Menu
in , , ,

MAN CITY v UNITED: DHAMIRA YA KUWEKA REKODI DHIDI YA HITAJI LA KULINDA HESHIMA

Tanzania Sports

Manchester City wanaweza kujipoza machungu ya kipigo cha 3-0 walichokipata dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa kushinda taji la Ligi Kuu ya England kesho Jumamosi kwa rekodi ya maana ikiwa watafanikiwa kuwafunga wapinzani wao Manchester United ndani ya dimba la Etihad.

Ikiwa watapata ushindi vijana wa Pep Guardiola watakuwa timu ya kwanza kwenye historia ya miaka 26 ya Ligi Kuu ya England kushinda taji la ligi wakiwa na michezo sita iliyosalia kuhitimisha mashindano. Rekodi hii itaakisi ubabe na utawala wa maana wa Manchester City kwenye msimu huu wa Ligi Kuu ya England.

Vinara Manchester City wanawazidi vijana wa Jose Mourinho walio katika nafasi ya pili kwa alama 16 na hivyo swali lililosalia ni lini matajiri hao wa Etihad wataunyakua rasmi ubingwa na si iwapo wataweza kuunyakua ubingwa huo wa msimu huu unaoelekea ukingoni.

Wababe hawa wa Ligi Kuu ya England kwa vyovyote vile wana shauku kubwa ya kurejesha taswira ya ufalme wao iliyoharibiwa na Liverpool baada ya kipigo cha 3-0 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa uliopigwa Jumatano. Hata hivyo mchezo huu unachezwa siku tatu tu kabla ya mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Liverpool na hivyo unampa wakati mgumu Pep ambaye anaamini kuwa kikosi chake kinaweza kupindua matokeo dhidi ya Liverpool.

Baada ya miongo kadhaa wakiwa wanyonge mbele ya mahasimu wao hao, Manchester City sasa wameubadili kabisa upepo ambapo wanaelekea kutwaa taji lao la tatu la EPL tangu 2012 huku United wakiwa na moja tu pekee tangu wakati huo ambalo walilitwaa kwenye msimu wa 2012/13 ambao ulikuwa wa mwisho kwa Sir Alex Ferguson.

Guardiola ambaye alilazimika kupitia kipindi kigumu kwenye msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya England sasa amewanyamazisha wakosoaji wake waliodai kuwa mbinu zake za mchezo laini wa kucheza pasi nyingi usingeweza kufua dafu kwenye Ligi ya England waliyodai kuwa ni ngumu inayohitaji mchezo wa nguvu zaidi.

Kiungo raia wa Ubelgiji Kevin De Bruyne amekuwa mchezaji wao bora zaidi mbaka sasa huku David Silva, Leroy Sane, Raheem Sterling na Sergio Aguero wote pia wakiwa wametoa michango ya maana. Lakini kutokana na hitaji la lazima la kujaribu kupindua matokeo dhidi ya Liverpool huenda nyota wote hawa watapumzishwa kwenye mchezo wa kesho Jumamosi wakiwasubiri Liverpool.

Mhispania Pep Guardiola ambaye ni kocha wa zamani wa FC Barcelona na Bayern Munich alishinda taji lake la kwanza kwenye soka la England Februari mwaka huu alipowafunga Arsenal 3-0 kwenye mchezo wa fainali ya Carabao Cup uliopigwa katika dimba la Wembley.
Tangu wakati huo vinara Manchester City tayari walikuwa wameshawaacha mbali wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England na itapendeza zaidi kwao ikiwa watatwaa ubingwa huo kwa rekodi nzuri wakihitaji ushindi kwenye mchezo wa kesho pekee kuweka rekodi hiyo.

Kwa upande wa United ushindi hauwezi kuwapa matumaini yoyote ya maana ya kushinda taji la EPL kwa kuwa City watahitaji kushinda michezo miwili tu kwenye sita itakayosalia ili kujihakikishia ubingwa. Pia kipigo hakitawawaweka kwenye hatari ya kukosa nafasi nne za juu kwa kuwa kuna pengo la alama 12 kati yao na Chelsea walio kwenye nafasi ya tano. Hawana cha maana cha kujiongezea wala cha kupoteza kuhusu msimu huu.

Lakini kwa vyovyote iwavyo Mashetani hao Wekundu hawapo tayari kukubali fedheha ya kuwaona mahasimu wao wakitangaza ubingwa kwa kuwafunga wao. Mbaya zaidi watavunja rekodi yao waliyoweka msimu wa 2000/01 chini ya Sir Alex ya kutwaa taji la ligi mapema zaidi wakiwa na mechi 5 zilizosalia.

Hivyo United wana kila sababu ya kuwafunga City ama kuambulia angalau sare ili kuchelewesha sherehe za ubingwa za mahasimu wao hao. Shukrani kwa Liverpool waliowapa City sababu ya kupuuza mchezo huu wa kesho kwa kuwa wana kibarua kizito cha kujaribu kupindua matokeo ya 3-0 ya Ligi ya Mabingwa siku tatu baada ya mchezo huo.

Pengine Manchester City sasa watapuuza nafasi ya kuandika historia ya kushinda taji la Ligi Kuu ya England mapema zaidi tena dhidi ya mahasimu wao. United na Jose Mourinho wanapata faida kubwa ya kujilinda dhidi ya fedheha. Hata hivyo City wana kikosi kipana na huenda watafanikiwa kutwaa taji hapo kesho hata wakiwapumzisha Kevin De Bruyne na wenzie.

Written by Kassim

Exit mobile version