Je, Hatma ya kesi yake kubadili Taswira ya EPL?
Wiki ya pili ya kesi ya Manchester City dhidi ya Ligi Kuu ya England (EPL) kuhusu madai ya uvunjifu wa sheria za kifedha inaendelea kwa kasi. Mbali na kesi inayoendelea, Manchester City pia wanatarajia uamuzi wa haraka kutoka katika kesi nyingine dhidi ya Ligi Kuu kuhusu malalamiko yao juu ya mikataba ya kiuchumi inayoitwa “Associated Party Transaction” (APT). Uamuzi huu unaweza kuwa na athari kubwa kwa jinsi kesi hii itakavyozidi kuendelea.
City wanaripotiwa kuwa na matumaini ya kushinda kesi hii ya sasa baada ya kuanzisha mchakato wa kisheria ambao haujawahi kutokea. Mnamo Juni, Manchester City waliwasilisha madai ya kurasa 165 dhidi ya EPL, wakidai kuwa sheria za APT zinawabagua wamiliki kutoka ‘Uarabuni’. Sheria hizi za APT zilipitishwa na Ligi Kuu ya England mnamo Desemba 2021 baada ya klabu ya Newcastle United kununuliwa na waarabu kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF). City wanapinga kwamba sheria hizo zimeelekezwa dhidi ya umiliki wa mataifa ya uarabuni, hususan baada ya kuongezeka kwa uwekezaji waarabu kwenye vilabu vya soka vya England.
Pamoja na kesi hii ambayo uamuzi wake utatolewa mapema, mjadala mkubwa tangu kuanza kwa msimu huu mpya wa EPL, ni kesi ile kubwa na ya kihistoria dhidi ya Manchester City, bingwa mtetezi, ambaye anakabiliwa na tuhuma nzito za ukiukwaji wa kanuni za kifedha. Tuhuma hizi 115 zinazodaiwa kutokea kati ya 2009 na 2018, zinatarajiwa kutolewa uamuzi wake kabla ya msimu huu kumalizika.
Ripoti mpya za Septemba 2024 zinaonyesha kuwa kesi hii imeingia hatua za mwisho huku mawakili wa pande zote mbili wakiwa tayari kwa maamuzi mazito. Inafahamika kuwa uamuzi huu hautakuwa tu na athari kwa Manchester City, bali pia kwenye mustakabali wa sheria za kifedha kwenye Ligi Kuu na mpira wa Ulaya kwa ujumla.
Manchester City inakabiliwa na madai ya kushindwa kutoa taarifa sahihi za kifedha, hususan mapato ya udhamini, pamoja na kutotoa taarifa za malipo ya kocha wa zamani, Roberto Mancini. Kwa mujibu wa Premier League, City pia haikuzingatia sheria za faida na uendelevu kati ya 2015 na 2018, na haikutoa ushirikiano kikamilifu wakati wa uchunguzi huo.
Madai haya yanashtua kwa kuwa yanagusa kipindi ambacho City imekuwa ikitajwa kuwa moja ya klabu bora zaidi barani Ulaya, ikitwaa mataji kadhaa ya Ligi Kuu na kufikia mafanikio makubwa chini ya kocha Pep Guardiola. Hata hivyo, ushindi wao umeibua maswali miongoni mwa mahasimu wao, huku baadhi wakidai kuwa City imepata mafanikio haya kwa njia isiyo halali.
Adhabu gani inastahili ikikutwa na hatia?
Katika mazungumzo ya faragha, wamiliki na watendaji wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu England (EPL) wamekuwa wakibishana kuhusu adhabu inayostahili kwa City iwapo itapatikana na hatia. Baadhi wanadhani kwamba klabu hiyo inaweza kulazimishwa kulipa faini kubwa, lakini wengine wanaamini kuwa adhabu kama hiyo haifai na isiyo ya haki.
Wengine wanashinikiza kuwa adhabu kali kama kukatwa alama kati ya 70 hadi 80 ni muhimu ili kuhakikisha City inashushwa daraja hadi Championship. Wanaotetea adhabu hii wanataja mfano wa klabu ya Saracens katika ligi ya mpira wa raga nchini humo, ambapo walipoteza alama 35, kupigwa faini na kushushwa daraja kwa kuvunja sheria za matumizi ya mishahara.
Akizungumza kwenye podikasti ya No Tippy Tappy Football ya Footy Accumulators, Sam Allardyce yeye alikosoa vikali wale wanaopendekeza Manchester City kuadhibiwa.“Allardyce alisema, “Nadhani ni wivu mtupu,” akiongeza kuwa anahisi baadhi ya watu wanataka City kuadhibiwa kutokana na mafanikio yao makubwa kwenye soka. Allardyce, ambaye aliwahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya England, alionekana kuunga mkono klabu hiyo, akiwataka watu kuwa waangalifu katika kuhukumu bila kuzingatia ukweli wa kesi.
Wakati huo huo, kuna hofu kwamba kushindwa kwa Premier League kuihukumu na kuiadhibu Manchester City katika kesi hii, kutaibua maswali makubwa kuhusu uwezo wa ligi hiyo kujisimamia, hasa kwa kuzingatia uwezekano wa kuwepo kwa mdhibiti huru mwaka ujao. Wakurugenzi wengi wa vilabu wanasema motisha yao ya kufuata sheria itapungua sana ikiwa Premier League itaonekana kutokuwa na nguvu ya kuchukua hatua dhidi ya City.
