CHAN
MAJINA ya waamuzi watakaochezesha Mashindano ya Soka kwa Mataifa ya Afrika yanayohusisha wachezaji wanaocheza Ligi za ndani yametajwa. Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika nchini Cameroon kwa mwaka 2021.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyofuzu na tayari Kocha wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije ametaja kikosi chake ambacho kinaelekea nchini Cameroon hivi karibuni.
Hata hivyo mjadala mkubwa umeibuka nchini baada ya orodha ya waamuzi waliotajwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF.
Orodha ya marefa waliotajwa na CAF hakuna hata mmoja kutoka Tanzania hali ambayo imeibua mjadala mkali juu ya mwenendo wao. Kinachoshangaza ni kwamba waamuzi wa Tanzania wamekuwa na fursa ndogo ya kuchezesha mashindano makubwa barani Afrika.
Mashindano ya Mataifa ya Afrika yaani CAN ambayo hujumuisha wachezaji wa ligi zote barani humu hayajawahi kutoa fursa kwa waamuzi wa Tanzania kuchezesha mechi zozote.
Si CAN wala CHAN marefa wa Tanzania wamekuwa na nafasi finyu kupenya katika eneo hilo nabado mjadala unazidi kutanuka na kufanya tathmini juu ya ufanisi wa waamuzi wetu.
Ilitegemewa kuwa CHAN ni sehemu ambayo waamuzi wengi wangeweza kutumia kupanda daraja la uchezeshaji wa mashindano ya CAN.
Licha ya baadhi ya waamuzi kupenya katika hadhi ya beji ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA lakini hali imekuwa tofauti linapokuja kwenye mashindano makubwa.
Wengi hawana nafasi, hawateuliwi. Mashindano ya ngazi za vilabu mfano Ligi ya Mabingwa tumeona waamuzi kutoka hata mataifa ya Djibout, Sudan, DR Congo, Somalia ambayo yametawaliwa na vurugu na vita vya wenyewe kwa wenyewe lakini wanapenya na kuonesha umahiri wao kwenye mashindano mbalimbali.
Mashindano ya Kombe la CAF nayo huwaoni waamuzi wa Tanzania wakitamba. Mashindano ya All Africa Games yanapofanyika huwezi kuwaona waamuzi wa Tanzania wakitamba. Mashindano ya Olimpiki huwezi kuwaona waamuzi wa Tanzania wakitamba. Mashindano ya Fainali za Kombe la Dunia huwezi kuona waamuzi kutoka Tanzania wakifanikiwa kupenya walau hata kuwa washika vibendera.
Marefa wetu Tanzania wameishia kuchezea mechi za CECAFA, Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Kuu Zanzibar, Chalenji na hata kupata mwaliko wa kuchezesha mashindano ya COSAFA ambayo Tanzania inaalikwa mara kwa mara hakuna nafasi hiyo.
Mechi wanazopata marefa wa Tanzania kuchezesha ni zile ambazo haziwapi nafasi ya wao kutengeneza umahiri wao. Kwahiyo kama hizo mechi ndogo ndogo wanashindwa kujitengenezea sifa za umahiri ni wapi sasa watafanikiwa kufanya hivyo?
Shirikisho la soka CAF katika mashindano yake limekuwa likiwaondoa waamuzi wa Tanzania. kwamba kila mashindano yanapowadia mfano CHAN, AFCON,CAF, CAFCL,Shirikisho na Super Cup hakuna nafasi kwa waamuzi wa Tanzania. mataifa ambayo yanatamba ni yale ya Afrika magharibi, kusini mwa Afrika ambako Afrika kusini imekuwa kinara na umahiri wao umeonekana wazi wazi.
Kushindwa kufurukuta kwa waamuzi wetu kunaleta maana kuwa wanachezesha vibaya, hawana viwango ni sawa na kusema Ligi Kuu Tanzania bara haina waamuzi wenye ubora. Ligi Kuu Tanzania inachezeshwa na waamuzi wabovu na wasioweza kutafsiri shieria.
Ligi Kuu Zanzaibar nayo inachezeshwa na waamuzi wabovu, Kombe la Mapinduzi linachezeshwa na waamuzi wabovu. CECAFA huwateua waamuzi wabovu wa Tanzania kuchezesha mashindano yake. nayo TFF inaonekana inalea waamuzi wabovu. Chama waamuzi nacho kitaonekana kina wanachama ambao ni waamuzi wabovu.
