*Stoke wapata ushindi wa kwanza Manchester
*Swansea, Southampton na QPR pia washinda
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City wamepigwa mweleka, baada ya kupoteza mechi kwenye dimba lao la Etihad.
Stoke City ndio waliowaadabisha mabingwa hao ambao kwa kawaida hugawa dozi kubwa wanapocheza nyumbani, na hii ni mara ya kwanza katika historia ya Stoke kupata ushindi Manchester.
Shujaa wao alikuwa Mame Biram Diouf ambaye jitihada zake binafsi uwanjani zilizaa matunda katika dakika ya 58 na kuwaacha City wakishangaa na washabiki kukasirika hadi mwisho wa mchezo wenyeji waliposhindwa kusawazisha.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Senegal aliyepata kuchezea United, alikimbia umbali wa yadi 70 na mpira kabla ya kumtazama kipa Joe Hart na kutikisa kamba kwa mpira wa chini chini. Katika kuwaongezea maumivu kwa kocha Manuel Pellegrini na mabingwa hao, Yaya Toure aliyetarajia kupata penati alipewa kadi ya njano kwani mwamuzi Lee Mason aliona kwamba amejirusha.
Katika mechi zao 12 zilizopita kwenye uwanja huo, Stoke walifungwa na Man City na Man United kadhalika, na sasa kocha Mark Hughes atataka kurudia ushindi kama huu dhidi ya timu yake ya zamani ya Man U alikocheza chini ya Sir Alex Ferguson.
SWANSEA WAPAA USHINDI ASILIMIA 100
Swansea wameendelea na asilimia 100 ya ushindi katika mechi zake tatu, kwa kuwakung’uta West Bromwich Albion 3-0.
Swansea walioanza ligi kwa kuwafunga Manchester United 2-1 Old Trafford, walipata mabao mawili kupitia kwa Nathan Dyer dakika ya pili na ya 70, katikati ya muda huo jingine likafungwa na Wayne Routledge dakika ya 24. West Brom walikuwa hawajapoteza mechi zao mbili za awali msimu huu.
SOUTHAMPTON WAWATANDIKA WEST HAM
Southampton wamemudu kuziba mapengo ya kuondokewa na wachezaji wengi nyota, baada ya kuwalaza West Ham 3-1 kwenye mechi ngumu.
Wenyeji West Ham walianza kupata bao dakika ya 27 kupitia kwa Mark Noble, lakini kiungo anayetaka kuondoka Southampton, Morgan Schneiderlin alionesha makali yake kwa kufunga mabao mawili dakika ya 45 na ya 68, huku mchezaji mpya, Pelle akifunga dakika ya 83.
Hiyo itakuwa faraja kubwa kwa kocha Ronald Koeman ambaye amepokwa wachezaji wake wazuri zaidi na Liverpool, Arsenal na Manchester United kiangazi hiki hadi washabiki kuanza kulalamikia klabu.
QPR USHINDI WA KWANZA WA MSIMU
Harry Redknapp alikuwa mtu mwenye furaha baada ya kuibuka kidedea kwenye mechi ya timu yake, Queen Park Rangers (QPR) dhidi ya wagumu Sunderland.
QPR walipata bao lao kupitia kwa Charlie Austin na kuwa ushindi wa kwanza kwa timu hiyo msimu huu. Kadhalika ilikuwa ni mechi waliyoianza wakiwa wamepoteza mechi zao tatu zilizopita kwa ujumla, ambamo hawakuwa wamefunga hata bao moja.
Walianzia mguu mbaya leo, baada ya Loic Remy kuondolewa kwenye orodha ya wachezaji kutokana na Chelsea kuwasilisha mezani dau la kumsajili linalofikia matakwa ya kipengele cha mkataba wake. Remy ndiye angeongoza mashambulizi, badala yake Austin, mfungaji, ndiye akabeba jukumu hilo.
Newcastle, CRYSTAL PALACE SARE 3-3
Uwanja wa St James’ Park ulikuwa na karamu ya mabao ya piga nikupige, baina ya Newcastle na Crystal Palace, ambapo ubishi wao uliishia bila mshindi – mabao 3-3.
Wakicheza chini ya kocha mpya, Neil Warnock, Palace walipata bao dakika ya kwanza tu ya mchezo kupitia kwa Gayle lakini lilisawazishwa na Janmaat wa Newcastle dakika ya 37.
Palace waliweka bao la pili kupitia kwa Puncheon dakika ya 48 lakini likarudishwa na Aarons dakika ya 73. Mchezo uliendelea, ambapo Williamson aliwafungia Newcastle dakika ya 88 na wenyeji wakajua wangeondoka na ushindi, lakini bao likarudishwa na Wilfried Zaha anayecheza kwa mkopo Palace kutoka Manchester United katika dakika ya mwisho.