Menu
in , , , ,

MANULA ALIWAWEKA HAI SIMBA, HUKU YANGA WAKIKOSA UMAKINI

Jana kulikuwa na mechi ya ligi kuu ya Tanzania bara, mechi ambayo kwa
kiasi kikubwa ilikuwa imebeba hisia za watu wengi.

Mechi hii huigawa nchi sehemu mbili kwa sababu timu hizi zimebeba
asilimia kubwa ya mashabiki Tanzania.

Kila jicho na sikio lilikuwa katika uwanja wa uhuru ukisubiri matokeo
ya hii mechi.

Ni kweli matazaminio ya nje ya uwanja ndiyo yanayoonekana ndani ya uwanja?

Nje ya uwanja hii ni mechi kubwa sana, kila mtu huichukulia katika
ukubwa ambao hubebana na ubora wa mechi.

Kwa nadharia ya kawaida ya nje ya uwanja mechi hii huwa ni bora ,
lakini ukiingia uwanjani kuna kitu tofauti na nadharia ambayo huwepo
nje ya uwanja.

Mechi hii ni maarufu sana lakini siyo mechi bora kama ambavyo wengi huitazama.

Mechi hii hutawaliwa na presha ya nje kwanza, presha ambayo huingia
ndani ya uwanja, na kuwafanya wachezaji wacheze kwa presha na kukosa
umakini kwa kiasi kikubwa , hivo kuondoa ladha ya mchezo husika.

Jana Yanga walipata nafasi za wazi sana lakini hawakufanikiwa kuwa
watulivu na kuzitumia nafasi hizo.

Pamoja na kukosa kwao utulivu pia golikipa wa Simba, Aishi Manula
alionesha kiwango kikubwa sana ambacho kiliwaweka Simba hai muda
mwingi mwa mchezo.

Tshishimbi alifanikiwa kwa kiasi kikubwa hasa hasa kipindi cha pili
kupoza mashambulizi ya timu ya Simba pale katikati na kuwa mtu ambaye
anaanzisha mashambulizi kupitia katikati.

Hii ilimsaidia Raphael Daudi pamoja na Buswita ambaye alikuwa anaingia
katikati akitokea pembeni kuleta uwiano mzuri eneo la katikati.

Hali hii iliwanyima raha kina Kotei, Muzamiru na Niyonzima.

Kotei alikuwa akijitahidi kuzuia kwa kiwango kikubwa lakini
hakufanikiwa ku icommand timu hali iliyofanya Simba hasa hasa kipindi
cha kwanza isiwe na uwezo wa kusogea sana.

Baada ya Mkude kuingia alifanikiwa ku i command timu kwa kiasi kikubwa
na ikawa inasogea katika eneo la Yanga zaidi.

Kuingia kwa Mkude kulitosha kuonesha kuwa alihitajika kwa kiasi
kikubwa katika hii mechi.

Niyonzima ni kipenzi na roho ya viongozi na mashabiki wa simba ,lakini
siyo kipenzi na roho ya timu uwanjani.

Hana madhara makubwa ya moja kwa moja , anapiga pasi nyingi ambazo
hazina faida kwenye timu.

Hana jicho la kupiga pasi za madhara, na hiki ndicho kiliwagharimu Simba.

Alikosekana mtu ambaye angeweza kutengeneza nafasi nyingi za magoli au
kufunga akitokea katikati ya uwanja.

Kwangu mimi Mohamedi Ibrahim au Said Ndemla wana madhara makubwa
kuzidi Haruna Niyonzima lakini hawaaminiwi kuanza.

Golikipa wa Yanga hakuwa makini kwenye kuokoa mpira ule wa juu kwa
sababu hesabu zake hazikuwa nzuri ingawa alikuwa na uwezo wa kuokoa
mpira ule vizuri bila kuleta madhara yoyote yale.

Safu ya ulinzi ya Yanga imeimarika kwa kiasi kikubwa.

Dante amekuwa akicheza vizuri na Yondani. Kuna maelewano mazuri kati yao.

Kama ilivyo kwa Yanga, pia kwa Simba safu yao ya ulinzi ilikuwa na
maelewano makubwa ingawa jana ilipewa mzigo mzito, kwani safu ya
kiungo iliruhusu mashambulizi mengi lakini Mwanjali na Jurko
walisimama imara.

Ajib alikuwa amekamatwa, na hii ni kwa sababu kwa mechi za hivi
karibuni alionekana kama mchezaji hatari kwenye kikosi cha Yanga.

Kukamatwa kwa Ajib kulimfanya Chirwa awe huru, uhuru ambao
ulisababisha madhara kwa Simba.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version