*Faida yashuka kwa 10% katika miezi mitatu
Manchester United wamesema kwamba hapatakuwa na usajili wowote katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo Januari mwezi mmoja unusu ujao.
Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa United, Ed Woodward amesema hawana mpango wa kuimarisha kikosi chao, ambacho wametumia pauni milioni 150 majira ya kiangazi kukiweka kilivyo chini ya kocha mpya Louis van Gaal.
Woodward amesema hayo wakati ambapo Manchester wameshuhudia kushuka kwa faida kwa asilimia ell by 9.9 hadi kufika pauni milioni 88.7 katika kipindi cha miezi mitatu kilichoishia Septemba mwaka huu.
Mtendaji huyo amesema kwamba faida hiyo ingeweza kushuka zaidi kama si kuongezeka kwa fedha za wadhamini na ankara ya mishahara kupungua. Amesema kwamba hesabu za mwaka wa fedha 2014/15 zitzidi kushuka kwa sababu timu yao haipo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo amesema kwamba klabu imefanikiwa kutiliana saini mkataba mzito wa udhamini, mkataba aliosema ni wa kihistoria kwani hawajawahi kupata kiasi hicho, akisema hiyo itasaidia katika kuijenga klabu hiyo.
Mkataba huo wamefanya na Adidas utakaoanza msimu wa 2015/16 kwa miaka 10 na thamani yake ni pauni milioni 750.
Kwa upande wa usajili, alisema hawataki kumaliza matatizo yao kwa mipango ya muda mfupi, na kwamba wanaweza kufikiria tena iwapo wachezaji ambao waliwapania kwa muda mrefu watapatikana.
Katika pauni milioni 150 walizotumia msimu wa kiangazi, walisajili wachezaji ghali kama Angel Di Maria aliyevunja rekodi ya klabu, kwani waliwalipa Real Madrid pauni milioni 59.7 kwa ajili ya winga huyo.
Wachezaji wengine waliotua Old Trafford ni akina Ander Herrera (£28m), Luke Shaw (£27m), Marcos Rojo (£16m) na Daley Blind (£13.8m). Radamel Falcao aliingia kwa mkopo wa pauni milioni sita kwa msimu.
Hata hivyo, pamoja na usajili huo klabu imekumbwa na mkururo wa majeruhi, ambapo kwa sasa wanao karibu 10. Woodward amesema mipango yao ni kusubiri hadi msimu ujao wa kiangazi ili kuona cha kufanya.