Manchester United wakamata usukani
Manchester United wameukamata usukani wa Ligi Kuu ya Uingereza kwa mara ya kwanza msimu huu.
Vijana wa Alex Ferguson waliwapokonya Chelsea uongozi huo kwenye mechi ya mapema dhidi ya Arsenal, baada ya ushindi wa 2-1.
Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Robin van Persie aliwapa mateso timu yake ya zamani, kwa kuwaonesha wanachokikosa alipofunga bao mapema dakika ya tatu.
Baada ya kupokewa kwa kuzomewa na washabiki wa Washika Bunduki wa London jijini Manchester, Van Persie alidokoa mpira uliokosewa na nahodha wa Arsenal, Thomas Vermaelen na kuuweka kimiani.
Vermaelen alirejea kosa kama hilo mapema kipindi cha pili, na itabidi ashukuru tu kwamba wachezaji wa United hawakuwa makini kumtungua golikipa Mtaliano, Vito Mannone.
Ilikuwa mechi ya kumbukumbu chungu kwa Arsenal, kwani kipindi kama hiki msimu uliopita, walikung’utwa mabao 8-2 Old Trafford.
Marejeo yake yalishindikana Jumamosi hii, kutokana na uimara wa Arsenal katika mechi waliyogawana kutawala mchezo kwa asilimia 50 kila moja.
Wayne Rooney alikosa penati tata iliyotolewa kwa kupiga nje, na kipa Mannone aliishaifuata ukingoni mwa goli. Mwamuzi alidai Santi Cazorla alishika mpira.
Bao la pili la United lilifungwa na beki Patrice Evra baada ya kuuwahi mpira katika eneo la hatari na kupiga kichwa, likiwa shambulizi fuatilizi baada ya mabeki wa Arsenal kuokoa mpira.
Arsenal walipoteza mchezaji mmoja, baada ya kiungo mahiri Jack Wilshere kuoneshwa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya dhidi ya Evra, kadi ambayo kocha Arsene Wenger anasema ilitokana na ukali tu wa mwamuzi, tangu kadi ya njano ya mwanzo.
Kiungo anayetamba katika mechi karibu zote za Arsenal, Carzola alifunga bao katika mkwaju wa mwisho wa mechi hiyo, kutokana na udhaifu dhahiri wa ukuta wa Man U msimu huu.
Ni ushindi huo uliowakweza Manchester United hadi nafasi ya kwanza kwa kufikisha pointi 24, moja mbele ya Chelsea walioongoza kwa muda mrefu.
Vijana wa Stamford Bridge walishindwa kutumia mchezo dhidi ya Swansea kurejea kileleni, baada ya kuambulia sare ya 1-1 ugenini.
Chelsea wanaoweza kuwa katika matatizo ya kisaikolojia, walitangulia kufunga kupitia Victor Moses na kulinda bao hadi dakika za mwisho mwisho waliposhindwa kuhimili shinikizo la vijana wa Michael Laudrup.
Alikuwa Pablo Hernandez aliyemzidi maarifa kipa mzoefu, Petr Cech kwa kumtungua kutoka kwenye kona.
Tottenham wakicheza uwanja wa nyumbani walishangazwa kwa kichapo kutoka kwa Wigan, ambapo walishindwa kabisa kukomboa bao lililofungwa na Ben Watson.
Spurs walizomewa na washabiki wa nyumbani, mtindo uliokuwa umesahaulika, baada ya kubadili mwenendo wao wa kukosa ushindi walioanza nao msimu huu.
Norwich City wamejidhihirishia ufanisi kipindi hiki kwa kutofungwa mechi ya nne mfululizo, baada ya kuwatia adabu Stoke City kwa bao 1-0.
Bradley Johnson alifunga kwa kichwa katika kipindi cha kwanza, baada ya mpira wa adhabu ndogo tata iliyopigwa na Robert Snodgrass.
Mchezaji Gabriel Agbonlahor alimaliza ukame wa mabao katika mechi 28 kwa kuwapatia Aston Villa bao moja lililowazamisha Sunderland.
Everton wameanza kuizoea sare, baada ya kutoshana nguvu kwa mabao 2-2 na Fulham. Everton walipata mabao yao kupitia kwa Marouane Fellaini wakati golikipa wao Tim Howard alijifunga mapema. Bao la kusawazisha la Fulham lilipatikana dakika ya 89, mfungaji akiwa Steve Sidwell na kuwaacha wageni wakijiuliza kulikoni.
Manchester City waliokabiliana na West Ham United ugenini, waliambulia suluhu katika mchezo mgumu.
City wamekuwa timu pekee mpaka sasa isiyopoteza mechi, lakini nusura West Ham waibuke washindi, kama si bao la Kevin Nolan kukataliwa na Yossi Benayoun kuparaza mtambaa wa panya.
Mario Balotelli alipoteza nafasi ya wazi ya kufunga, ambapo timu yake ilionesha uhai zaidi kipindi cha pili, japokuwa Carloz Tevez na Gareth Barry walipoteza nafasi nzuri pia.
Ilikuwa siku nyingine ya msongo wa mawazo kwa bosi Roberto Mancini, aliyeingia mapema uwanjani kwa nusu ya pili ya mchezo, akajichimbia mwenyewe akisubiri wachezaji wake kutokea.
Hii ni mechi ya kwanza kwa City kushindwa kufunga walau bao moja tangu Aprili mwaka huu, licha ya kuwaanzisha kwa mara ya kwanza Balotelli, Tevez na Edin Dzeko kwa pamoja. City wanabaki nafasi ya tatu.