*Spurs, Villa wawapiga Cardiff, Norwich
Manuel Pellegrini amefanikiwa kupata kombe la kwanza akiwa na Manchester City na sasa anawinda mengine matatu.
Pellegrini aliyerithi mikoba ya Roberto Mancini msimu huu, aliwaongoza vijana wake kuwafunga Sunderland 3-1 na kutwaa Kombe la Ligi katika uwanja huru wa Wembley Jumapili hii.
Sunderland walipambana katika harakati za kutafuta kombe la kwanza kubwa tangu 1973 walipotwaa Kombe la FA kwa kuwafunga Leeds United na walitangulia kuwapiga City kwa bao safi la Fabio Borini katika dakika ya 10 tu ya mchezo.
Hata hivyo, Yaya Toure alisawazisha bao hilo kwa mkwaju aliopiga akiwa umbali wa yadi 25 katika dakika ya 55 kabla ya Sami Nasri kufunga bao zuri na kubadilisha kabisa mwenendo wa mchezo huo na kuweka hai matumaini ya kutwaa taji, baada ya msimu uliopita kupigwa na Wigan Athletic katika fainali ya Kombe la FA.
Jesus Navas aliyeingia kipindi cha pili alifunga bao la tatu dakika ya mwisho ya mchezo na kuwa pigo kubwa kwa Black Cats, hasa ikizingatiwa jinsi walivyojitahidi katika muda wote wa mchezo kuwakabili City.
Pellegrini alisema kwamba anataka kutwaa makombe yote manne msimu huu, yakiwa ni ubingwa wa England, Kombe la FA na Kombe la Mabingwa wa Ulaya. Hii ni mara ya tatu kwa City kutwaa kombe hili la ligi, mara ya kwanza ikiwa ni 1970 walipowashinda West Bromwich Albion, mwaka 1976 dhidi ya Newcastle United lakini miaka miwili kabla ya hapo walipoteza kwenye fainali dhidi ya Wolves.
SPURS, VILLA WAWAPIGA CARDIFF, NORWICH
Katika mechi za Ligi Kuu ya England, Tottenham Hotspurs walifaidika na bao moja dhidi ya Cardiff na kujiimarisha katika kufukuzia nafasi nne za juu msimu huu ili ije kuweza kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu ujao.
Spurs walipata bao hilo kupitia kwa Roberto Soldad, likiwa ni bao lake la kwanza katika mechi tisa licha ya kuwa ni mshambuliaji aliyesajiliwa kwa bei kubwa na kuwasogelea Manchester City walio nafasi ya nne.
Katika mechi nyingine, Aston Villa waliwaduwaza Norwich City kwa kuwakandamizia mabao 4-1 licha ya kutangulia kufungwa mapema kipindi cha kwanza. Zilikuwa dakika 15 za aina yake, ambapo Villa walicharuka na kufunga mabao bila huruma.
Kwingineko, Swansea walikwenda sare ya 1-1 na Crystal Palace katika mechi iliyochezwa Wales.
Kwa matokeo ya jumla ya mwisho wa wiki, Chelsea wanaongoza wakiwa na pointi 63 wakifuatiwa na Liverpool na Arsenal wenye pointi 59 kila mmoja, Man City anazo 57 na Spurs 53. Hata hivyo, Man City ana michezo miwili mkononi.
Nafasi tatu za mwisho zinashikwa na Sunderland wenye pointi 24 na michezo miwili mkononi, Cardiff pointi 22 na Fulham wamejituliza mkiani kwa pointi zao 21.