Mlinzi Marcos Rojo aliyesajiliwa Manchester United kutoka Sporting Lisbon ya Ureno anakabiliwa na shauri la jinai kwao Argentina, na ndilo linamzuia kuanza kuchezea timu yake mpya.
Hadi Jumapili hii asubuhi alikuwa hajapatiwa visa ya kumwezesha kufanya kazi nchini, kutokana na madai kwamba ana kesi ya jinai ya kupigana na jirani nchini Argentina tangu 2010 ambayo bado ipo kwenye majalada ya polisi.
Rojo (24) alikamilisha usajili kwa dau la pauni milioni 16 wiki mbili zilizopita, lakini upelelezi wa vitendo vyake vya jinai unasababisha zuio la yeye kupewa visa, walau kwa muda huu, japokuwa Kocha Mkuu wa Man U, Louis van Gaal anasema ana uhakika mchezaji huyo atakuwa tayari kwa mechi dhidi ya Queen Park Rangers (QPR) Septemba 14.
Imeelezwa, hata hivyo, kwamba Chama cha Soka (FA) cha England kimeshamalizana na suala la mtu huyo wa tatu na kimetoa hati ya kumwezesha kucheza, lakini kinachosubiriwa sasa ni visa, kwani aliyoingia nayo ni ya utalii.
Hivi sasa Rojo yupo Madrid, Hispania kwa ajili ya kusubiri kuhojiwa na watumishi wa Ubalozi wa Uingereza ambao watatathmini kwa kina ugomvi aliosababisha wakati huo, na wakiona inafaa watampatia visa ya kufanya kazi nchini Uingereza.
Fernando Burlando ambaye ni mwanasheria wa Rojo, amedai kwamba mchezaji huyo aliyekuwa kwenye Timu ya Taifa ya Argentina ameshaonekana na polisi kuwa na kesi, hivyo anasubiriwa kupelekwa mahakamani, lakini akasema watalimaliza suala hilo.
Amedai hata akitiwa hatiani, anaweza kuwekwa chini ya uangalizi na kupewa adhabu ya kufanya kazi za jamii, ambazo si lazima azifanyie nchini Argentina, hivyo ataweza tu kuingia Uingereza.
Kabla ya mechi ya Jumamosi hii ya Man United dhidi ya Burnley iliyoisha kwa suluhu, Van Gaal alisema; “ni suala la muda tu. Mimi ni kocha wa klabu kubwa zaidi duniani lakini siwezi kubadili sheria.”
Baada ya mechi hiyo, akasema; “naamini kwamba tutakapocheza na QPR atakuwa ameshaipata (visa).”