Safari ya ushindi kwa asilimia 100 kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) kwa Manchester City imefikia ukingoni msimu huu, baada ya kuduwazwa na West Ham kwa kufungwa mabao 2-1.
Baada ya kufungwa kwa idadi hiyo hiyo ya mabao na Juventus kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) wiki iliyopita, City walirejea Etihad wakitaka kushinda mechi ya sita ya EPL mfululizo, lakini West Ham wakawakatalia.
Iwapo wangepata ushindi wangeweka pengo la pointi sita juu ya msimamo wa ligi, lakini walikuwa vijana wa Slaven Bilic walioonesha kandanda safi la kushambulia kwa kushitukiza, na kupata bao lao la kwanza kupitia kwaVictor Moses akimzidi maarifa kipa Joe Hart dakika ya sita tu.
Kana kwamba hiyo haitoshi, wageni walifunga bao la pili kupitia kwa Diafra Sakho kutoka umbali wa yadi sita. Vijana wa Manuel Pellegrini waliamka na mchezaji aliyevunja rekodi ya usajili, Kevin De Bruyne alichomoa moja dakika ya 45.
Sunderland na Newcastle wameendelea kuwa na wakati mgumu, wakiwa kwenye eneo la kushuka daraja baada ya mechi ya sita. Jumamosi hii, Sunderland walikubali kichapo cha 2-0 kutoka kwa vijana waliopanda daraja msimu huu, Bournemouth.
Newcastle waliotarajia kufufuka hasa baada ya kuchukua kocha mpya, aliyepata kufundisha Timu ya Taifa ya England, Steven McLaren waliangukia tena pua, nao wakifungwa na timu iliyopanda daraja msimu huu ya Watford.
Aston Villa wakiwa nyumbani na kocha wao Tim Sherwood waliaibika tena, kwa kufungwa 1-0 na West Bromwich Albion na Stoke wakaenda suluhu na Everton. Jumapili hii Southampton wanawakaribisha Manchester United dimba la St Mary’s; Tottenham Hotspur ni wenyeji wa Crystal Palace wakati Norwich ni wageni wa Liverpool dimbani Anfield kukamilisha mzunguko wa sita.