Menu
in , , ,

Manchester City na Arsenal zajifariji

*Zapoza vipigo vya Ulaya kwa ushindi mwembamba

*West Ham hoi, Reading, Sunderland na Stoke sare

Ushindi mwembamba wa Manchester City na Arsenal haukuwafutia machungu ya vipigo vya Ulaya, lakini yamezipaisha kwenye msimamo.
Man City wamewafunga Swansea bao 1-0 na kusogea nafasi ya pili wakati Arsenal wamesogea nafasi ya tano baada ya kuwafunga Queen Park Rangers bao moja vile vile.
Bado makunyanzi yamebaki Etihad, baada ya kocha Roberto Mancini kusema mchezaji asiyeelewa mbinu zake hafai kuchezea klabu kubwa.
Lakini goli la Carlos Tevez la dakika ya 60 na kazi nzuri ya kipa Joe Hart vilitosha kuwahakikishia City pointi tatu muhimu.
Makocha wa timu zote mbili waliondoka uwanjani na huzuni, baada ya wachezaji wao, Micah Richards wa City na golikipa Michel Vorm wa Swansea kupata majeraha makubwa.
Wote walitibiwa muda mrefu uwanjani, hivyo kwamba palikuwapo nyongeza ya kihistoria ya muda wa mechi kwa dakika 12, isiyopata kutokea katika EPL.
Man City walionekana bado kuweweseka kwa kipigo cha Ajax cha mabao 3-1 ugenini, ambacho kimsingi kimefuta ndoto za kufanya vyema kwenye ligi hiyo.
Arsenal waliotoka kuchapwa 2-0 na Schalke kwenye mashindano hayo na pia kuangukia pua mbele ya Norwich Jumamosi iliyopita, iliambulia ushindi wa bao moja lililofungwa na Mikel Arteta dakika ya 84.
Tofauti na Man City, Arsenal wapo vizuri kwenye kundi lao kuwania hatua za mtoano Ligi ya Mabingwa, kwani wana nafasi ya pili kati ya timu nne.
Washabiki wa Arsenal walifurahia kurejea dimbani kwa kiungo wao wa kimataifa, Jack Wilshere aliyecheza kwa zaidi ya saa moja tangu mwanzo wa mchezo.
Wilshere mwenye kipaji adimu amerejea baada ya kukosekana kwa karibu miezi 18 kutokana na majeraha na pia beki wa kulia aliyevunjika mguu Mei, Bacary Sagna alirejea na kucheza dakika zote.
Bado Arsenal hawakuonekana kuwa na machachari waliyokuwa nayo kabla ligi kwenda mapumziko kupisha mechi za kimataifa tatu zilizopita.
Uhai ulijitokeza baada ya Stephen M’Bia wa QPR kupewa kadi nyekundu alipompiga nahodha wa Arsenal,Thomas Vermaelen, baada ya wawili hao kugongana.
West Ham United walioanza ligi kwa tambo za Sam Allardyice huku wakifanya vyema, wanaonekana kuanguka kadiri muda unavyokwenda.
Jana ilikuwa zamu yao kupokea kichapo kutoka kwa Wigan, na yalikuwa mabao 2-0, wakati ushindi ungewaweka West Ham katika nafasi ya nne kwenye chati.
Wigan walitiwa kasi na uchezaji mzuri wa Shaun Maloney, huku James McCarthy  na James McArthur wakidhibiti eneo la kiungo.
Magoli ya Wigan yalifungwa na Ivan Ramis dakika ya nane na McArthur mara baada ya mapumziko.
Katika mchezo mwingine, Aston Villa na Norwich walitoshana nguvu kwa bao 1-1. Huu umekuwa msimu ambao Aston Villa wameanza vibaya zaidi katika miaka 43, na sare hii wameiambulia nyumbani Villa Park.
Wenyeji walitangulia kufunga kupitia kwa Christian Benteke, lakini Michael Turner akaendeleza majonzi Villa Park kwa kusawazisha katika kipindi cha pili, Villa walipobakiwa na wachezaji 10 uwanjani.
Villa walipata pigo hilo katika dakika ya 53, kwa beki wao Joe Bennet kupewa kadi nyekundu kwa mchezo wa rafu, baada ya kupata kadi ya pili ya njano.
Wagumu wawili – Stoke City na Sunderland walitoka suluhu. Stoke waliingia uwanjani wakiwa na rekodi ya ushindi wa mechi moja, sare sita na kushindwa mbili.
Sunderland kwa upande wao waliingia wakiwa wameshinda mechi tatu, sare tano na kupoteza moja, hivyo haikushangaza kwa mechi kumalizika kwa kukosa mbabe.
Mechi hii haikukosa majeruhi, na alikuwa mchezaji wa kimataifa wa Ireland, Mark Wilson aliyeumia vibaya kifundo cha mguu. Watazamaji walichoshwa na dakika nane za nyongeza ambapo nusura Peter Crouch awafungie Stoke.
Reading wanaotafuta ushindi wa kwanza baada ya kupanda daraja waliambulia sare ya mabao 3-3. Wakati washabiki wakiamini timu yao ilishalala, Hal Robson-Kanu alisawazisha katika dakika ya 90.
Mechi hii iliyofanyika uwanja wa Madejski, Reading, inaelezwa kuwa ilijaa udhaifu katika nyanja za ufundi wa kimpira kuliko zote zilizochezwa Jumamosi hii.
Reading walifunga mabao yao kupitia kwa
Mikele Leigertwood aliyefyatua mkwaju mkali dakika ya 26. Kocha Martin Jol wa Fulham alimtoa
Hugo Rodallega na kumwingiza Bryan Ruiz, aliyesawazisha bao dakika ya 60.
Ruiz alitoa pasi kwa Chris Baird iliyozaa bao la pili kutokana na kona muda mfupi baadaye.
Baird aliumia na kutoka nje kwa kuteleza vibaya wakati akishangilia bao hilo, jambo lililoathiri ngome ya wageni hivyo kwamba ndani ya dakika tano, Reading walifunga mabao mawili katika dakika tano za mwisho.
Garath McCleary aliyeingia kipindi cha pili alisawazisha mambo dakika ya 85, lakini Dimitar Berbatov akaing’arisha Fulham katika dakika ya 88 kabla ya Robson-Kanu kuwanyang’anya tonge mdomoni.
Macho na masikio yanaelekezwa Stamford Bridge Jumapili hii, ambapo mabingwa wa Ulaya, Chelsea wanawakaribisha Manchester United. Everton nao wakawakaribisha Liverpool, katika mtanange wa watani wa hadi wa Merseyside
Newcastle United ya Alan Pardew watawakaribisha West Bromwich Albion walio chini ya Steve Clarke na alioanza vyema ligi. Southampton wanaochechemea watawaalika Tottenham Hotspur inayoanza kung’aa chini ya Andre Villas-Boas.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version