Menu
in , , ,

Manchester United matumbo joto

Robin van Persie

*Tisa kuchinjwa, Van Persie afikiria kutimkia Italia

Ikiwa imebaki mechi moja kumalizika kwa Ligi Kuu ya England (EPL), ambapo Manchester United wanaelekea kushika nafasi ya nne na kutupwa kwenye mechi za mchujo za Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), wachezaji wapo matumbo joto.

Habari zinasema kwamba hatima ya wachezaji tisa, wakiwamo nyota waliodhani kwamba wamefika, itajulikana Jumatatu hii, pale kocha Louis van Gaal atakapoweka hadharani mipango yake kwa msimu ujao.
Wapo watakaoambiwa wakitaka wabaki lakini watasugua benchi, wa kutakiwa kutolewa kwa mkopo, kuachwa kwa kuwa mikataba inamalizika au kuuzwa ili kupunguza gharama za klabu na pia kuwapatia fedha kununua wachezaji wazuri zaidi.

Hatima ya kipa David De Gea inadhaniwa itabaki mikononi mwake mwenyewe, baada ya kuandaliwa mkataba mnono huku akitakiwa na Real Madrid wa Hispania. Kocha Van Gaal amesema wao wamemaliza kazi, ni juu yake kuamua na anashangaa kwa nini anapata kigugumizi.

Wachezaji ambao hawajui hatima yao na kocha ataamua au kuwashauri kwa manufaa yao ya baadaye ni pamoja na mshambuliaji wa kati aliyehamia Old Trafford kutoka Arsenal akiwa kiwango cha juu sana, Robin van Persie.

Wengine ni Anders Lindegaard, Rafael, Jonny Evans, Adnan Januzaj, James Wilson, Radamel Falcao, Nani na Javier Hernandez ‘Chicharito’ aliye kwa mkopo Real Madrid.

Tayari Van Gaal amefanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji hao, huku wengine alitarajiwa kukutana nao wikiendi hii kabla ya uamuzi wa mwisho kufikia.

“Unajua lazima nizungumze nao, tutakuwa na kinywaji cha pamoja kwa ajili ya kuagana baada ya hapo. Baada ya mechi yetu ya Jumapili nitakuwa na nafasi ya kutoa tamko Jumatatu. Inategemea mazungumzo yataendaje ndio tujue kama mchezaji yupo anabaki na yupo anaondoka,” anasema Van Gaal.

Wakati hayo yakijiri, Van Persie amekuwa na kikao kizito na wakala wake ili kuamua hatima ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi aliyesajiliwa na Sir Alex Ferguson na kumwacha kwenye mataa, akistaafu, lakini akafarijika kwa Mdachi mwenzake, Van Gaal kumrithi David Moyes, hadi akafikiria angepewa unahodha.

Lakini sasa mambo yamebadilika kiasi kikubwa – kutoka ndoto za uongozi kwenye timu hadi kubaki benchi na sasa kuondoka ndani ya klabu ama kwa hiari au kwa kuachwa mkataba umalizike kiangazi kijacho achape mwendo.

Wakala huyo, Kees Voos, anadaiwa kupanda ndege kwenda Italia kujadiliana na mabosi wa Juventus na Roma ili mteja wake ajiunge nao msimu ujao. Angependa zaidi kujiunga Juventus maana kwa sasa wapo juu Ulaya, wakiwa wamefika fainali ya UCL kwa kuwatwanga Real Madrid kwenye nusu fainali.

Tovuti ya Italia, TuttoMercatoWeb imeeleza kwamba Voos anatarajiwa kufanya majadiliano kabla ya Jumatatu, ambapo inadai uwezekano mkubwa ni kuingia Juve, kwa sababu wachezaji wake, Carlos Tevez na Fernando Llorente wanatarajiwa kuondoka.

Hata hivyo, Roma wanapewa nafasi pia, kwani walituma barua kuuliza juu ya uwezekano wa wao kumpata mshambuliaji huyo mkongwe ambaye tayari amekataa ofa kubwa zilizotolewa na klabu za Uturuki – Galatasaray, Besiktas na Fenerbache.

Inadaiwa kwamba Waturuki hao wapo tayari kumpa mshahara wa pauni 220,000 kwa wiki, lakini mwenyewe anaona kwamba kwenda kucheza huko ni kushuka hadhi.

Baada ya Van Gaal kuonesha uwezekano wa kutompatia mkataba mpya, akazingatia mkataba wa miaka mitatu Uturuki na fedha hizo, inaelezwa kwamba anafikiria upya, lakini atasubiri matokeo ya majadiliano ya klabu za Italia na mshahara watakaotoa.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version