*City, Liver, Saints safi
Mauzauza ya vigogo kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Ligi (Capital One Cup) yameendelea kwa Manchester United kuduwazwa na Middlesbrough.
United waliotoka kwenda sare na Manchester City wikiendi iliyopita kwenye michuano ya Ligi Kuu, Jumatano hii pia walitoshana nguvu na Boro kwenye mechi iliyofanyika Old Trafford, huku wageni wakiandamana na washabiki kadiri ya 10,000.
Ilikuwa changamoto ya mikwaju ya penati iliyowaadhiri Mashetani Wekundu, ambapo kwa ajabu ni kwamba wachezaji watatu wa Timu ya Taifa ya England, nahodha Wayne Rooney, Michael Carrick na Ashley Young walishindwa kutumbukiza mikwaju yao kimiani.
Katika muda wa kawaida, United nusura wachapwe, kwani mpira wa Stewart Downing ulitumbukizwa kwenye lango la Man U na mchezaji wao, Daley Blind lakini bahati yao ni kwamba mwamuzi msaidizi akasema mchezaji Kike alikuwa ameotea wakati mpira ukienda kimiani.
Middlesbrough wameonesha kiwango kizuri na uwezekano wa kurejea Ligi Kuu ambako walicheza mara ya mwisho msimu wa 2008/9. Hivi sasa, kikosi hicho cha kocha Aitor Karanka kinashika nafasi ya nne katika Ligi Daraja la Kwanza (Championship).
MAN CITY NA MAUAJI KWA PALACE
Manchester City wameendelea kuonesha maguvu katika kupata ushindi kwa idadi kubwa ya mabao, baada ya kuwabomoa Crystal Palace kwa mabao 5-1, huku Kevin De Bruyne akifunga bao lake la sita katika mechi tisa.
Ameitafsiri thamani yake kwa vitendo, kwani alinunuliwa kwa pauni milioni 54 kiangazi kilichopita kutoka Wolfsburg, baada ya Chelsea kuwa wamwita garasa hapo awali. Mabao mengine ya City yalifungwa na Wilfried Bony, kinda Kelechi Iheanacho, Yaya Toure na Garcia Alonso. Palace walifunga kupitia kwa Damien Delaney.
KLOPP APATA USHINDI WA KWANZA LIVERPOOL
Hatimaye kocha mpya wa Liverpool, Jurgen Klopp amepata ushindi wa kwanza. Nao umekuja kwenye michuano ya Kombe la Ligi, kwa bao la mapema la Nathaniel Clyne dhidi ya Bournemouth lililowapeleka Liver robo fainali ya michuano hiyo.
Nusura Klopp aambulie sare ya nne mfululizo kama si kipa wake, Adam Bogdan kuzuia kwa miguu mpira wa Junior Stanislas aliopiga karibu na ukiwa unaelekea nyavuni. Liver walionekana wachovu kwenye ushambuliaji, hasa baada ya Christian Benteke kuungana na Daniel Sturridge nje ya dimba baada ya kuumia. Wote wanaumwa magoti.
Ilibidi Klopp atie imani yake kwa Divoc Origi, Mkenya ambaye pia ni raia wa Ubelgiji na Roberto Firmino aliyesajiliwa kwa pauni milioni 29 kiangazi kilichopita lakini hajaonesha makeke.
Liverpool wanashikilia rekodi ya kutwaa kombe hili mara nyingi zaidi – nane, na huenda Klopp akawasaidia kulitwaa kwa mara ya tisa. Mabingwa watetezi, Chelsea na Arsenal walitolewa Jumanne. Wengine waliovuka kuingia robo fainali ni Everton, Hull, Sheffield Wednesday na Stoke.