*City waangukia pua kwa Everton, Reading kilio
*Arsenal wageuza wembe, Liverpool, QPR chali
Pamoja na kupata ushindi mwembamba dhidi ya Reading wasio na kocha, Manchester United imelisogelea taji la soka.
Vijana wa Alex Ferguson walijisogeza umbali wa pointi 15 kutoka kwa mahasimu na majirani wao, Manchester City.
Wakati United wakiambulia bao moja lililofungwa na
Wayne Rooney Old Trafford, City wakicheza bila nyota wao waliadhiriwa na Everton kwa kukandikwa mabao 2-0.
Huku zikiwa zimebaki mechi tisa kwa timu nyingi, kuna kila dalili kwamba kicheko mwaka huu kitakuwa Old Trafford, baada ya msimu uliopita kuwa nyumba ya jirani – Etihad.
Hata hivyo, aina ya mchezo walioonesha United haukuvutia wengi, waliotarajia watoke na ushindi mnono. Reading walikuwa chini ya kocha wa timu ya vijana, Eamonn Dolan anayeshika kwa muda nafasi ya Brian McDermott aliyefukuzwa Jumatatu.
City wakicheza bila Yaya Toure, Vincent Kompany, na Sergio Aguero walijitahidi bila mafanikio kufumania nyavu za Everton.
Hawakuamini Leon Osman alipomzidi maarifa kipa Joe Hart kwa kuandika bao la kwanza, na hata Steven Pienaar alipopewa kadi nyekundu, City walishindwa kutumia faida ya mtu mmoja zaidi kwa karibu nusu saa. Badala yake Nikica Jelavic alikomelea msumari wa mwisho dakika ya 90 na kumwacha Roberto Mancini akilalamika mwenyewe. Kocha msaidizi wa City, David Platt alikiri pengo lililopo sasa ni kubwa, lakini akaahidi kikosi chao kitajielekeza kushinda mechi zilizobaki.
Katika mechi nyingine, Arsenal waliacha historia Ujerumani katikati ya wiki kwa kuwabandika Bayern Munich 2-0, wamegeuza wembe na kuwanyoa kwa idadi hiyo hiyo Swansea, timu ngumu ya Wales.
Alikuwa beki wa kushoto, Nacho Monreal aliyefungua kitabu kwa bao lake la kwanza kwa timu tangu ajiunge Januari mwaka huu, akiwasikitisha wana Swansea kwenye uwanja wa Liberty.
Gervais Lombe Yao Kouassi ‘Gervinho’ kuandika bao la pili dakika za lala salama, akikata kiu ya siku nyingi ya washabiki wa Arsenal kuona mabao yake, kwani amekuwa na kosakosa nyingi.
Kwa ushindi huo, Arsenal wamebaki nafasi ya tano kwa kufikisha pointi 50, wakati Swansea ni wa tisa kwa pointi zao 40.
Liverpool waliokuwa wameanza kasi ya kupanda msimamo wa ligi waliduwazwa na Southampton, kwa kupewa kichapo cha 3-1 katika dimba la St. Mary’s.
Huo ni ushindi ambao Saints waliuhitaji, lakini kwa upande wa pili umeua kwa kiasi kikubwa ndoto za Liverpool kumaliza ligi katika nafasi nne za juu.
Aston Villa waliokuwa kwenye dimbwi la kushuka daraja, wameendelea kujinusuru kwa ushindi wa pili mfululizo, walipowafunga wanaoburuta mkia, Queen Park Rangers (QPR) mabao 3-2 katika mechi ya vuta nikuvute Villa Park.
Kocha Paul Lambert walau sasa atapumzika, baada ya timu yake kufikisha pointi 30 na kujitenga na tatu za mwisho kwa tofauti ya pointi sita. QPR wamebaki na pointi zao 23, wakifungana na Reading kwa pointi na hata uwiano wa mabao. Kati yao na Villa wapo Wigan wenye pointi 24 na Jumapili hii wanakipiga na Newcastle.
West Bromwich Albion walishindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kutoka suluhu na Stoke City, hivyo kushika nafasi ya nane kwa pointi zao 44, huku Stoke wakiwa wa 10 kwa pointi 34.
Jumapili hii inashuhudia Tottenham Hotspurs wakiwakaribisha Fulham, Chelsea wakiwaita Stamford Bridge vijana wa West Ham United wakati Norwich City ni wageni wa Sunderland.