Menu
in , , ,

Man U wamwendea Sanchez

Tanzania Sports

*Wanatoa ofa kubwa kuliko Man City

*Theo Walcott anakwenda Everton?

MAMBO yanazidi kunoga kwenye Dirisha la Usajili, ambapo Manchester United wameingia kwenye vita dhidi ya Manchester City kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji wa Arsenal, Alexis Sanchez.

City waliomkosa Sanchez siku ya mwisho ya usajili kiangazi mwaka jana, walitarajia kumpata kwa ulaini Januari hii au hata kusubiri kiangazi mwaka huu mkataba wake utakapokuwa umemalizika, lakini sasa wanaona kuna ushindani.

Wakati Man City wametoa dau la pauni milioni 20 tu, huku Arsenal wakitaka pauni milioni 35, Manchester United wameweka mezani pauni milioni 25 wakimwita Sanchez ambaye inaaminika kwamba hata hivyo alishaanza mazungumzo na City.

Taarifa zinasema kwamba Jose Mourinho anachuana na jirani hasimu wake, Pep Guardiola mwenye kikosi imara na ongozi kwenye ligi msimu huu, ambapo inadaiwa Sanchez amepewa ofa ya mshahara wa pauni 250,000 kwa mwezi huko City.

Arsenal wamekuwa katika mazungumzo na City tangu walipowasilisha dau hilo dogo kwa vile hapakuwapo ushindani sana dhidi ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Chile mwenye umri wa miaka 29. United pia wanataka kumpa Sanchez mshahara mkubwa zaidi ya uliotolewa na City.

Hata hivyo, baada ya Sanchez kucheza chini ya Guardiola akiwa Barcelona, si ajabu akapenda kwenda City lakini pia matajiri hao wa Etihad wanaweza kuongeza dau la ada na mshahara kwa mchezaji ambaye akibaki Emirates ataondoka kiangazi pasipo Arsenal kupata hata senti tano.

Mourinho anampa hasimu wake, Arsene Wenger wa Arsenal ofa nyingine, nayo ni kumsajili Henrikh Mkhitaryan, lakini kikwazo kinaweza kuwa kwa raia huyo wa Armenia kulipwa mshahara wa kwenye pauni 200,000, kiasi kikubwa ambacho Arsenal hawangependa kutoa. Wawakilishi wa Sanchez walizungumza na City kiangazi na kukubaliana lakini wakakwamishwa dakika ya mwisho baada ya Thomas Lemar wa Monaco kukataa kujiunga na Wenger.

Safari hii wakuu wa Arsenal wameshakubaliana kwamba wamuuze Sanchez, lakini baada ya kupata mbadala wake ambaye kipaumbele kimewekwa kwa Mbrazili Malcom (20) wa Bordeaux na walishafanya majadiliano ya awali na wawakilishi wake. United na Tottenham Hotspur wamepata kuhusishwa na Malcom katika wiki zilizopita.

Bordeaux wanataka ada ya walau pauni milioni 44.5 na wangependa kubaki na mchezaji huyo hadi mwisho wa msimu na hali inazidi kuwa tata kutokana na haki miliki yake, ambapo klabu hiyo ya Ufaransa ina umiliki kwa asilimia 50 tu na zilizobaki ni mawakala wengine.

Wakati huo huo, Everton wamefungua majadiliano rasmi juu ya kumsajili winga Mwingereza wa Arsenal, Theo Walcott Januari hii, kocha Sam Allardyce ‘Big Sam’ akitaka kuimarisha kikosi chake, akimuona Walcott (28) kuwa ni hatari sana kwenye kupachika mabao.

Allardyce amesema kwamba mazungumzo yalikuwa yakifanyika, uwezekano mkubwa unaotafutwa ukiwa ni kumsajili moja kwa moja na si kumchukua kwa mkopo. Everton waliomuuza mshambuliaji wao mkuu, Romelu Lukaku kiangazi mwaka jana, wapo tayari kuwapa Arsenal pauni milioni 20 na kumhakikishia muda mwingi wa kucheza.

Walcott ametwaa Kombe la FA na Arsenal mara mbili, ambapo amecheza mechi 395 kwa klabu hiyo lakini msimu huu amepewa dakika 47 tu za Ligi Kuu ya England (EPL), akitumwa zaidi kucheza kwenye mechi za makombe mengine ambazo si kubwa kama za EPL.

Manchester United pia wameulizia juu ya washambuliaji wengine wawili – Yule wa Leicester, Jamie Vardy (30) na wa West Ham kutoka Mexico, Javier Hernandez aliyekuwa Old Trafford kati ya 2010 hadi 2015. Klabu ya Ligi Kuu ya Marekani, Los Angeles FC nao pia wanamtaka Hernandez.

Manchester United na Chelsea wanataka kumsajili kiungo mchezeshaji wa Brazil, Arthur Melo (21) anayekipiga Gremio. Liverpool wapo kwenye mazungumzo na winga wa Leicester kutoka Algeria, Riyad Mahrez, lakini jamaa huyo mwenye umri wa miaka 26 anataka kwenda Arsenal alikokataa majuzi

Liverpool wanawasiliana rasmi na RB Leipzig ili kumpata mshambuliaji wao, Naby Keïta kuziba nafasi ya Philippe Coutinho aliyekwenda Barcelona, lakini wanaambiwa itabidi waongeze fedha, kwa sababu wangependa kumwona akiondoka kiangazi na si Januari hii.

Liverpool wanataka kumuuza Daniel Sturridge (28) kwa pauni milioni 30, lakini vikwazo ni majeraha yake ya mara kwa mara yanayomfanya kutokuwa timamu muda mwingi, bei wanayotaka lakini pia mshahara wake mkubwa wa £150,000- kwa wiki.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version