Mechi baina ya Manchester United na Liverpool ililazimika kuahirishwa baada ya fujo za washabiki wa Man U walioandamana hadi uwanjani kwao Old Trafford.
Polisi waliingilia kati na kuwarudisha nyuma washabiki hao waliokuwa wanawapinga wamiliki wa klabu – Familia ya Glazers, malalamiko yakiwa juu ya kitu kilichopotezwa na ambacho huenda kisirudi tena kwenye soka.
Mapema wikiendi hiyo, hali ya hewa ilionekana kutokuwa nzuri, na baadhi ya washabiki wakafanikisha azma yao ya kuingia uwanjani kabisa, wakisukumwa na kile kinachoonekana kuwa hasira kali.
Wengine walibaki nje wakiandamana kuwapinga wamiliki. Ili kuelewa moto wa maandamano na upinzani unaokabili klabu mbalimbali kubwa wakati huu, lazima kutazama na kufikiria mambo mengi yanayotokea kwenye klabu husika.
Aina ya utawala kwenye klabu umekuwa ukipingwa lakini pia uongozi wa wakurugenzi mbalimbali pamoja na kufanya vibaya kwa klabu tofauti na ama kujiingiza au kujiondoa kwenye mashindano Fulani au kushindwa kufuzu hatua mbalimbali.
Washabiki wa United waliozingira uwanja ambao umezungukwa na maduka makubwa ya kisasa, walisikika wakisema; “tunaamua lini mtacheza. Tunawataka Glasers waondoke.”
Walikuwa pia wakiimba, huku wamiliki wakiwa hawapo, tena wakiwa mbali sana kwa kuvuka bahari kubwa – Marekani.
Palikuwapo na mabango yaliyotoa ujumbe kwa wamiliki hao matajiri. Baadhi ya washabiki walifanikiwa kuvunja vioo na wengine kuingia kwenye dimba nyasini kabisa. Kulikuwa na hali ya hatari isiyotakiwa kwenye soka lakini ndio hivyo, Ligi Kuu ya England (EPL) ilikuwa imepatwa.
Yalikuwa maandamano na mabango yaliyoonekana kama njia ya mwisho ya kukabiliana na wamiliki hao. Yameonesha ni wapi nguvu ipo na udhaifu baina ya wamiliki, viongozi na washabiki. Walikwenda pia kinyume cha kanuni za kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.
Washabiki wanaonekana kwamba wamekata tamaa na Jumapili hiyo ilikuwa nyeusi kwao na wadau wa Old Trafford. Kitu kilicholipua moto huo ni suala la European Super League, lakini ukosefu wa kuaminiana ulianza siku nyingi.
Washabiki wanataka Glazers waiuze klabu, lakini hawawezi kulazimishwa kufanya hivyo kwa sababu ni mali yao. Ni wazi kwamba iliposimamia ligi hii ya England si imara kama ilivyopata kuaminiwa. Tutarajie maandamano na mabango zaidi huko tuendako.