Menu
in , ,

Man City vs Chelsea

Manchester City wanahitaji alama 15 pekee katika michezo yao 10 ya Ligi Kuu ya England iliyosalia ili kujihakikishia ubingwa. Kesho Jumapili watawakaribisha mabingwa watetezi Chelsea ndani ya dimba la Etihad. Ushindi kwa Manchester City utawasogeza karibu zaidi na taji la EPL wakati Chelsea wakihitaji ushindi kwa ajili ya kujiweka salama kwenye vita ya kuwania nafasi nne za juu inayowahusisha pia Man Utd, Liverpool, Tottenham na pengine na Arsenal pia.

Kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Septemba mwaka jana baina ya timu hizi ndani ya Stamford Bridge, vinara Manchester City waliibuka na ushindi mwembamba wa 1-0 kwa bao safi la shuti kali la mguu wa kushoto lililowekwa wavuni na kiungo wao mahiri Mbelgiji Kevin De Bruyne. Mtanange baina ya miamba hawa kwenye msimu uliopita kwenye dimba la Etihad uliwashuhudia Chelsea wakipata ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji wao.
Matokeo ya michezo ya karibuni yanawapa City faida ya kujiamini wakiwa wamewachakaza Arsenal kwa vipigo viwili mfululizo vya 3-0 kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Carabao wiki iliyopita na ule wa EPL uliopigwa Alhamisi. Chelsea wao wanakwenda Etihad wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha 2-1 kutoka kwa Manchester United walichokipata ndani ya Old Trafford wiki iliyopita.

Licha ya ubora wa Manchester City chini ya Pep Guardiola, Chelsea wanao uwezo wa kutosha kuiletea matatizo timu yoyote. Wanae Eden Hazard ambaye amedumu kama mchezaji tishio kwa muda mrefu na pia kuna Willian aliyeonesha kiwango safi mno kwenye mchezo dhidi ya Man Utd wiki iliyopita na ule wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya FC Barcelona. Hata hivyo vijana hawa wa Antonio Conte wamepoteza michezo mitatu kati ya minne iliyopita ya EPL.

Manchester City wanaoongoza jedwali la Ligi Kuu ya England kwa tofauti ya alama 16 wataingia uwanjani kusaka alama tatu muhimu wakiongozwa na Kevin De Bruyne na nyota wengine tegemeo. Wao ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi (82) kwenye ligi tano kubwa za barani Ulaya mbaka sasa ukiwatoa PSG waliofunga 84. Ni ngumu mno kuwazuia matajiri hawa wa Etihad kukuadhibu hivyo Chelsea wanahitajika kuwa makini dakika zote za mchezo.

Raheem Sterling ambaye kutokana na jeraha la goti alikosa michezo miwli iliyopita ambayo timu yake ilicheza dhidi ya Arsenal anatarajiwa kurejea dimbani hapo kesho. Nyota huyo wa zamani wa Liverpool ameifungia City mabao 15 na kupika mengine 6 kwenye michezo 25 ya Ligi Kuu ya England aliyocheza msimu huu. Uwepo wake utawaongezea City kasi na ubunifu katika mashambulizi iwapo Guardiola atachagua kumjumuisha kwenye kikosi.

Kikosi cha chelsea

Mlinzi wa kulia Kyle Walker pia anatarajiwa kurejea kwenye kikosi kufuatia majeraha mepesi aliyoyapata kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Arsenal. Kiungo Fabian Delph ambaye amekuwa akitumka zaidi kama mlinzi wa kushoto msimu huu atakuwa nje akimalizia kifungo chake baada ya kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwenye mchezo wa Kombe la FA ambao City walifungwa kwa 1-0 na kutupwa nje wiki mbili zilizopita. Benjamin Mendy yeye ni majeruhi wa muda mrefu.

Kwa upande wa Chelsea mlinzi David Luiz, kiungo Tiemoue Bakayoko na mlinzi kinda Ethan Ampadu wote ni majeruhi na watakuwa nje. Hata hivyo kiungo Ross Barkley aliyesajiliwa Januari akitokea Everton anatarajiwa kurejea uwanjani baada ya kupona majeraha aliyoyauguza kwa wiki kadhaa. Kwa ujumla timu zote mbili hazina balaa kubwa la majeruhi. Uwepo wa nyota wote muhimu kwenye vikosi vyote utaupa mchezo huu msisimko na ladha inayotarajiwa.

Hata hivyo Antonio Conte anabaki na kibarua cha kuamua ni nani hasa anafaaa kutumiwa kama mshambuliaji wa kati. Kwenye michezo kadhaa ya karibuni amekuwa akimtumia Eden Hazard kwenye eneo hilo lakini mkakati huu haujaonesha matunda ya maana na kwa kiasi kikubwa umepunguza makali ya Chelsea kwenye eneo la kushoto ambalo Mbelgiji huyo kwa kawaida hucheza. Alvaro Morata ameonesha uwezo finyu na hali ya kutokujiamini kwenye siku za karibuni. Huenda Giroud atapewa nafasi.

Written by Kassim

Exit mobile version