Picha ya namna hii inakwenda mbali zaidi. Sisemi kuwa ni lazima kila nchi iwe na waamuzi kwenye mashindano ya Soka barani Afrika lakini angalau waamuzi wetu wangeliweza kutamba miaka ya nyuma na sasa tungepunguza kuwajadili kwa namna hasi na kuwapachika majina kuwa ni wabovu.
Katika hisia za kawaida za mwanadamu mambo hayo yanapotokea unaweza ukacheka lakini hili halichekeshi. Linaumiza, linafikirisha, waamuzi wa Tanzania wanapaswa kujitathmini ni wapi wanapofeli na namna gani wanaweza kuchezesha mashindano makubwa kama AFCON,CHAN,CAFCL kwa bara la Afrika na duniani.
Hisia zingine ni kwamba waamuzi wanaovaa beji za FIFA bado wameshindwa kuzitendea haki. Ni kwamba CAF inaona FIFA imetoa beji kwa waamuzi wabovu wasio na sifa ya kuchezesha hata michuano ya ndani ya Afrika ya CHAN. Kwa namna nyingine mtu anawez akutafakari hizi Beji za FIFA walizopewa waamuzi wetu zina maana gani katika vifua vyao ikiwa wametemwa hata.
Je, waamuzi wetu kweli hawawezi kuchezesha hata mashindano ya CHAN? Kama jibu ni hapana, basi tuambiwe tatizo ni wao kuwa mizigo ama nini? Kama jibu ni ndiyo, ina maana waamuzi wetu wamekubali kuwa wao ni mizigo?
Ukanda wetu wa Afrika mashariki umewahi kuwa na mwamuzi bora kabisa Charles Kasembe wa Uganda. Refa huyo alikuwa mahiri na aliwavutia wengi kila alipochezesha mechi alizokabidhiwa.
Tatizo pekee la Charles Kasembe lilikuwa kutumia diplomasia kupindukia kuliko kuchukua uamuzi wa kudhibiti mchezo. Yaani alikuwa anapiga maneno mno kujaribu kutuliza wachezaji.
Ni kweli Kasembe alipendwa na wachezaji, alijua kudhibiti presha ya mchezo lakini lilipofika suala la uamuzi mkali uliopo ndani ya sheria anazosimamia alikuwa hachukui hatua hizo badala yake alikuwa akitumia diplomasia zaidi.
Mwamuzi huyo ameknikumbusha yule aliyechezesha pambano la Simba na FC Platinum kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam, aliwahurumia sana Wazimbabwe na kwa namna fulani alitumia diplomasia zaidi kuliko kuchukua uamuzi ulioko kwenye sheria za soka. alijikuta anajadiliana na wachezaji mara kwa mara badala ya kutoa adhabu pale mamlaka yake yanapoingiliwa.
Charles Kasembe alikosa nafasi ya kuchezesha mashindano makubw aya CAF sababu ilikuwa hii. Mojawapo ilikuwa michezo ya fainali za AFCON wakati ule zikiitwa CAN. Hata kama alitaka kuwa kama PierLuigi Colina.
Tangu hapo walikuwepo akina wengine hapa Tanzania lakini hawajawahi kufurukuta ngazi za kimaaifa. Tatizo linakuwa nini? Na kwama sasa hata mashindano ya ndani ya Afrika CHAN waamuzi wetu wamekosa nafasi, inaleta maswali mengi.
Sisemi CHAN inatakiwa na waamuzi wabovu lakini ni mhali ambako marefa wetu wangeweza kuonesha umahiri wao. Hata hivyo wataoneshaje umahiri ikiwa hata kuchezesha michuano hiyo ya ndani hawajafikia ubora unaotakiwa na CAF?
Je ndio watapata nafasi za kuchezesha mashindano makubwa kama Olimpiki au Fainali za Kombe la Dunia kila zinapowadia? Vinginevyo tuseme marefa wetu ni mizigo, lau kama sio basi watuoneshe kwa vitendo hadi wachaguliwe kuchezesha mashindano ya kimataifa.