Iliwachukua miaka 30 klabu ya Liverpool kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England. Kwenye miaka hiyo wameshuhudia wapinzani wao wa jadi klabu ya Manchester United wakitwaa mataji 20 ya Ligi Kuu England.
Chini ya uongozi wa Alex Ferguson tangu mwaka 1986 hadi 2013 klabu ya Manchester United ilikuwa tishio. Ilitamba uwanjani. Ikatamba sokoni. Ikatamba kwenye manunuzi ya wachezaji nyota. Mchezaji yeyote alipoambiwa anatakiwa kwenda timu inayofundishwa na Alex Fefuson hakusita.
Ni wachache kama Ronadinho Gaucho ndiyo waliotema ofa za Alex Feguson na kwenda Barcelona. Wakati Alex Feguson akipewa Man United mwaka 1986 akitokea kwao Sctoland, alikuta ufalme wa Liverpool ulikuwa haupimiki.
Liverpool walikuwa miamba ya England kisoka. Walivutia amstaa wengi. Walijaza vipaji vingi na zaidi ilikuwa bidhaa muhimu katika soko la biashara na soka. Liverpool walikuwa watemi miaka 1990 sambamba na timu zingine maarufu kama Nottingham Forest, Reading, Leeds United,West Ham,Bolton na nyinginezo.
Hata hivyo kwa kipindi kirefu Liverpool walipoteana katika mbio za ubingwa wa EPL, tena miaka minne baada ya Alex Ferguson kutua Manchester United na miaka sita baadaye ya mabadiliko ya muundo wa mashindano ya Ligi Kuu England mwaka 1992.
Tangu walipoteana Liverpool walipitia kwa makocha wengi wakiwemo Rafa Benitez, Gerrard Houllier,Kenny Dalglish,Brendan Rodgers na wengineo, lakini haikufua dafu kwenye suala la kutwaa ubingwa.
Liverpool wana rekodi ya kutwaa mataji matano ya Ligi ya Mabingwa lakini waliendelea kuugulia lilipofika suala la ubigwa wa Ligi Kuu England. Mastaa kibao wamepita katika klabu hiyo wakiweko Steven Gerrard, Fernando Torres,Xabi Alonso,Djbril Cisse, Salif Diao,El Hadji Diouf,Michael Owen, Steve Mcmanaman na wengineo.
Ni jambo lisiloridhisha kuona timu kubwa kama Liverpool inacheza EPL miaka 30 na kutwaa ubingwa mmoja. Lakini ujio wa Brendan Rodgers kwa kiasi fulani ulianza kutengeneza dalili za kubadili mambo kwani walikosa ubingwa katika dakika za lala salama.
Juregn Klopp ndiye alikuja kuwabadili kabisa Liverpool kutoka timu yenye mashaka na kuifanya tishio tena kwenye EPL. Tangu alipokabidhiwa mikoba ya kuwania majogoo hao maarufu kama Lierpudlian mambo yalibadilika.
Angalau Liverpool wakatwaa taji lao kwanza baada ya kupitia miaka 30, kisha wakajiongezea taji lingine la UEFA, huku wakiwa wamelikosa la Europa baada ya kufungwa na Sevilla.
Kwenye miaka ya Klopp Liverpool wametinga fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili na kushinda moja, huku wakikumbuka kichapo maridadi kutoka kwa mabingwa wa wakati wote barani Ulaya, Real Madrid wenye maskani yao jijini Madrid.
Wakati tukikumbuka miaka 30 ya Liverpool kukosa ubingwa, lipo jambo lingine kuwahusu wapinzani wao, Manchester United ambao nao wameanza kutia hofu kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England.
Je, kwanini nawahofia Manchester United kuugulia ugonjwa wa Liverpool? Kujibu swali hilo nitaanzia pale alipoondoka gwiji wao wa soka Alex Ferguson. Tangu kuondoka Alex Ferguson hali ya Manchester United sio nzuri kisoka.
Kelele wanazokutana nazo ni zile za majirani zao Man City ambao wanatemba EPL, na sasa wanaongoza ligi wakiwa na pointi 50 baada ya kuwachapa Liverpool mabao 4-1. Ukitazama Manchester United ya leo ni kama vile Ferguson ameondoka na ubingwa wake wa EPL.
Pale Old Traford wamekuja David Moyes,Jose Mourinho, Luis van Gaal, na sasa Ole Gunnar Solskjaer, lakini hawajatwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Imepita miaka 8 sasa tangu Man United walipotwaa ubingwa wa EPL, msimu wa 2012/13. Na pia imepita miaka minne tangu walipotwaa taji lolote yaani tangu mwaka 2017 wametoka kapa.
Kwahiyo miaka 8 ya ukame wa taji la EPL kisha kukaa miaka minne bila ubingwa wa aina yoyote ni hali ya kutisha kwa Man United. Ni timu kubwa ambayo haiwezekani ikakaa miaka minne bila ubingwa.
Kwa namna fulani hali hiyo itawaathiri pia Arsenal ambayo tangu kuondoka kwa Arsene Wenger wamekuwa wakihangaika huku na huko kuziba pengo lake lakini mambo yamekuwa magumu.
Kocha wao Mikel Arteta alianza vizuri na alionesha mwelekeo lakini bado hajapata matokeo mazuri kwa kazi yake. Arteta ametwaa taji taji moja la FA lakini hakuna mwendelezo wa kile kilichofanyika.
Hali kadhalika Man United wamekuwa wakisuasua misimu kadhaa kwa sasa. Hawaonekani kurejesha makali waliyokuwa nayo enzi za Ferguson. Ni kama vile ufalme umetoweka kwenye viunga vya Old Traford. Wapo wanaotamani Ferguson arudi kwenye ukocha lakini umri ulishamtupa mkono na hawezi kustahimili presha za mechi na uongozi kama alivyofanya kwa zaidi ya miaka 20.
Taji lao la mwisho la Ligi ya Mabingwa walipata mwaka 2008 wakiwa Alex Feguson baada ya kuwachapa Chelsea katika mchezo wa fainali. Tangu hapo hawajafua dafu kwenye Ligi ya Mabingwa, na wamekuwa wakitolewa na kuhamia Europa League kutokana na matokeo mabovu.
Kwa hali ilivyo sasa licha ya kushika nafasi ya pili EPL hadi sasa, lakini hatuwezi kusema Man United wanaweza kutwaa ubingwa msimu. Pengine pia hatuwezi kuwapuuza katika mbio hizo, ila mashaka yangalipo juu ya uwezo na utayari wa kutwaa taji hilo.
Ukame umekita mizizi Old Traford. Hakuna anayeogopa kumenyana na Man United tena. Old Traford hakuna wachezaji wa kuhofiwa tena. Namna gani Ole Gunnar atachanga karata zake na kuondoa ukame huo kisha mataji yakameremeta Old Traford? Swali hilo litajibiwa kwa kusubiri na kuona. Muda utaongea.