*Chelsea na PSG
Manchester United wamepangwa kucheza na Bayern Munich kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
United waliofurahia sana ushindi wao wa Jumatano dhidi ya Olympiakos katika raundi ya 16 ya michuano hiyo mikubwa barani, sasa watawavaa mabingwa watetezi, Bayern, ambao msimu uliopita na msimu huu waliwatoa Arsenal.
Kwa hali waliyo nayo, Man U ndio waliopewa droo ngumu zaidi, lakini mchezaji wa Bayern, Philipp Lahm anasema hawawezi kujidanganya wala kuchekelea, kwa sababu Man U wanao wachezaji wenye uwezo mkubwa.
Wawakilishi wengine wa England, Chelsea watawakabili wale wa kutoka Ufaransa, Paris Saint Germain wakati mabingwa wa Hispania, Barcelona watacheza dhidi ya wapinzani wao kwenye La Liga, Atletico Madrid. Katika droo nyingine, Real Madrid wa Hispania watakabiliana na Wajerumani Borussia Dortmund.
Mechi za awali zitachezwa kati ya Aprili mosi na pili wakati marudiano yatakuwa wiki moja baadaye. Fainaliz a mwaka huu zimepangwa kufanyika nchini Ureno, katika dimba la klabu ya Benfica liitwalo Estadio da Luz jijini Lisbon, Jumamosi ya Mei 24.
Ratiba hiyo imetoka siku moja bada ya Kocha David Moyes wa United kusema kwamba timu yake inaweza kutwaa taji hilo la Ulaya. United wanachukuliwa kwamba hawataweza tena kutwaa ubingwa wa England na pia ni vigumu kupata nafasi nne za juu ili wapate kushiriki UCL msimu ujao.
Mwaka 1999 Man U na Bayern walicheza kwenye fainali ya UCL, ambapo mabao ya dakika za mwisho ya Ole Gunnar Solskjaer naTeddy Sheringham yaliwapatia kombe vijana hao waliokuwa chini ya Sir Alex Ferguson.
Katika robo fainali ya msimu wa 2009/2010, Bayern waliwatoa United kwa faida ya bao la ugenini.
PSG wanaongoza Ligi Kuu ya Ufaransa kwa tofauti ya pointi nane na wamepangwa dhidi ya Chelsea ambao pia wakati wa upangaji walikuwa wanaongoza Ligi Kuu ya England kwa tofauti ya pointi nne. Chelsea hawajafungwa katika michezo yao miwili ya mwisho dhidi ya PSG.