Manchester City wamanza kwa nguvu Ligi Kuu ya England (EPL) kwa kuwacharaza West Bromwich Albion 3-0.
Katika mechi iliyochezwa Jumatatu hii usiku, vijana wa Manuel Pellegrini walitumia kiungo, Yaya Toure aliyepachika mabao mawili mapema dakika ya tisa nay a 24.
Nahodha wa City aliyemaliza msimu uliopita akiwa chini katika kiwango, Vincent Kompany alitia bao la tatu. Beki huyo wa kati alifunga bao maridadi la kichwa dakika moja kabla ya kutimia saa nzima ya mchezo.
Ilikuwa mechi ambayo Man City walimuanzisha mshambuliaji wao aghali zaidi, Raheem Sterling aliyesajiliwa kwa pauni milioni 49 kutoka Liverpool kiangazi hiki.
Macho yote yalikuwa kwa Sterling, 20, wakitarajia atambe lakini alikuwa Toure na kiungo mchezeshaji wa Hispania, David Silva waliong’ara zaidi na kuna utata juu ya nani hasa alifunga bao, kwani shuti la Toure lilimparaza Silva kabla ya kumparaza tena beki wa West Brom, Craig Dawson.
Kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, Sterling alikuwa katika nafasi nzuri ya kufunga bao akiwa mwenyewe na kipa Boaz Myhill lakini alimpelekea karibu mno, hivyo akaokoa.
Katika hatua nyingine, Chelsea wanakata rufaa kupinga kadi nyekundu aliyopewa kipa wake namba moja, Thibaut Courtois aliyooneshwa kwenye mechi ya kwanza ya EPL dhidi ya Swansea.
Kipa huyo alitolewa nje baada ya kumwangusha mshambuliaji Bafetimbi Gomis ambaye baada ya hapo alifunga penati iliyotolewa, golini akiingia kipa namba mbili, Asmir Begovic.
Kocha Jose Mourinho alikataa kujadili uamuzi wa kumtoa nje kipa huyo, na sasa wamekata rufaa ili awepo kwenye mechi ya wikiendi ijayo dhidi ya Manchester City.
Katika mechi hiyo, Chelsea walikwenda sare ya 2-2 na Swansea, ukiwa si mwanzo mzuri wa kutetea taji lao walilotwaa msimu uliopita.
Chama cha Soka (FA) cha England kinatarajia kutoa uamuzi wa kadi hiyo nyekundu Jumanne hii. Ligi hiyo inaendelea Ijuma, ambapo Aston Villa watawaalika Manchester United.