Menu
in , , ,

Manchester United waangukia pua


*Wafungwa na Stoke, Moyes hoi
*Sunderland wawapiga Newcastle
*Howard Webb atoa kadi tata

Shamrashamra za kocha David Moyes na kikosi chake cha Manchester United kuondoka kwenye kufungwa mechi iliyopita zimegeuka machungu.
Mashetani Wekundu hao wamepotezea dira nyumbani kwa Stoke walikofungwa mabao 2-1 katika mchezo mkali.
Stoke walianza kupata bao kupitia kwa Charlie Adam dakika ya 38 ambalo lilikuja kusawazishwa kipindi cha pili na Robin van Persie dakika ya 47, ambapo RVP alicheza mbele sambamba na Juan Mata na Wayne Rooney tangu dakika ya kwanza na kuwatia hofu wapinzani wao.
Alikuwa Adam tena aliyecheka na nyavu kutoka umbali wa yadi 25 dakika ya 52 na Moyes alijaribu kila njia kujinusuru lakini hakuweza.
Alifika mahali akamwingiza Chicharito, ikielezwa kwamba ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao anapoingia ‘jioni’ na kwamba ana bahati ya kufunga hapo Stoke, mambo yalibaki vile vile, ambapo RVP ndiye alimpisha.
Mabeki wawili wa United, Phil Jones na John Evans waliumia na kutolewa kipindi cha kwanza, lakini Stoke nao walipoteza wachezaji wawili kipindi cha pili kwa kuumia.
Hii ni mara ya kwanza tangu mwaka 1984 kwa Stoke kuwafunga Manchester United, kwa hiyo Moyes atarudi Manchester kwa uchungu akajipange upya kwa mechi zijazo.

SUNDERLAND WAWASASAMBUA NEWCASTLE

Timu iliyokuwa katka hatari ya kushuka daraja, Sunderland wamefanikiwa kushinda mabao 3-0 walipocheza ugenini kwa watani wao wa jadi, Newcastle.
Mabao ya Fabio Borini, Adam Johnson na Colback yalitosha kumwacha kocha Gus Poyet akichekelea kwani sasa wamepanda hadi nafasi ya 14.
Kocha Alan Pardew wa Newcastle alionekana kutoamini kilichokuwa kikiendelea, kwa sababu alitumia ‘silaha’ zake anazoziamini na walilisogelea lango la wapinzani wao mara nyingi lakini wakaishia kwa kigugumizi na kurudi.
Wamepokea kichapo hicho katika wiki ambayo wamemuuza mchezaji wao mahiri Yohan Cabaye kwa Paris St-Germain, baada ya kuwagomea Arsenal msimu uliopita.
Hali ni ngumu kwa Newcastle kwa sababu hawajashinda mechi zao tano kati ya sita zilizopita walizocheza.

WEST HAM SAFI, WEBB ATOA KADI TATA

West Ham walipata ushindi wa 2-0 dhidi ya Swansea lakini wakapata pigo kwa mshambuliaji wao aliyerejea akitoka kwenye majeraha Andy Carroll kupata kadi nyekundu.
West Ham wanakwenda vyema sasa, baada ya Jumatano iliyopita kufanikiwa kuwazuia Chelsea kwa kwenda nao suluhu katika dimba la Stamford Bridge.
Carroll ndiye alitoa pasi zilizozaa mabao hayo mawili na kocha Sam Allardyce amesema kwamba wataikatia rufaa kadi hiyo, kwa sababu Carroll ndiye aliyekuwa amechezewa rafu.
Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England alipewa kadi nyekundu baada ya kurusha mikono wakati akijinasua mikononi mwa Chico Flores aliyemkaba shingo na kushuka naye wakati Carroll akipiga kichwa.
Baada ya kujinasua kwenye mikono hiyo alipepesuka na wakati akizunguka labda kutafuta uwiano alimparaza Flores kwenye nywele, naye Flores akaonesha kana kwamba amempiga machoni, na mara moja mwamuzi Howard Webb akatoa kadi nyekundu.

MATOKEO MENGINE EPL

Katika mechi nyingine, Cardiff walifanikiwa kuchomoa kwa Norway na kupata ushindi wa mabao 2-1.
Everton wakicheza nyumbani Goodison Park, walifanikiwa pia kukomboa bao kwa Aston Villa na kisha kushinda kwa mabao 2-1.
Fulham nao walipepesuka kwa kufungwa mabao 3 -0 na Southampton wanaoonekana kuanza kurudi kwenye chati baada ya kutoa sare na Arsenal kwenye mechi iliyopita.
Hull waliwashika Tottenham Hotspur kwa kwenda nao sare ya 1-1.
Jumapili hii Arsenal wanawakaribisha Crystal Palace huku West Bromwich Albion wakiwa wenyeji wa Liverpool. Jumatatu Manchester City wanawakaribisha Chelsea, na haijulikani kama mvua ya mabao itaendelea.
Kwa matokeo ya leo, Man City wanaendelea kuongoza wakifuatiwa na Arsenal, Chelsea na Liverpool licha ya wote kuwa nyuma kwa mchezo mmoja.
Everton wanafuata nafasi ya tano, Spurs wa sita na Man United wameendelea kubaki pale pale ya saba wakifuatiwa na Newcastle, Southampton na Aston Villa.
Stoke kwa ushindi wao wanashika nafasi ya 11 wakifuatiwa na Swansea, Hull, Sunderland, Norwich, Crystal Palace na West Brom.
Katika eneo la kushuka daraja, ambapo timu zote zimecheza leo ni West Ham wenye pointi 22, Cardiff 21 na Fulham wametulia mkiani kwa pointi 19.

51.574685-0.099881

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version