Menu
in , , ,

Manchester United hawakamatiki


*Arsenal wasafisha hali ya hewa Emirates

 

*Reading, Everton, Stoke, Sunderland hoi

 

Mzunguko wa 27 wa Ligi Kuu ya England umeshuhudia vinara wake, Manchester United wakizidi kupaa.

 

Ilikuwa kicheko tu kwa Alex Ferguson, United walipowafinya Queen Park Rangers (QPR) mabao 2-0.

 

Kwa matokeo hayo, Man U wamefikisha pointi 68, zikiwa ni 15 zaidi ya wanaowafuata – Manchester City, wanaoamilisha mzunguko huu Jumapili hii kwa kucheza na Chelsea walio nafasi ya tatu.

 

Rafael Da Silva alifungua neema United, kisha mkongwe Ryan Giggs akaweka bao la pili kipindi cha pili, ikiwa ni mechi yake ya 999.

 

Rafael alionesha umahiri katika ulinzi, alipookoa katika mstari mpira wa kichwa wa Chris Samba uliokuwa ukizama nyavuni

 

Hali ya hewa imetulia kiasi Emirates, baada ya Arsenal kuwafunga Aston Villa mabao 2-1, siku chache baada ya matokeo mabaya kwa vijana hao wa Arsene Wenger.

 

Español: Santi Cazorla, futbolista español.
Español: Santi Cazorla, futbolista español. (Photo credit: Wikipedia)

 

Kiungo wa Kihispania, Santi Cazorla alifungua kitabu mapema dakika ya sita, na ndiye aliyeunga bao la pili pia dakika ya 85.

 

Mabao yote yalifurahiwa, kwani lile la kwanza lilionekana walau kurejesha heshima inayopotea Emirates, na la pili lilikuwa faraja baada ya washabiki kuwa roho juu kwa mwelekeo wa sare ulioonekana dhahiri.

 

Arsenal walilegea kipindi cha pili, wakashindwa kumiliki mpira ipasavyo, na Villa hawakusita kuteka fursa hiyo muhimu kwa kusawazisha kwa kiki ya yadi 20 ya Andreas Weimann.

 

Wakijua wanajiweka pabaya kuitafuta nafasi muhimu ya tatu au ya nne, Arsenal waligangamala, na jitihada za kiungo wa kimataifa wa England, Jack Wilshere zilizaa matunda alipommegea beki wa kushoto aliyepanda, Nacho Monreal aliyempasia Mhispania mwenzake Cazorla aliyetikisa nyavu.

 

Arsenal wamefurahi pia kwa waliokuwa wakiwapumulia kisogoni, Everton kuangukia pua Carrow Road, walipochapwa mabao 2-1 na Norwich City.

 

Kwa matokeo hayo, Everton wanabaki nafasi ya sita wakiwa na pointi 42 wakati Arsenal wamefikisha pointi 47, wakishika nafasi ile ile ya tano, nyuma ya Tottenham Hotspurs wenye pointi 48 na wanacheza Jumatatu hii na West Ham United.

 

Norwich walikuwa chini kwa umiliki wa mpira, na kushitukia wakiachwa nyuma kwa bao dakika ya 39, Leon Osman alipocheka na nyavu.

 

Hata hivyo, Norwich walitumia vyema dakika tano za mwisho, ambapo Kei Kamara alifunga bao dakika ya 85 kabla ya Grant Holt kuwamaliza vijana wa David Moyes kwa bao la dakika za majeruhi.

 

Norwich wanashika nafasi ya 12 sasa.

 

Tetemeko lilitokea katika Uwanja wa Madejski, pale Reading walipoadhiriwa nyumbani na Wigan kwa kusasambuliwa mabao 3-0.

 

Nyota wa Ivory Coast, Arouna Kone aliwanyanyua Wigan kutoka eneo la kushuka daraja kwa kufunga mabao mawili na Maynor Figueroa kufunga la tatu.

 

Reading walimaliza mchezo wakiwa 10, baada ya Pavel Pogrebnyak kuzawadiwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Figueroa.

 

West Bromwich Albion walikuwa na mwendelezo mzuri walipowafunga Sunderland mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na Romelu Lukaku, moja kwa penati.

 

Huu ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Wet Brom nyumbani kwao Hawthorns tangu Desemba mwaka jana, ambapo walipata penati baada ya Craig Gardner kuzuia kwa mkono majalo ya Liam Ridgwell. Sunderland walifuta machozi kwa bao la Stephane Sessegnon.

 

Katika mechi ya mapema Jumamosi hii, Fulham walijiweka pazuri baada ya bao pekee la Dimitar Berbatov kuwazamisha Stoke City.

 

Huu ni ushindi wa nne tu katika mechi 19. Stoke walipoteza nafasi ya kusawazisha, pale kipa Mark Schwarzer alipookoa penati ya Jonathan Walters. Kipa huyo alitajwa kuwa mchezaji bora wa mechi, ambapo timu yake imetoka eneo la kushuka daraja.

 

penalty.

 

Kwa hali ilivyo sasa, timu tatu zilizobaki mkiani na zinazotishiwa kushuka daraja ni QPR wenye pointi 17, Reading pointi 23 na Aston Villa pointi 24. Wanaochungulia humo ni Wigan wenye pointi 24 pia, lakini wana uwiano mzuri wa mabao dhidi ya Villa.

 

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version