Menu
in , , ,

Manchester United warejea kileleni

Kocha Alex Ferguson ameadhimisha uwekwaji wa sanamu yake katika uwanja wa Old Trafford kwa zawadi ya ushindi dhidi ya Queen Park Rangers (QPR).

Kocha huyo aliyepewa heshima baada ya kuwafundisha United kwa miaka 26, aliona timu yake ikiwa nyuma kwa bao moja kama ilivyotokea mechi nyingi zilizopita.

Haikutarajiwa, hata hivyo, kwamba QPR waliomtimua kocha Mark Hughes Ijumaa wangeibuka na ushindi, na United wakatumia dakika nane za kipindi cha pili kupachika mabao matatu.

Kocha mteule wa QPR, Harry Redknapp alishuhudia kutoka jukwaani kichapo hicho, kwa matumaini ya kubadilisha hali siku zijazo.

Kwa ushindi huo, Manchester United wanaongoza ligi. Mabao yao yalifungwa na Jonny Evans, Darren Fletcher na Javier Hernandez ‘Chicharito’ wakati lile la QPR lilipachikwa na Jamie Mackie.

Wakali wengine wa msimu huu, West Bromwich Albion walio chini ya Steve Clarke walitumia vyema udhaifu wa hapa na pale wa Sunderland kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 na kujikita nafasi ya tatu.

Hii ni mara ya kwanza tangu 1980 kwa West Brom kushinda mfululizo mechi nne za ligi. Mabao yao yalifungwa na Zoltan Gera, Shane Long, Romelu Lukaku na Marc-Antoine Fortune.

Yale ya Sunderland yalifungwa na Craig Gardner na Stephane Sessegnon.

Everton walibanwa kwa bao la dakika ya 90 lililofungwa kwa kichwa na Sebastien Bassong na kuishia kwa sare ya 1-1.

Everton waliodhani wangeondoka na ushindi baada ya kichapo cha wiki iliyopita, walipata bao la kuongoza kupitia Steven Naismith mapema baada ya kazi nzuri ya Bryan Oviedo.

Kwingineko, Charlie Adam alibandika bao muhimu lililowatenganisha Stoke City na wapinzani wao Fulham kwenye uwanja wa Britannia.

Adam alipachika bao hilo baada ya kumegewa pande na Peter Crouch, bao lililoelezewa na kocha Tony Pulis kwamba limewaongezea heshima.

Hata hivyo, sare hiyo inawaacha Stoke wakiwa nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi, Fulham wakiwa wa tisa.

Reading waliendelea kuboronga baada ya ushindi wao wa kwanza wa msimu Jumamosi iliyopita, ambapo safari hii wamefungwa mabao 3-2 na Wigan ya kocha Roberto Martinez.

Ilikuwa siku ya Jordi Gomez wa Wigan, kwani alifunga mabao yote matatu kwa timu yake, huku bao la mwisho likipatikana dakika ya mwisho na kufuta ndoto za ushindi wa Reading.

Vijana wa Brian McDermott walianza kuliona lango la wapinzani wao kupitia kwa Sean Morrison, kabla ya kusawazishwa na kupachikwa la pili.

Golikipa wa Wigan, Ali Al Habsi alishindwa kuwa imara na kuachia mkwaju wa Hal Robson-Kanu kumchomoka na kujaa wavuni, na kufanya mabao kuwa 2-2.

Martinez alifurahia ushindi wa dakika ya mwisho, ambapo Mhispania mwenzake Gomez alikuwa akicheza kwa mara ya kwanza katika miezi miwili.

Ushindi huo ni zawadi murua kwa Mwenyekiti wa Wigan, David Whelan aliyesherehekea miaka 76 ya kuzaliwa.

Arsenal wanaosherehekea bado kuingia hatua ya mtoano Ligi ya Mabingwa Ulaya walishindwa kufurukuta Villa Park kulikotota maji, baada ya kwenda suluhu na Aston Villa.

Nusu ya kwanza ilikuwa tulivu, huku nyota wa Villa Andreas Weimann na beki mchangamfu wa Arsenal, Laurent Koscielny nusura wazipatie timu zao mabao.

Dakika za mwisho Arsenal walijaribu kila njia kupata bao, lakini wakaambulia pointi moja. Timu mbili hizi zimekuwa na matokeo ya suluhu kuliko nyingine zote katika historia ya ligi kuu ya Uingereza.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version