*Kocha McDermott aachia ngazi Reading
Manchester United wanatarajia kuongeza shinikizo ili kumpata tena mchezaji wao wa zamani, Cristiano Ronaldo kutoka Real Madrid.
Inasemekana kilifanyika kikao kizito mwishoni mwa wiki kati ya maofisa wa Man U na Nike, kampuni inayomdhamini Ronaldo kwa viatu na mambo mengine.
Nike hawapendezwi kuona Ronaldo akitangaza bidhaa za kampuni shindani kama Adidas na nyinginezo klabuni Real Madrid, hivyo wanataka kuona akijiunga na klabu kubwa inayovaa nembo zao.
Fitna inayogharimu pauni milioni 75 inaelezwa ilitengenezwa ili kumng’oa mpachika mabao huyo mahiri wa Bernabeu, lakini hakuna uhakika wa kufanikiwa.
Kocha Alex Ferguson ameshasema angependa kumrejesha Ronaldo Old Trafford alikoondoka 2009 na Ronaldo mwenyewe amekuwa akieleza mapenzi yake kwa timu na heshima kwa Ferguson.
Hata katika mechi ya wiki iliyopita jijini Manchester ambapo Real Madrid waliwafunga Manchester United 2-1, Ronaldo hakushangilia bao lake.
Zipo habari kwamba Ferguson alikutana na kocha wa Real, Jose Mourinho ‘The Only One’ kwa karibu saa nzima baada ya mechi, ambapo Mourinho alidai United walistahili ushindi.
Uwanjani, Mourinho alikwenda kumnong’oneza jambo Sir Alex, kitu kilichostafsiriwa kwamba huenda naye anatafuta kumrithi Mskochi huyo, kwa vile mambo yake Bernabeu si mazuri sana msimu huu.
Hata hivyo, mipango ya Ronaldo kurejea Manchester zilielekea kuzngwa na ofisa mwandamizi wa Real Madrid aliyepata kuwa mshambuliaji, Emilio Butragueño.
Katika kupoza hali ya hewa Madrid, Butragueño mwenye sauti kubwa hapo, amekaririwa akisema Ronaldo mwenye umri wa miaka 28 anafungwa na mkataba wake hadi 2015, na viongozi wanapenda abaki, kwani wanafurahishwa na kazi yake.
Katika tukio jingine, kibarua cha kocha wa Reading, Brian McDermott kimeota majani, katika mazingira yanayoonesha kwamba amelazimishwa kujiuzulu.
McDermott (51) ndiye aliyewaongoza Reading kupanda daraja msimu uliopita, akachaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi hivi karibuni, lakini tangu hapo timu yake imepoteza mechi nne mfululizo.
“Mmiliki Owner Anton Zingarevich anamshukuru Brian kwa kazi yake. Utafutaji wa kocha mpya unaanza mara moja, na matarajio ni kujaza nafasi hiyo haraka iwezekanavyo.
“Brian aliiwezesha klabu kupanda Ligi Kuu mwaka jana, ikiwa ni mara ya pili tu katika historia ya klabu…hata hivyo, kutokana na hali ilivyo, mmiliki
Zingarevich ameona ulazima wa kufanya mabadiliko,” taarifa ya klabu inasema.
McDermott alijiunga Reading 2000 akifanya kazi chini ya Alan Pardew ambaye sasa ni kocha wa Newcastle United.
Mwaka 2009 baada Reading kumfukuza kazi kocha wao, Brendan Rodgers (sasa bosi wa Liverpool wanaofanya vizuri), McDermott alipewa ukocha wa muda kabla ya kuwa kocha kamili.
Reading wanashika nafasi ya 19 kati ya 20 zinazoshiriki Ligi Kuu, wakiwa na pointi 23 sawa na Queen Park Rangers (QPR) wanaoshika mkia na wamebakisha mechi tisa kumaliza ligi.