Menu
in

Manara Hii Haikubaliki Umefeli

Manara

Manara

Kuna siku niliwahi kusema kuwa hawa maafisa Habari wa kibongo tunawalea sana kuwapa ‘Airtime’ ifike wakati kama tunataka kusonga mbele basi tuachanae nao kabisa.

Inawezekana maneno yangu yakawa makali sana lakini yana ukweli ndani yake, siku moja niliwahi kuandika makala juu ya Maafisa Habari walivyokuwa maarufu kuliko wachezaji.

Sio kwa ubaya kama wamekuwa maarufu kuliko makocha au wachezaji lakini wanafanyaje kazi zao hapo ndipo kunapokuwa patamu.

Na hapa bila kuficha tuwaangalie Simba na Yanga ambao ndio mara nyingi wanakuwa maarufu kuliko wachezaji, lakini kuna wakati kauli zao mbovu sana ukitaka ukweli juu ya jambo fulani la timu wanazoziongoza wanakuwa wakali sana.

Makala yangu ambayo niliwahi kuitoa humu nilisema juu ya kufahamika kwako lakini pia wanaleta chachu gani katika soka Haji Manara nikamuweka nafasi ya kwanza kwa huduma yake kwa mashabiki na soka la Tanzania.

Ni kweli wanaleta utamu wakati mwingine wanakosa weledi kabisa na kuleta mambo ya kitoto katika taarifa zao.

Haji Manara miongoni mwa Maafisa Habari wa Simba wasiokuwa na kauli nzuri hasa unapotaka kujua jambo lililotokea katika timu yake anajidai anauchungu wa timu zaidi ya weledi.

Bahati nzuri Manara ni Mwanahabari na aliwahi kufanya kazi pale Radio Uhuru anajua yote namna ya kutafuta habari sasa imekuaje leo amekuwa ‘Unprofessional’.

Manara amekuwa mkali na kutoa maneno ya shombo kila unapotaka habari za Simba ambazo zilizokuwa na mlengo hasi.

Anaona yuko na mapenzi ya timu zaidi ya kuhudumia kiweledi ambapo sio vizuri kabisa.

Mara nyingi namsikia akihojiwa na wakati mwingine hata mimi nikifanya mahojiano naye amekuwa mkali tena kama hakujui ndio kabisa anaweza hata kuzima simu  wengine alishawahi kuwaambia kuwa hafanyi mahojiano na waandishi wadogo wasiojulikana.

Haya yote tunayalea sisi Waandishi kuwaelekeza kila jambo kwao hebu tujaribu kuwahama tuangalie kwanza upepo unaendaje.

Alichokifanya Manara alipokuwa anahojiwa na watu wa Wasafi Media juu ya ugomvi wa mshambuliaji wao Meddie Kagere dhidi ya kocha Sven Vandenbroeck kuenea mtandao na yeye kutoa maneno yasiyokuwa na maana haikubaliki.

Iko hivi, taarifa ambayo imesambaa katika mitandao ya kijamii ilihusu mshambuliaji wa Simba Meddie Kagere na kocha Sven Vandenbroeck zinaeleza kuwa wamepigana chanzo cha ugomvi huo hakijajulikana.

Ndipo kampuni ya Wasafi Media wameanza kumtafuta Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu juu ya sakata hili alijibu kuwa hakuna ugomvi juu ya tukio hilo wako shwari wote.

Lakini Wasafi Media hawakuishia hapo waliendelea kutaka habari zaidi ndipo wakampigia Haji Manara na kutaka kufahamu zaidi ndipo yalipoanza mapovu kumtoka.

Aliwaita majina mengi mabovu, aliwaita wajinga, aliwaambia ndio wanaanzisha mijadala isyokuwa na tija na mengine mengi, jamani nini maana ya habari.

Swali la kujiuliza kwani namna ya kutafuta habari kupoje wakati umepata tukio? lengo la Wasafi wapate uhakika ili wanaowasikiliza wajue kinachoendelea.

Hivi sisi Waandishi tunapangiwa cha kuandika au kusema au namna ya kutafuta habari.

Manara alisoma kweli zile 5W+H? unajua kuna vitu huwa vinaumiza bila kuvikemea vitaendelea  na natamani afoke tena juu ya hili nitaendelea kumuandika.

Kwa Waandishi ambao wameenda shule na wanajua namna ya kutafuta habari pamoja na kuweka usawa ‘Balance Story’.

Katika kuandika habari kuna kitu kinakatazwa  kinaitwa ‘Intrusion of Privacy’ yaani kuingilia uhuru wa mtu lakini kwa habari hii hakuna aliyeingiliwa uhuru wake  ni habari kama zilivyo nyingine.

Tena Manara alitakiwa ajibu vizuri  kama alivyofanya Rweyemamu angejibu alichoulizwa kila kitu kingeenda sawa.

