*Eto’o wa Chelsea awaangamiza kwa hat trick
*Arsenal, Man City waendelea kutesa kileleni
Manchester United wapo katika hali mbaya msimu huu wa ligi baada ya kupoteza mechi ya kukata na shoka dhidi ya Chelsea kwa mabao 3-1.
David Moyes alikuwa amewekwa katika mtego kwenye mchezo huu muhimu, ambapo licha ya kuanza vibaya ligi hii, alitakiwa kushikilia rekodi ya Man U kuwashinda Chelsea katika mechi zao nyingi.
Mshambuliji wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o alifunga mabao hayo katika dakika za 17, 45 na 49 na kujijengea jina kubwa kote katika dimba la Stamford Bridge na nje yake.
Bao la kufutia machozi la Manchester United lilifungwa na Javier Hernández katika dakika ya 78 lakini halikutosha kuwaondosha wana Old Trafford katika aibu ya mwaka huu.
Kwa ushindi huo, Chelsea wanakuwa nyuma ya Arsenal kwa pointi mbili wakati Manchester City wanawapumulia kwa tofauti ya pointi moja. Arsenal wana pointi 51.
Moyes alionekana mwenye kusononeka kwa sababu anatofautiana kwa pointi 14 kwa hasi na vinara wa ligi hiyo Arsenal katika mzunguko huu wa 22.
Nahodha wa United, Nemanja Vidic alipata kadi nyekundu kizembe baada ya kumchezea vibaya Eden Hazard.
Kocha Moyes anaweza kujitetea kwamba hakuwa na vinara wake wa upachikaji mabao, Wayne Rooney na Robin van Parsie lakini matokeo yanabaki kuwa hayo hayo.
Katika mechi nyingine, Tottenham Hotspur walifanikiwa kupachika mabao 3-1 dhidi ya Swansea katika siku ambayo mchezaji aliyekuwa ametupwa benchi, Emmanuel Adebayor alifanya mambo makubwa mchezoni, ikiwa ni pamoja na kupachika mabao mawili.
Kwa matokeo hayo, Arsenal wanabaki vinara kwa pointi zao 51 wakifuatiwa kwa tofauti ya pointi moja moja na Manchester City na Chelsea.
Chelsea wanafuatia wakiwa na pointi zao 49 wakifuatiwa na Liverpool wenye 43 sawa na Spurs.
Everton wanafuatia kwenye msimamo wakifuatiwa na Manchester United, Newcastle, Southampton, Aston Villa, Hull, Norwich, Stoke, West Brom, Swansea, Crystal Palace, Fulham, West Ham, Sunderland na Cardiff mkiani.