*Wakung’utwa 3-0 na Liverpool SC
*Arsenal wajizatiti, wawapiga Spurs
Ilikuwa Jumapili yenye matukio mazito kwa mechi za mahasimu wanne katika mechi mbili, ambapo Manchester United na Tottenham Hotspurs wamepigwa kwao.
Ligi Kuu ya England ilisonga mbele Jumapili hii, kwa Kocha David Moyes kutafuta jinsi ya kutoka kwenye jinamizi la timu aliyorithi na Tim Sherwood wa Spurs akitaka kuwakandamiza Arsenal.
Hata hivyo, Liverpool wanaoshika nafasi ya pili kwa kupachika mabao mengi waliwatia doa kubwa Mashetani Wekundu kwa kuwafumua kwa mabao matatau bila majibu.
Mabao ya Liverpool yalifungwa na nahodha wao Steven Gerard mawili kwa penati, akakosa penati moja na jingine akafunga Luis Suarez.
Kihistoria, Liverpool na Manchester United ndio mahasimu wakubwa kitaifa na kwa miaka mingi Man U wamekuwa wakiwakandamiza vijana hawa ambao sasa wapo chini ya Brendan Rodgers.
Man U walimaliza kwa mchezaji mmoja pungufu kwa sababu nahodha wao,Nemanja Vidic alioneshwa kadi nyekundu kwa mchezo mchafu dhidi ya Daniel Surridge.
Vidic, mchezaji wa muda mrefu wa Man U hakukabidhi beji ya unahodha kwa mchezaji yeyote, bali aliitupa kwenye eneo la kujidai la makocha, akionesha alivyosikitishwa kwa kutolewa kwake nje.
ARSENAL WAWAPIGA SPURS KWAO
Katika mechi nyingine ya EPL, Arsenal walifanikiwa kuibuka kidedea katika mechi ngumu ugenini kwa mahasimu wao wa London Kaskazini.
Bao la Tomas Rosiscky ndani ya dakika 10 za mwanzo lilitosha kuwafaidisha Arsenal licha ya pilika nyingi za Spurs, zikiwamo mara nyingi za mchezaji wao wa zamani, Emmanuel Adebayor ambazo hazikuzaa matunda.
Arsenal walianza kwa kasi nzuri hadi kupata bao, na kujaribu kupata la pili, lakini inaelekea walipewa maelekezo makali na kocha wao Sherwood kwa jinsi walivyorejea kwa kasi kubwa na kuliandama lango la Arsenal kama nyuki.
Kipa wa Arsenal, Wojciech Szczesny alifanya kazi kubwa kupita kiasi pamoja na mabeki wake kuwazuia wachezaji wa Spurs kutikisa nyavu. Beki wa kati, Laureny Konscielny anayewaniwa na Bayer Munich na Barcelona naye alifanya kazi isiyo kifani kama mawenzake Per Mertesacker.
Kwa matokeo ya leo, Chelsea wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 66, Lioverpool wakiwa wa pili kwa pointi zao 62 kama Arsenal, lakini Gunners wana mabao pungufu.
Manchester City wanashika nafasi ya nne kwa pointi zao 60 lakini wana mechi mbili pungufu ya Arsenal na Liverpool na mechi tatu pungufu ya Chelsea.
Spurs wenye pointi 53 ni wa tano wakiwa na mechi sawa na Chelsea wakifuatiwa na Everton wakati Manchester United wanashika nafasi ya saba wakiwa na pointi 48 na wamecheza mechi sawa na Liverpool na Arsenal.
Wa tatu kutoka mkiani ni Sunderland waliocheza mechi 27 na wamejikusanyia pointi 25 sawa na Cardiff ambao hata hivyo wamecheza mechi 30 na wanaoburuza timu zote ni Fulham wenye pointi 24 kutokana na mechi 30.