Hata hivyo, City, inaendelea kujitetea kwa nguvu dhidi ya mashitaka haya, ikisema kuwa ina ushahidi usio na shaka wa kuonyesha kwamba haina hatia. Kesi hii imevuta hisia kutoka kwa wadau wengi wa soka duniani. Kwa mfano kwamupande wa ligi kuu ya Hispania, La Liga, kupitia rais wake Javier Tebas, imekuwa mkosoaji mkali wa klabu zinazomilikiwa na mamlaka za nchi, akitaka ichunguzwe zaidi mipango ya kifedha ya City na klabu nyinginezo. Anasema hivi kwa kuwa City, inaonekana kunufaika na chini ya Mamlaka ya Umoja wa Falme za kiarabu (UAE). Kwenye hilo City mara zote imekuwa ikisisitiza kuwa klabu hiyo hawamilikiwi na serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), lakini mmiliki wake Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan ni makamu wa rais na naibu waziri mkuu wa UAE, ambaye pia ni mwanafamilia ya kiflame ya Abu Dhabi. Sheikh Mansour ni kaka wa rais wa sasa wa UAE, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, na amemuoa Sheikha Manal binti Mohammed Al Maktoum, binti wa Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, mtawala wa Dubai. Ni bilionea haswa ambaye anamiliki hisa nyingi katika vilabu mbalimbali vya soka duniani kupitia City Football Group, ikiwemo Manchester City F.C, kupitia kampuni ya Newton Investment and Development, ambayo anaimiliki kikamilifu na imesajiliwa Abu Dhabi.
Kwa Nini Manchester City Haikubali Makosa?
Wachambuzi wa soka wanaeleza kwamba City inaonekana kuwa iko tayari kupambana kisheria kwa muda mrefu ili kuepuka adhabu yoyote dhidi yake. Wanasheria wa klabu hiyo, wakiwa na msaada wa wamiliki wenye nguvu kifedha kutoka UAE, wamedai kuwa City imekuwa ikitendewa isivyo haki na klabu nyingine za Ligi Kuu, huku wengine wakisema hatua hii inalenga kubomoa mfumo wa kifedha uliopo ndani ya soka la England.
Mmoja wa wanasheria wa City aliwahi kusema kuwa mmoja wa mabosi wa City, Khaldoon Al Mubarak, aliwahi kuapa kuwa “ataajiri wanasheria bora zaidi duniani kwa gharama yoyote” ili kuepuka adhabu yoyote dhidi yao kwenye kesi hiyo. Hii inaonyesha kuwa City iko tayari kwa vita virefu vya kisheria, huku ikitafuta kutetea jina lake na mafanikio yake ya soka.
City haikubaliani na makosa hayo ikionyesha ina matumaini fulani ya kushinda kesi kutokana na kile ambacho kimeshawahi kutokea kwenye kesi za namna hiyo dhidi yake huko nyuma. Waliwahi kupigwa marufuku kushiriki mashindano ya Ulaya kwa miaka miwili na shirikisho la soka Ulaya, UEFA kwa madai ya kukiuka kanuni za kifedha mnamo Februari 2020. Hata hivyo, adhabu hiyo ilifutwa na Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) mnamo Julai mwaka huo huo, mahakama ilipoamua kuwa “mengi ya makosa yaliyodaiwa hayakuthibitishwa au yalikuwa yamepitwa na wakati (nje ya muda wa ukomo wa miaka mitano wa shirika hilo)”. Katika kesi hiyo City walipigwa faini ya €10 milioni (£8.6m; $11m) kwa kutotoa ushirikiano ipasavyo wakati wa uchunguzi.
Athari za Kesi Hii kwa Soka la Ulaya na Dunia
Matokeo ya kesi hii si tu yataathiri soka la England bali pia mfumo wa kifedha wa soka zima la Ulaya. Ligi Kuu ya England imekuwa kivutio kikubwa duniani, ikiingiza mapato ya mabilioni ya fedha kupitia mikataba ya matangazo na udhamini. Kwa mfano kampunimmoja tu ya NBC ya Marekani imetoa $450 milioni kwa haki za matangazo ya Ligi Kuu, kiasi ambacho ni zaidi ya mara mbili ya mikataba ya haki ya matangazao kwa ligi kuu za La Liga (Hispania) na Bundesliga (Ujerumani).
Mikataba kama hii itakuwa ya kwanza kuathirika. Rais wa La Liga, Javier Tebas, ameonya kuwa matokeo ya kesi hii yatakuwa na umuhimu mkubwa kwa mpira wa Ulaya. Amesema, “Uendelevu wa kiuchumi wa Ligi Kuu ni muhimu ili kuzuia mfumuko wa mishahara na gharama katika nchi nyingine za Ulaya. Matokeo ya kesi ya Manchester City yatakuwa kipimo cha uadilifu wa ligi nzima.”
Wachambuzi wa kisheria wanaona kuwa City itakabiliana na changamoto kubwa, huku hukumu kama itakutwa na hatia ikitarajiwa kuwa kali, hasa kwa kushindwa kutoa ushirikiano kikamilifu wakati wa uchunguzi. Adhabu inaweza kuanzia faini kubwa hadi kukatwa alama au hata kushushwa daraja. Ligi Kuu imekuwa ikishutumiwa kwa kushindwa kutekeleza sheria zake kwa ukali, na hivyo kesi hii inaweza kuwa mtihani wa uwezo wake wa kuendesha mpira kwa haki na usawa.
Wakati uamuzi wa kesi hii ukisubiriwa kwa hamu, wengi wanajiuliza: Je, hii ndiyo itakuwa mwisho wa enzi ya mafanikio ya Manchester City, au wataponyoka tena kama ilivyokuwa mwaka 2020?