopo karibu na milango ya uwanja unaochezwa mchezo.
EPL si pekee iliyokumbwa na janga la corona hata Ligi zingine barani Ulaya zimekumbwa na tatizo hilo. Hii ina maana vilabu vimepoteza mapato, watu wamepoteza kazi na taharuki ya kijamii imekuwa kubwa. Mashabiki wa Bundesliga nchini Ujerumani walitakiwa kuingia viwanjani kabla ya kubadili uamuzi huo mapema mwezi uliopita baada ya kuongezeka idadi ya wagonjwa na vifo.
Mapema jumanne wiki hii shirikisho la soka nchini Ufaransa nalo limeambiwa na serikali kuwa hakuna ruhusa mashabiki kuingia uwanjani kipindi hiki, badala yake watapewa ruhusa hiyo mwanzoni mwa Januari 2021.
Wakati EPL yakichukuliwa maamuzi ya kurejesha mashabiki viwanjani kwa utaratibu maalumu, watanzania ni miongoni mwa walioathiriwa nao. Barani Afrika uamuzi wa Shirikisho la soka CAF kupanga mechi ya Tanzania na Tunisia saa 4 usiku ulilenga kupunguza idadi ya mashabiki kuingia uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam. Lengo la kupanga mechi muda huo ni kufuata muongozo wa Shirikisho hilo kuchukua tahadhari zote za maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Nchini England majadiliano ya namna kuingiza mashabiki viwanjani ndicho kitu kinachojadiliwa zaidi hususani kabla ya krismasi lakini hakuna uhakika. Kukosekana uhakika huo kunazidi ‘kuwaweka jela’ mashabiki na kuwa na kiu ya kuvinjari tena viwanjani.
Mashabiki ambao walizoea kuimba na kutamba mbele ya wachezaji wao, Kuwazomea wapinzani wao na kuleta hamasa kwa wachezaji wao imekuwa adimu kwa kipindi cha miezi 7 sasa.
Kila mbinu inayopangwa kuwarejesha mashabiki imekuwa ikikumbana na kikwazo cha mlipuko mpya wa maambukizi ya corona. Badala ya idadi ya wagonjwa na vifo kupungua, hali inakuwa tofauti kila uamuzi wa kufungulia mashabiki unapokaribia, ndiyo maana serikali zinafanya kazi za kuahirisha mara kwa mara.
Tishio la ugonjwa huu limekuwa chanzo cha kudorora hamasa ya Ligi mbalimbali barani ulaya na kwingineko duniani. Si Ligi pekee bali hata mashindano kama vile Ligi ya Mabingwa Afrika na mengineyo ambapo michezo imechezwa bila mashabiki.
Naamini hata leo mashabiki wakiruhusiwa ni lazima idadi yao idhibitiwe kama mapendekezo ya wizara ya michezo ya England inavyosema. Ugonjwa huo utabadili tabia za mashabiki na pia unaweza kupunguza mashabiki bila hata masharti ya serikali kwa sababu watu watachukua tahadhari wenyewe kabla ya kuzuiwa milangoni na mamlaka zianzohusika.
Kwamba itakuwa dhana ya pili ya mashabiki kujiweka jela baada ya kuwekwa na mamlaka zinazohusika na michezo. Wasiwasi huo unaweza kuchangia kushuhudia msimu unamalizika bila mashabiki viwanjani lakini litakuwa pigo kwa timu nyingi sana.