Harafu hii sio mara ya kwanza na nyie Wasafi Media mbona kila siku mnakumbatia vitu  ambavyo havina mantiki.

Kwani lazima ahojiwe Manara ?

Mbona Magori au Hans Pope wanaongea vizuri hata kama jambo  likiwa baya au kuchafua timu wanajibu vizuri.

Niwarudishe nyuma wakati sakata la Morrison na Yanga juu ya kibali Wanachi kukibania, mlimpigia Magori mwanzo alisema tofuati ila sio kwa kashfa mara ya pili alifunguka vizuri na akaweka kila kitu sawa.

Sasa kwanini kila siku mkubali kutukanwa  na mtu mmoja ambaye yeye anajiona ndio kila kitu katika nchi.

Ukweli ni kwamba sijawahi kumchukia Manara lakini kama anavyosema yeye kuwa mtu akitaka kuichafua ‘Brand’ ya Simba anakufa naye na mimi pia mtu anapotaka kuichafua tasinia  ya Habari atufundishe namna yakutoa habari harafu hajui chochote huwa nakufa naye.

Harafu na nyie mashabiki fuata upepo kuna wakati kabla hujapiga simu kuchangia jambo jaribu kutafakari sio kwakuwa ameongea Manara ndio unaona jambo limekamilika, changanua kisha toa maoni ya kimpira.

Naamini Manara muungwana atawaomba radhi Wasafi ila sio sababu ya kuacha kuliongea na kulichukia kwa kiwango cha ‘Degree’ aache hivi vitu.

Ni kweli nishawahi kuandika kuwa Manara analifanya soka liheshimiwe kwa upande wa mazuri yake ila kwa upande huu wa kuongea mbovu amefeli kwa kiasi kikubwa.

Ajaribu kuangalia namna ya kuongea  kama anavyojiita msemaji wa taifa basi ahusike na uhusikahuo sio kutoa miboko kila wakati.

Kozi ya Habari ‘Mass Communication’ imekuwa ikidhalrauliwa sana, sio tu mashabiki kwa kuwa wanaweza kupost vitu Instagram wanajiona wanahabari ila hata Wanasiasa nao wamekuwa wakitudharau sana.

Sisi kama Waandishi tunaweza kufanya jambo na hili likaisha kabisa kazi kubwa tunafanya kisha tunaonekana wajinga kipindi hiki cha kampeni hao wanasiasa ndio wanarudi kujua umuhimu wetu.

Kwa upande wa Yanga nako tatizo lipo Hassan Bumbuli naye ukienda kumuuliza kitu kilicho ‘Negative’ ili upate uhakika anakujibu lugha mbovu kabisa.

Nilishawahi kumuhoji juu ya swala zima la Amisi Tambwe kulipwa hela zake na mustakabali wa FIFA aliniambia kuwa tuache mambo ya kijinga, hivyo vinaondoa sifa ya kuhudumia taasisi kubwa kama Yanga au Simba.

Hebu tujiulize nani anamjua Afisa Habari wa Manchester United,Arsenal,Liverpool na Chelsea, usitumie ‘Google’ jibu moyoni tu wakati unasoma makala hii, kisha nenda ‘Google’ kaangalie kama hujatumia dakika tano au sita kumjua .

Hii ni mifumo ambayo inatumika zaidi huku Afrika hasa Tanzania  kutokana na kuwa nyuma kabisa katika maendeleo ya soka, yaani Ofisa Habari anafahamika zaidi kuliko hata Kocha wa timu ?

Labda nikueleze kitu Afisa Habari wa Arsenal na timu nyingine zilizoendelea wanachokifanya kubuni mambo mbalimbali ya kihabari kwa ajiri ya watu wao, kutoa habari ambazo huwa hazina mikwaruzo kama zetu.

Miongoni mwa Maafisa Habari ambao wamepita Yanga Dismas Ten ni moja ya watu hodari sana yeye alikuwa anafuata weledi uliokuwa unatakiwa na ndio maana kila siku anahamishwa vitengo kutokana na uwezo wake mzuri.

Ningekuwa Yanga ningempa shavu kubwa sana Ten katika weledi wake anafaa sana kila mmoja shahidi, Jarida la Yanga  ambalo linaendelezwa hivi sasa, muonekanao wa jingo la Yanga kwa ndani hivi sasa moja ya mawazo yake.

Haya yote yanatokea Bongo tu hakuna sehemu nyingine na ndio maana sihami hapa.

Niwape pongezi Thobias Kifaru wa Mtibwa Sugar na Masau Bwire waRuvu Shooting  hawa watu hawana mbwembwe kabisa wanachokifanya wao kutuburudisha na maneno yao.

Written by Amini Nyaungo

For the past 9 years, I have been working as the Sports news Journalist in online and print media this experience help me to be utilized by the different sports events where I have got chances to the media as the football pundit in different media in Tanzania.

Leave a Reply

Exit mobile version