Huu ni ushahidi kuwa Man United inataka kuondokana na pengo kubwa lililowasumbua katika safu ya ushambuliaji. Kikosi cha sasa hakina washambuliaji wenye hadhi ya Ruud van Nistelrooy, Andy Cole, Louis Saha, Wayne Rooney, Van Persie na wengineo.
KUMALIZIKA msimu wa Ligi Kuu England ni mwanzo wa hekaheka za usajili kwa ajili ya msimu ujao. Timu mbalimbali zinafanya jitihada za kusajili wachezaji waliowafuatilia, huku Manchester United ikiwa miongoni mwa zile zinazotaka kuimarisha kikosi chao. Manchester United ambayo ilikuwa kwenye mbio za mataji manne; EPL,FA,Carabao na Europa League imemaliza kwa kutwaa taji moja. Manchester United inakabiliwa na kibarua cha kuziba mapengo matano yanayowakabili kabla ya kuanza msimu mpya wa 2023/2024. Tetesi za usajili wanaohusishwa nazo, zinadhihirisha kuwa Man United wanahaha kutatua matatizo katika mapengo hayo.
Beki wa Kati
Hili ni pengo la kwanza ambalo Man United wanatakiwa kuziba. Safu ya ulinzi wa kati inawategemea Lisandro Lopez, Harry Maguire, na Raphael Varane. Taarifa zinasema Lisandro Martinez, beki wa kati wa Man United anatarajiwa kusaini mkataba mpya hivi karibuni.
Wakati hatua hiyo ikuchukuliwa inaonesha wazi Eric Bailly ambaye amerejea kutoka mkopo huko Ligue One, vilevile Harry Maguire huenda akauzwa ili kuleta beki mpya. Safu ya ulinzi ya Man United imekabiliwa na changamoto kubwa kiasi cha kumfanya kocha Eric Ten Hag kubadili mfumo mara kwa mara na kumpa nafasi Luke Shaw kucheza nafasi hiyo akitokea pembeni kushoto pamoja na Malacia.
Man United wapo sokoni kwa sasa wanawinda saini ya beki wa kati wa Napoli, Kim Min-jae ambaye anaweza kuwagharimu kiasi cha pauni milioni 51. Huu ni shahidi kuwa safu ya ulinzi ya Man United ina mapengo ambayo yanatakiwa kuzibwa haraka kabla ya kuanza msimu mpya na hasa kama wanataka kuwania ubingwa wa EPL.
Golikipa wa kisasa
Je kiwango cha mlinda mlango namba moja David De Gea kinaridhisha? Je ni sababu gani ilichangia akaachwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Hispania ilipokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022? Bila shaka kocha Luis Enrique alikuwa anatuma ujumbe mzito kwa mabosi wa Man United.
Mara kadhaa kiwango cha golikipa huyo kimekuwa kikisuasua na zaidi hachezi kama makipa wa kisasa ambao hutumika kama walinzi wa mwisho (yaani nambari tano). Mfumo unawafanya makipa wacheze eneo la walinzi wa kati, lakini De Gea si kipa mwenye uwezo wa juu wa kucheza mpira kwa miguu kama Manuel Neuer, Andre Onana,Unai Simon na wengineo.
Wasiwasi mkubwa umeibuka ikiwa golikipa huyo ataendelea kuwa nambari moja katika kikosi cha Man United ama iingie sokoni kusajili mwingine. Ingawa Ten Hag amesisitiza kuwa atabaki na kipa wake, lakini eneo hilo ni miongoni mwa pengo ambalo timu hiyo inatakiwa kuliziba ili kuimarisha uwezo.
Mshambuliaji
Marcus Rashford ni mshambuliaji mzuri ambaye anaweza kutumika katika kikosi chochote. Hata hivyo safu ya ushambuliaji wa Man United ukiondoa nyota huyo hakuna mwingine mwenye kiwango cha kuwa mbadala. Man United inahusishwa na washambuliaji wawili, Randal Kolo Muani wa Eitratch Franfurt anayekadiliwa kugharimu pauni 105 na Harry Kane kutoka Tottenham Hotspurs.
Huu ni ushahidi kuwa Man United inataka kuondokana na pengo kubwa lililowasumbua katika safu ya ushambuliaji. Kikosi cha sasa hakina washambuliaji wenye hadhi ya Ruud van Nistelrooy, Andy Cole, Louis Saha, Wayne Rooney, Van Persie na wengineo. Ten Hag anatakiwa kuwa na mshambuliaji mwenye uwezo wa kutupia mabao 20 kwa msimu ili kujihakikisha nafasi ya kushinda taji la EPL. Kinyume cha hapo pengo hilo lisipozibwa litawagharimu.
Kiungo mkabaji
Eneo la kiungo mkabaji lilipata huduma ya Carlos Casemiro ambaye alisajiliwa kutoka Real Madrid. Lakini hakuna mbadala wake mwenye kiwango cha juu na hadhi ya kucheza katika kikosi cha miamba hiyo. Ten Hag anatajwa kuwinda saini ya kiungo mkabaji wa West Ham Declan Rice ambaye amekuwa na misimu kadhaa mizuri katika kazi yake. Akiwa timu ya Taifa ya England maarufu kama Simba Watatu,
Declan Rice ameunda safu ngumu ya kiungo na Kalvin Philips. Umahiri wa Rice unajulikana na ndio sababu ya Ten Hag kutamani huduma yake. Nyota huyo anaweza kuwa mpango wa pili mzuri au kuanza sambamba na Casemiro katika kikosi cha kwanza na kutengeneza kombinenga matata ya kiungo. Man United wamekuwa na changamoto eneo hili ambalo limekuwa likiwaadhibu kabla ya ujio wa Casemiro.
Mawinga
Man United imepata kuwa na mawinga matata katika kikosi chake miaka ya nyuma. Katika kikosi cha sasa winga halisi ni Alejandro Gernacho. Kwa namna Ten Hag anavyotumia mifumo yake, anahitaji mpango mbadala wa kuwa na winga mwingine. Kwa sababu Gernancho ametumika katika mechi kadhaa kubadili matokeo na kasi yake imekuwa na mchango mkubwa kwa timu.
Nyota huyo hupendelea kucheza winga wa kushoto. Je itakuwaje ikiwa Man United watasajili winga wa kulia ambaye atakuwa akichachafya upande huo, kisha Gernacho akiteleza kwa kasi upande wa kushoto? Bila shaka hili ni pengo ambalo Man United wanatakiwa kuliziba kama wanataka kupigania ubingwa. Na hasa msimu ujao watashiriki Ligi ya Mabingwa, hivyo wanahitaji kikosi kizuri ambacho kitaendana na hadhi ya mashindano hayo.