*United wamenyeka ushindi wa 1-0
Nguvu ya Manchester City imedhihirika baada ya kuweza kushinda ugenini nyumbani kwa timu kubwa, tena katika mashindano ya kimataifa.
Vijana hao wa Maniel Pellegrini walikuwa na udhaifu wanapocheza ugenini hata kwenye ligi ya ndani, lakini usiku wa Jumanne hii waliwafunga mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), Bayern Munich 3-2.
City walikatisha ushindi wa mechi 10 mfululizo za UCL wakalingana kwa pointi 15 lakini Wajerumani wapo juu kwa uwiano mzuri wa mabao.
Bayern walianza kuwaadhibu City kupitia kwa Thomas Muller dakika ya tano tu na Mario Gotze dakika saba baadaye.
Hata hivyo, Man City walijipanga na dakika ya 28 David Silva alichomoa moja baada ya kupata majalo ya Jesus Navas, Aleksandar Kolarov akasawazisha kwa penati baada ya James Milner kuchezewa rafu dakika ya 59 na dakika mbili tu baadaye Milner mwenyewe akacheka na nyavu kuandika bao la ushindi.
UNITED WAFURUKUTA KULINDA HADHI
Katika mechi nyingine, Manchester United walipigana kufa na kupona kulinda hadhi yao Old Trafford baada ya kuwa wamefungwa katika mechi mbili mfululizo hapo.
Walikabiliana na Shakhtar Donetsk katika mchezo wa kukamilisha ratiba kwani Man U walishafuzu na wakapata ushindi mwembamba wa bao 1-0.
Hata hivyo ushindi huo ni muhimu, kwani wameshika nafasi ya kwanza kwenye kundi lao na hivyo watapangwa na timu isiyokuwa kali kwenye hatua za mtoano.
United walinusurika kufungwa mara kadhaa na wakati wote kocha David Moyes aliye kwenye shinikizo alionekana kutokuwa na raha, na ilikuwa hadi kipindi cha pili Phil Jones alipofunga na kuwapoza washabiki.
THELUJI YAKWAMISHA MECHI
Nchini Uturuki, mechi baina ya Galatasaray na Juventus ya Italia iliahirishwa baada ya kuchezwa kwa dakika kadhaa.
Uamuzi huo ulifikiwa baada ya jitihada za kusafisha uwanja kwenye mistari na miduara inayogawanya dimba kuonekana haingesaidia sana.
Mechi iliendelea kuchezwa huku theluji ikianguka na pia barafu, na mwamuzi aliamua kuwaita wachezaji na maofisa kisha wakapelekwa vyumbani na kazi ya kusafisha theluji ikaanza.
Pamoja na kuisafisha, wafanyakazi walijaribu kuchora upya mistari na miduara kwa kutumia rangi nyekundu kwa sababu iliyokuwapo ni nyeupe inayofanana na theluji kiasi cha kuwapa shida waamuzi kutambua iwapo mpira umepitiliza eneo husika.
Hata hivyo, baadaye zoezi lote hilo lilionekana kwamba halingeweza kukidhi chochote, kwa sababu theluji ilizidi kuanguka kwa wingi, ndipo mechi ikaahirishwa na inatarajiwa kuchezwa Jumatano hii.
MATOKEO MENGINE YA UCL
Katika mechi nyingine za mwisho kwenye makundi zilizochezwa Jumanne hii, Real Socieadad walilala 0-1 kwa Bayer Leverkusen, FC Copenhagen nao wakapoteza 0-2 kwa Real Madrid.
Benfica walifanikiwa kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Paris Saint Germain, Olympiakos wakawafunga RSC Anderlecht 3-1 na Viktoria Plzen wakawafunga CSKA Moscow 2-1.