Chama cha Soka (FA) kimemwadhibu mshambuliaji wa kati wa Liverpool, Mario Balotelli kwa kumtoza faini ya pauni 25,000 na kuzuiwa kucheza mechi moja.
Adhabu hiyo inatokana na kuchapisha katika mtandao wa jamii maneno ya kibaguzi na lugha ya kuudhi, kinyume na kanuni za soka, na sasa anaikosa mechi muhimu dhidi ya Arsenal Jumapili hii.
Balotelli (24) aliyepata kuzichezea AC Milan ya Italia akitoka Manchester City amekuwa katika ukame wa mabao, kwani amefunga mawili tu katika mechi zake 15 akiwa Anfield. Inadaiwa kwamba majuzi kocha Brendan Rodgers alihoji iwapo mchezaji huyo kweli ana thamani ya pauni milioni 16 alizomnunua nazo.
Mtaliano huyo pia ametakiwa kuhudhuria kozi ya elimu, ambayo labda itamsaidia kubadilika tabia, kwani amekuwa na mambo yasiyo ya kawaida, ikiwa ni pamoja na kuchoma bafu yake baada ya kuwasha fashifashi, kupasi nguo huku akisikiliza muziki, akicheza na kusoma kitabu cha Zlatan Ibrahimovic kwa wakati mmoja.
Maneno aliyoandika yalikuwa juu na chini ya picha ya Super Mario yakisema: “Usiwe mbaguzi! Kuwa kama Mario. Yeye ni fundi bomba aliyeelimishwa na Wajapani, anazungumza Kiingereza na mwenye mwonekano kama raia wa Mexico…ruka kama mtu mweusi, nyakua sarafu kama Myahudi.”
Balotelli alishakiri kosa hilo, lakini akasema alidhani alikuwa anachapisha utani tu, na baada ya adhabu akasema anasikitika kwamba wachezaji wenzake na washabiki wa Liverpool wanaadhibika kwa kitu alichofanya yeye, akasema nia yake ni kutekeleza uamuzi wa FA na kuhakikisha harudii tena makosa hayo.
Msemaji wa Liverpool alisema wamepokea uamuzi wa FA, watautafakari na watakachoamua wataeleza baada ya kusoma hukumu yenyewe, na hata kama kuna hatua za kinidhamu dhidi ya Balotelli ni suala baina ya klabu na mchezaji huyo mtukutu.