Menu
in , ,

MAPYA AJALI YA CHAPECOENCE

Tanzania Sports

Ndege iliisha mafuta, rubani alidharau

*Mwanasoka aliyenusurika kurudi uwanjani

*Imeelezwa kuwa golikipa amekatwa mguu

MAPYA yanazidi kujitokeza juu ya ajali ya ndege iliyoua wachezaji wa
Klabu ya Brazil ya Chapecoense, ambapo inadokezwa kwamba ndege haikuwa
na mafuta ya kutosha, rubani alionywa mapema lakini akadharau.

Habari zinasema kwamba rubani huyo, Miguel Quiroga aliyekuwa akirusha
ndege iliyotengenezwa Uingereza aina ya Avro RJ85 aliambiwa mapema
kabisa na ofisa kwenye Uwanja wa Ndege wa Santa Cruz, Bogota ndege
hiyo ilikoruka kutoka hapo Kabla ya ajali kwamba ndege haikuwa na
mafuta ya kutosha.

Gazeti la Deber la Bolivia linasema kwamba licha ya onyo na wasiwasi
alioonesha ofisa huyo, rubani alisonga mbele na kurusha ndege kwenda
Medellin ilikoanguka. Katika mkanda uliovuja rubani huyo anasikika
akitoa onyo wakati wapo Medellin juu ya kukwama kwa mfumo wa umeme na
kukosekana kwa mafuta.

Rubani huyo alitaka kujaza mafuta eneo la Cobija kwenye mpaka kati ya
Brazil na Bolivia lakini alishindwa kwa sababu kwenye uwanja wa ndege
ulioko hapo haufanyi kazi usiku na hiyo ni kwa mujibu wa gazeti la
Brazil liitwalo O Globo. Alikuwa na uwezo wa kujaza mafuta Bgota
lakini akaamua kukatiza moja kwa moja hadi Medellin.

Mamlaka ya Anga ya Bolivia yamesitisha kwa muda kuendelea kutumika kwa
leseni za kampuni ya LaMia, ambayo ilikuwa inamilikiwa kwa pamoja na
rubani huyo na maofisa wengine wawili wa mamlaka hiyo.

Katika hatua nyingine, madaktari wamesema kwamba mlinzi wa
Chapecoense, Helio Hermito Zampier Neto (31), aliyenusurika kwenye
ajali hiyo ataweza kurudi uwanjani na kuendelea kucheza baada ya
kupona majeraha yake na upasuaji aliofanyiwa.

Helam, baba yake Neto, aliwanukuu madaktari wakisema kwamba mwanawe
ataweza kurejea uwanjani kwani yupo vyema na alichofanyiwa ni upasuaji
wa pafu, goti, kichwa na mbavu. Wamesema anaendelea vyema.

“Mwanangu anaendelea vyema na kila siku hali yake inaimarika ikizidi
kuwa nzuri. Ndio kwanza amefanyiwa upasuaji wa mguu na madaktari
wanasema atarudi kwenye soka. Tutaendelea kumuombea kwa sababu
tunamhitaji, akisharuhusiwa kutoka hospitalini tutakuwa naye karibu,”
akasema Helam.

Kuhusu golikipa Jakson Ragnar Follmann (24), madaktari wanasema kwamba
amekatwa mguu wa kulia na baada ya utafiti waliofanya wanaona kwamba
hakuna haja ya kukata wa kushoto. Mlinzi Alan Ruschel (27) amefanyiwa
upasuaji wa uti wa mgongo na inaelezwa kwamba ataweza tena kutembea
kama kawaida.

Miili ya waliokufa kwenye ajali hiyo ilitarajiwa kusafirishwa Ijumaa
hii, wengi wakiwa ni wachezaji na maofisa wa Chapecoense, waliokuwa
wakienda kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya fainali ya Copa
Sudamericana dhidi ya timu ya Medellin ya Atletico Nacional.

Nyumbani kwenyewe Chapeco, kusini mwa Brazil, mahema na vifaa
mbalimbali vimewekwa kwenye uwanja wao wa soka kwa ajili ya tukio la
Jumamosi hii. Mikanda iliyorekodiwa kwenye ndege hiyo inatarajiwa
kwenda kufanyiwa uchunguzi nchini Uingereza. Uchunguzi kamili juu ya
ajali hiyo unatarajiwa kuchukua miezi kadhaa.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version