*Cardiff, Fulham washuka daraja
Mwenendo wa ubingwa wa England sasa unatoa nafasi kubwa kwa Manchester City.
Baada ya kupambana kwa tabu kwenye uwanja wa ugenini, Man City walifanikiwa kuibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Everton waliokuwa pia wakipambana kuwania nafasi ya nne.
Timu zote sasa zikiwa zimebakisha mechi mbili ambapo pazia linashushwa Jumapili ijayo, kuna uwezekano wa bingwa kupatikana siku ya mwisho, tena kwa tofauti ya mabao, kwani sasa Man City na Liverpool wanafungana kwa pointi lakini vijana wa Manuel Pellegrini wanaongoza kwa tofauti ya mabao.
Kuteleza kwa yeyote kati yao atamwacha mwenzake atangazwe bingwa mpya na wote wakiteleza wanaweza kuwapa nafasi Chelsea wanaonyemelea. City wanamalizia michezo yao nyumbani kwa kucheza na Aston Villa na West Ham United wakati Liverpoo wana safari ngumu ya Crystal Palace Jumatatu hii kabla ya kumaliza na Newcastle dimbani Anfield.
Chelsea wamebakiza mechi dhidi ya Norwich Jumapili hii katika Uwanja wa Stamford Bridge kisha watasafiri hadi Wales kucheza na Cardiff City. Chelsea wanahitaji pointi sita lakini Liver na City wote washindwe mechi zao. Liver wanahitaji sita pia lakini Man City wapoteze au watoke sare walau moja wakati City wanachotakiwa ni sita pia iwapo Chelsea na Liver watashinda.
Wenzao hao wakifungwa hata sasa Man City wangetangaza ubingwa.
Kutokana na Manchester United kufungwa na pia Tottenham Hotspur kupoteza mechi wikiendi hii, Everton wana uhakika wa nafasi ya tano walau, kwani hawawezi tena kuwafikia Arsenal walio nafasi ya nne.
Kwa upande mwingine, ilikuwa kilio kwa Fulham na Cardiff ambazo zimeshuka rasmi daraja. Fulham wameanguka baada ya kujaribu kila njia, ikiwa ni pamoja na kubadilisha makocha mara kadhaa na kufanya usajili wa nguvu kwenye dirisha dogo. Cardiff wanashuka baada ya kuwa wamepanda msimu uliopita tu.