*Chelsea wawapiga PSG kwa matuta
*Arsenal wawasambaratisha Lyon 6-0
Mechi za kirafiki kabla ya kuanza kwa ligi kuu za mataifa mbalimbali zinaendelea, ambapo zile za Ligi Kuu England (EPL) zinaonekana kutamba.
Manchester United wamepata ushindi mzuri zaidi kwenye maandalizi haya ya msimu mpya baada ya kuwafunga Barcelona 3-1.
Mbele ya washabiki 68,414 katika uwanja wa Levi, Santa Clara, California nchini Marekani, nahodha Wayne Rooney na Jesse Lingard walitangulia kucheka na nyavu.
Baada ya saa moja kocha Louis van Gaal alibadili kikosi chake chote kilichoanza ili kutoa fursa kwa wengine kuonesha vitu vyao.
Bao la Barca lilifungwa na Rafinha wakati la tatu la United lilitiwa kimiani na Adnan Januzaj. Ushindi huu dhidi ya mabingwa wa Ulaya ni ishara nzuri kwa Man U ambao wameshinda mechi zao zote tatu nchini Marekani.
Watavaana na Paris Saint-Germain (PSG) Julai 29 na Van Gaal alisema upangwaji wa kikosi chake kwa mechi hizi mbili za mwisho utaashiria watakaoanza kwenye mechi dhidi ya Tottenham Hotspur siku ya kwanza ya EPL Agosti 8.
Majeraha kidogo yalimwacha nje beki wa kati wa United kutoka Bayern Munich, Bastian Schweinsteiger kama ilivyokuwa kwaMarcos Rojo aliyewasili kwa kuchelewa baada ya michuano ya Copa America.
Daley Blind anapewa nafasi kubwa zaidi kwenye beki ya kati kabla ya Chris Smalling wakati Memphis Depay anapewa jukumu la namba 10 nyuma ya Rooney.
Ashley Young, 30, anamaliza mkataba wake msimu ujao na mazungumzo hayajaanza juu ya kumwongezea mkataba. Hata hivyo alicheza vyema dhidi ya Barca.
Mchezaji aliyevunja rekodi ya usajili England, Angel Di Maria haijulikani hatima yake; hayupo na kikosi cha United na kocha Van Gaal anasema hajui kwa nini hayupo na kikosi chake.
Yapo madai kwamba Di Maria anatarajia kujiunga na PSG ambapo mazungumzo yanaendelea ili auzwe kwa pauni zaidi ya milioni 40.
CHELSEA WAWAPIGA PSG KWA MATUTA
Chelsea wamefanikiwa kuwafunga PSG kwa mikwaju 6-5 ya penati kwenye mechi ambayo Radamel Falcao wa Monaco aliyetokea Man United kwa mkopo alicheza.
Wakicheza nchini Marekani, vijana wa Jose Mourinho walimalizia vyema kwa penati ya Falcao kabla ya kipa wa The Blues, Thibaut Courtois naye kufunga ya ushindi.
Zlatan Ibrahimovic alitangulia kufunga bao kwa PSG kutoka yadi 12 baada ya shuti la Jean-Kevin Augustin kugonga mwamba.
Victor Moses mwenye utata wa wapi atacheza msimu ujao alisawazisha kutokana na pasi ya kufinyiwa na Cesc Fabregas.
Falcao aliingia katika dakika ya 69 kuchukua nafasi ya Diego Costa kwenye ushambuliaji. Juan Cuadrado aliongeza shaka ya Mourinho juu yake kwa kukosa penati wakati huu ambapo Mreno huyo anatafuta klabu ili amuuze winga huyu.
Chelsea walimwanzisha kipa wao mpya, Asmir Begovic kutoka Stoke anayechukua nafasi ya Petr Cech aliyehamia Arsenal kiangazi hiki.
Katika mechi yao ya mwisho nchini Marekani watachuana na Barcelona jijini Washington Julai 29 kabla ya kurudi England kujiandaa kwa mtangange wa kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal uwanjani Wembley Agosti 2.
ARSENAL WAWASASAMBUA LYON
Alex Iwobi amefunga bao lake la kwanza kwa Arsenal katika ushindi mnono wa 6-0 walioupata dhidi ya Lyon kwenye mechi ya kirafiki.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 19 ni binamu wa mchezaji wa zamani wa Bolton na Nigeria, Jay-Jay Okocha. Aling’ara vilivyo kwenye kipindi cha kwanza akiwa na Arsenal.
Olivier Giroud, Aaron Ramsey, Alex Oxlade-Chamberlain, Mesut Ozil na Santi Cazorla walifunga mabao mengine ya Arsenal.
Pamoja na kwamba Lyon si timu kubwa sana, Arsenal walionesha umahiri mbele ya lango na si ajabu kocha Arsene Wenger akaamua kuacha benki fedha alizopewa kwa ajili ya usajili.
Mmoja wa wakurugenzi wa Arsenal, Lord Harris amedai kwamba anaungwa mkono na bodi kutumia kiasi kikubwa cha fedha kusajili mchezaji wa kiwango kikubwa kabisa kutoka popote pale.
Arsenal wanacheza kwenye michuano ya kirafiki ya Emirates, ambapo timu nyingine zilizomo ni Villarreal wa Hispania na Wolfsburg kutoka Ujerumani