Menu
in , , ,

MAN CITY WATATWAA UBINGWA MSIMU HUU?! SABABU TANO HIZI HAPA

Pengine ni mapema mno kutabiri ni timu gani itatwaa ubingwa wa EPL msimu huu. Lakini zikiwa zimechezwa mechi mbili tu kwa kila timu tayari siioni timu yoyote ambayo itaweza kumaliza juu ya Manchester City ambao tayari wapo kileleni mwa msimamo wa EPL. Hizi hapa ni sababu kuu tano zitakazokufanya ukubaliane na utabiri huu.

1) UTULIVU WA MANUEL PELEGRINI

Kocha huyu kwa sasa anaonekana kuwa kwenye utulivu wa hali ya juu. Hii ni baada ya kurefusha mkataba wake na wakali hawa wa Etihad mapema mwezi huu ambao utamuweka Etihad mbaka Juni 2017. Jambo hili linamfanya aweze kujiamini na kupata utulivu wa kutosha na hivyo atalekeza mawazo yake yote kwenye malengo yake ya kutwaa ubingwa wa EPL kwa mara ya pili.

2) USAJILI WA UHAKIKA

Usajili uliofanywa na timu hii kwa ajili ya msimu huu ni usajili wa uhakika. Raheem Sterling na Fabian Delph wameongeza nguvu Etihad. Sterling ameshaonyesha makali yake kwenye michezo miwili ya kwanza hasa ule wa dhidi ya Chelsea ambapo aliwanyanyasa mno walinzi wa Chelsea.

Delph ni majeruhi lakini atarejea hivi karibuni na naamini atakuwa mbadala sahihi wa Toure Yaya ikiwa atalazimika kukosekana kikosini kutokana na majeruhi ama sababu nyingine.

Zaidi ya yote Man City wamemsajili beki kisiki Nicholas Otamedi. Mlinzi huyu ambaye alikuwa akisakwa pia na Manchster United atajumuika na Kompany na kuunda ukuta wa chuma.

3) UDHAIFU WA WASHINDANI WAKUU

Timu zenye dhamira ya kuwania taji msimu huu hazina uimara unaotosha kushindana na makali ya Man City. Timu hizo ni Arsenal, Chelsea, Liverpool na Manchester United.

Chelsea ambao wanajaribu kutetea taji lao msimu huu wameshaonyesha udhaifu kwenye ulinzi. Wameruhusu mabao matano kwenye mechi mbili. Hili ni jambo baya mno kwa kuwa Mourinho amekuwa akitegemea uimara wa safu ya ulinzi kushinda mataji.

Ivanovic na John Terry ambao ni kati ya walinzi tegemeo kwenye timu hii wameonyesha kushuka kiwango. Hata Mourinho ameonyesha kulitambua hili kwa kumtoa uwanjani Terry kwa mara ya kwanza tangu awe mwalimu wa Chelsea kwenye mchezo dhidi ya Man City wiki iliyopita.

Wapinzani wengine niliowataja hapo juu bado wanazitegeneza timu zao. Hawana vikosi vinavyotosha kupambana na Man City.

4) TOURE YAYA

Toure Yaya amerudi kwenye ubora wake. Kiwango alichokionyesha kwenye michezo miwili ya kwanza ni kiwango cha Toure tanayemfahamu. Anafanya kazi kubwa mno kwenye kulinda na kushambulia.

Msimu huu atakuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Manchseter City. Atawakinga kiasi cha kutosha walinzi wa timu yake kwa kuwazima viungo wa timu pinzani kwenye michezo yote rahisi na migumu.

Vilevile atawawezesha kina David Silva, Raheem Sterling na Sergio Aguero kuonyesha uwezo wao kwenye mashabulizi kwa kuwa atawasambazia mipira ya kutosha akisaidiana na viungo wengine.


5) SERGIO AGUERO

Hii ni mashine ya mabao. Msimu uliopita alifunga mabao 26 na kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa EPL. Sitashangaa iwapo atafunga zaidi ya idadi hiyo ya mabao msimu huu.

Tayari ameshafunga bao moja kwenye mechi aliyoanzishwa msimu huu. Kwa aliyepata fursa ya kulitazama bao lile ambalo mshambuliaji huyu alifunga dhidi ya Chelsea atakubaliana na mimi kuwa hakuna safu ya ulinzi yenye ubavu wa kumzuia asionyeshe vitu vyake.

Nafikiri Man City watakuwa vinara wa mabao kwenye EPL msimu huu kama ilivyokuwa msimu uliopita na sehemu kubwa ya mabao yatafungwa na mshambuliaji huyu hatari.

Advertisement

Written by Kassim

Exit mobile version