Menu
in

Man U hawataki mkurugenzi wa soka

Tanzania Sports

Kiangazi cha mwaka huu kitashuhudia kutimia miaka miwili tangu Manchester United walipotangaza kuanza kumtafuta mkurugenzi wa soka.

Washabiki wamekuwa wakishangaa kwamba imechukua muda mwingi kiasi hiki kupata mtu sahihi kwa kazi hiyo wakati katika kipindi hicho hicho maghorofa marefu sana tisa yamejengwa jijini.

Pengine ichukuliwe kwamba kumpata kiongozi mwandamizi kama huyo hapo Old Trafford si suala la utelekezaji wa haraka kama ilivyokuwa ikifanywa awali kwa watu kama makocha.

Kumpata mkurugenzi wa soka ilionekana kuwa moja ya vipaumbele wakati wa kocha Jose Mourinho, akiwa kwenye harakati za usajili kiangazi cha 2018. Kwa sasa, washabiki wanatakiwa kuelewa kwamba utafutaji wa mtu kwenye nafasi hiyo haupo tena kwenye ajenda, au walau si kipaumbele.

United hawatafuti mtu wa aiona hiyo kwa ajili ya kuongoza sera hasa katika masuala ya usajili, ambaye angesaidiana na kocha. Katika klabu nyingine, mkurugenzi wa soka au mkurugenzi wa michezo – ana ushawishi mkubwa katika maeneo ya usajili na utendaji wa siku hadi siku klabuni. Huwa na wajibu wa kusaka wachezaji wa kuongeza klabuni na hata kuchagua makocha wanaoona wanafaa kwa klabu zao.

Klabuni Manchester United, mfumo ni tofauti. Kimsingi hadhi ya kocha ni kubwa na klabu wanaonekana kwamba bado wanataka kuona kwamba kocha anabaki katika hadhi aliyokuwa nayo Sir Alex Ferguson ambaye ‘hakuwa anaambiwa kitu’ katika mipango yake.

Kwa sasa wanaye kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye hujadiliana moja kwa moja katika ngazi ya juu na Makamu Mwenyekiti Mtendaji, Ed Woodward na inaelezwa kwamba uhusiano wao ni ‘muhimu’. Lakini linapokuja suala la kuajiri na kufukuza, basi uamuzi upo mikononi mwa Woodward aliyebaki kuaminiwa na wamiliki wa klabu – Familia ya Glazer – hata baada ya makocha David Moyes, Louis van Gaal na Mourinho kuajiriwa na kufukuzwa.

Kuajiri na kufukuza kulikokuwa kwa gharama kubwa Old Trafford katika kipindi hicho, wakati kila mmoja alipoingia akapewa mkataba na fedha na kisha kuondoshwa na kulipwa fidia kunawezakuchunguzwa na ndiyo maana wengi katika sekta ya soka wanaona kwamba United wangefaidi zaidi iwapo wangekuwa na endelevu katika uchaguzi wa wachezaji chini ya mkurugenzi wa soka.

Hiyo ni hoja iliyopata kutolewa na Luis Compos – Mkurugenzi wa Soka wa Lille Oktoba mwaka jana. Ofisa huyu amenunua na kuuza wchezaji kama akina Fabinho, Bernardo Silva, Thomas Lemar, Anthony Martial na Nicolas Pepe na alifanya kazi na Mourinho klabuni Real Madrid.

Kadhalika, imetokea kwamba alipata kuhusishwa na kuhamia United, tena ilikuwa mwaka huu, likiwa ni jina la karibuni zaidi kutajwa katika mpango wa United kumpata mkurugenzi wa soka kwa ajili ya kuhakikisha wanapata wachezaji sahihi na kupata soko la kuuza wengine kupitia kwake.

Lakini sasa kiangazi kinakaribia huku soka ikiwa imesimama kutokana na janga la virusi vya corona vinavyosababisha hoa kali ya mapafu, lakini usajili utakuwapo baada ya kumalizwa msimu kwa namna yoyote itakayoamuliwa na waratibu na klabu husika za Ligi Kuu ya England (EPL).

Taarifa kwenye vijiwe vya soka pia zikawa zinataja kwamba kulikuwapo mazungumzo yaliyofikia pazuri baina ya United na Antero Henrique, mtu aliyemnyakua Kylian Mbappe na kumwingiza Paris Saint-Germain (PSG).

Pamekuwapo pia ngazi mbalimbali za majadiliano na watawala wenye uzoefu kama aliyekuwa Mkurugenzi wa Soka wa Everton, Steve Walsh; Mkuu wa Usajili wa zamani wa Tottenham Hotspur, Paul Mitchell; Mkuu wa Michezo na Maedeleo wa Red Bull, Ralf Rangnick; Stuart Webber wa Norwich City na golikipa wa zamani wa Man United, Edwin van der Sar ambaye sasa ni Mtendaji Mkuu wa Ajax.

Mchakato wa kumpata mkurugenzi wa soka haukuishia kwa watu hao, kwa sababu mazungumzo yalifanywa pia na wachezaji wa zamani wa hapo hapo Old Trafford, wakiwamo Rio Ferdinand, Patrice Evra, Nemanja Vidic na Darren Fletcher — lakini imekuja kuonekana kwamba hakuna nia ya dhati ya kupata mtu wa kukalia kiti hicho kilichobaki tupu hadi sasa.

Ukweli mrahisi ni kwamba, ikitokea mtu akapewa nafasi hiyo, hatakuwa na nguvu wala ushawishi na kocha atabaki kuwa kinara kwenye soka hapo, awe ni huyu aliyepo au mwingine kuletwa. Majukumu kwa sasa yamewekwa kwa aina kwamba menejimenti ya soka inaongozwa na kocha Solskjaer na Mike Phelan wakati kwenye usajili bado Solskjaer yupo pamoja na Marcel Bout, Mick Court na Jim Lawlor.

Wakati washabiki wakisubiri kuona mtu akiletwa kuchukua nafasi hiyo, menejimeti inaelekea kujiamini katika mfumo wa sasa wanaoona kwamba utamaanisha uthabiti kwa uendelevu wa kikosi. Ukweli ni kwamba mkurugenzi wa soka ndiye angeweka uthabiti na uendelevu wa kikosi pale kocha anapoondoka na kuja mpya, asipewe nafasi ya kufumua kikosi na kupanga kipya.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version