DAKIKA 20 za mchezo zilitosha kugundua kuwa kikosi cha kocha Pep Guardiola kilikuwa kinakwenda kubugizwa mabao mengi katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu England. Ulikuwa usiku mbaya kwa Man City ambao wakiwa kwenye dimba la nyumbani Etihad. Hakuna aliyetegemea kama timu hiyo itakubali kipigo kikali cha mabao 4-0 nyumbani kutoka kwa Tottenham Hotspurs, lakini imeshatokea na kudhihirisha hali ya mambo si njema klabuni hapo.
TANZANIASPORTS inakuletea masuala muhimu yaliyojitokeza ikiwemo rekodi ya a ibu waliyofikia Man City katika historia ya EPL.
Furaha katikati ya aibu
Maelfu ya mashabiki wa Man City waliojazana uwanjani hapo walishuhudia nyota wao aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora ya Ballon D’or Rodri akiwa amshikilia tuzo hiyo na kuwaonesha mashabiki wao. Katika ulimwengu wa soka tuzo hiyo ni muhimu kwake binafsi na klabu yao ya Man City ambayo haijawahi kuwa na mchezaji mwenye tuzo hiyo.
Aidha, inakuwa tuzo ya kwanza tangu alipochukua Cristiano Ronaldo mwaka 2008 na tangu hapo hakuna mchezaji wa EPL aliyetia fora hadi kupatikana kwa kiungo mkabaji Rodri. Furaha ya mashabiki wa Man City ilianza kuyeyushwa baada ya dakika 20 za mwanzo za mchezo huo ambapo James Maddisson alipachika mabao mawili na kutia mchanga kwenye kitumbua cha Pep Guardiola aliyetoka kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja na nyongeza.
Bingwa aliyefikia rekodi ya aibu
Mara ya mwisho bingwa kufungwa mechi tano mfululizo ilikuwa mwaka 1956. Man City wamefikia rekodi hiyo baad aya kukumbana na vipigo mara tano mfululizo. Vipigo vitatu vimetoka EPL wakati vingine viwili vimetokana na mashindano mengine; Carabao na UCL. Kufungwa kwa Man City huenda kukatajwa kuwa ni jambo la kawaida lakini idadi ya mabao ndiyo inatisha zaidi. Walipigwa bao 4 na Sporting Lisbon kutoka kwa kocha kijana na aliyehamia Man United sasa, Ruben Amorim, kisha wamekubali kipigo cha idadi hiyo kutoka kwa Tottenham Hotspurs kwenye EPL. Man City anakuwa bingwa wa pili wa EPL kufungwa mechi tano mfululizo.
Mabao mawili ya ‘birthday’
Hakuna kitu kizuri kama zawadi unayopewa katika siku yako ya kuzaliwa. Kwenye siku hiyo ndiyo inakumbusha maisha yako na ulikotoka hadi hapo ulipo. Mabao mawili ya Jaames Maddison yalikuwa na maana kubwa kwenye maisha yake kwani siku hiyo alikuwa anaadhimisha siku ya kuzaliwa ambapo alitimiza miaka 28. Mabao hayo yalikuwa sehemu ya ushindi wa bao 4-0 ambapo mengine mawili yalifungwa na Pedro Poro na Brennan Johnson. Kama kuna zaawadi ya ‘birthday’ aliyotoa kocha wa Tottenham Hotspurs Ange Postecoglou kwa Maddison ni kumpanga katika mchezo muhimu wa EPL. Maddison amesugua benchi mara kadhaa katika mechi za EPL, lakini katika mchezo wa jumamosi alipewa nafasi na imani ya kuonesha umahiri wake. Naye hakumnyima raha kocha wake pale alipopachika mabao mawili matamu na kuwapa ushindi wa pointi tatu muhimu.
Sherehe ya kocha
Kulikuwa na sherehe nyingine katika mchezo kati ya Tottenham Hotspurs na Manchester City. Kocha wa Tottenham Hotspurs alikuwa anafikisha mechi 50 tangu alipopewa jukumu la kuinoa timu hiyo. Kwahiyo ushindi wa mabao 4-0 umempa furaha katika maadhimisho yake tangu alipowasili EPL.
Hakuna kisingizio
Pep Guardiola aliingia katika mchezo huo akiwa na bila wachezaji wake muhimu Rodri na Ruben Dias huku kiwango cha Kevin De Brryune kikiwa kimeshuka mno. Kwa upande wa Tottenham Hotspurs waliingia dimba la Etihad bila wachezaji sita wa kikosi cha kwanza kutokana na kuwa majeruhi. Hivyo timu zote ziliiingia kiwanjani zikiwa na upungufu wa wachezaji imara.
Mkakati wa mbinu
Pep Guardiola aliingia mchezoni akiwa na viungo wawili Ilkay Gundogan na Bernado Silva ambao walikuwa wakishirikiana eneo la kiungo mkabaji na kiungo wa ushambuliaji. Ubunifu wa wachezjai hao ndiyo ulitakiwa zaidi lakini walijikuta wanakabiliana na mbinu tofauti na wlaivyotarajia. Kocha wa Spurs, Ange Postecoglou alimpanga James Maddison badala ya Brennan Johnson na ikiwa na maana Dejan Kulusveksi alitakiwa kucheza pembeni. Mbinu hiyo ililipa kwani iliwachukua dakika 13 tu Spurs kuandika bao la kwanza baada ya kazi nzuri ya Kulusevski aliyemhadaa Josko Gvadiol na kuipangua safu ya ulinzi. Kuchezewa kwa kasi kuliwanyima utulivu Man City na wakajikuta wanaingia kwenye mfumo wa Spurs hadi filimbi ya mwisho ubao ulisoma 4-0.
Rekodi ya kadi ya njano
Katika mchezo huo rekodi nyingine iliyowekwa ni ile ya kadi ya njano ya mapema zaidi aliyopewa kiungo Yves Bissouma. Kadi hiyo ilitolewa ndani ya sekunde 12 za mchezo. Nyota huyo alionywa kutokana na kumchezea madhambi Phil Foden.
Mechi kali mbili
Wakati Man City wakiwa wameweka rekodi ya aibu katika pengo la pointi 8 za EPL dhidi ya kinara wa ligi hiyo Liverpool, wiki ijayo watakaribishwa kwenye dimba la Anfield. Liverpool watawakaribisha Man City waliojeruhiwa mara tano na ikiwa watafungwa mchezo huo itakuwa rekodi ya aina yake. Kabla ya kuvaana na Liverpool, Pep Guardiola atakiongoza kikosi chake katika mchezo dhidi ya Fayenoord ya Uholanzi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.