Menu
in , , ,

Man City nusu fainali FA

*QPR wa Redknapp wakunjua makucha

* Reading, Sunderland, Swansea walala

 

Mabingwa wa England, Manchester City wameingia nusu fainali ya Kombe la FA kwa kishindo, baada ya kuwachakaza Barnsley mabao 5-0.

Carlos Tevez ndiye aliyeibuka shujaa Etihad, baada ya kufunga mabao matatu na kusaidia kupatikana mengine mawili.

Tevez aliyekamatwa na polisi hivi karibuni kwa madai ya kuendesha gari wakati amepigwa marufuku, alituliza akili yake na kuwafurahisha washabiki.

Raia huyo wa Argentina alifunga mabao mawili kipindi cha kwanza na la tatu kipindi cha pili. Aliwatengea mipira Aleksandar Kolarov na David Silva katika nusu zote za mchezo, nao wakafunga.

City walimchezesha golikipa namba mbili, Costel Pantilimon badala ya namba moja wao na England, Joe Hart na pia nahodha Vincent Kompany na mpachika mabao, Sergio Aguero hawakucheza.

Man City sasa wameshinda mechi nne mfululizo, na wanatafuta kuingia fainali ya FA waliyofika misimu miwili iliyopita.

English: Joleon Lescott, Vincent Kompany Lech ...
English: Joleon Lescott, Vincent Kompany Lech Poznań vs Manchester City FC, 4 November, 2010 (Photo credit: Wikipedia)

Bosi Harry Redknapp wa Queen Park Rangers (QPR) alikuwa mwenye furaha, baada ya vijana wake kuwalaza Sunderland 3-1 katika mzunguko wa 29 wa Ligi Kuu England (EPL).

Huo ndio ushindi wa kwanza mkubwa tangu kuanza msimu huu, na sasa QPR wamefungana kwa pointi 23 na Reading, wakishika nafasi za mwisho kwenye msimamo.

Wakicheza nyumbani Loftus Road, QPR walielemewa na kuruhusu bao dakika ya 20 kupitia kwa Steven Fletcher, lakini mchezaji mpya wa QPR, Loic Remy alisawazisha dakika 10 baadaye kwa kumbabatiza kipa Simon Mignolet.

QPR waliongeza shinikizo kwa wapinzani wao, na  Andros Townsend akawanyanyua washabiki wa QPR kwa mkwaju wa yadi 22 uliojaa kimiani.

Wakati washabiki wakianza kuondoka uwanjani, Jermaine Jenas aliongeza tamu ya ushindi wa QPR kwa kupachika bao la tatu dakika ya 90. Sunderland wanashika nafasi ya 14, chini zaidi ya eneo walilozoea.

Mwingine aliyepata ahueni Jumamosi hii ni bosi Paul Lambert wa Aston Villa, baada ya kufanikiwa kuwafunga Reading 2-1 na kujinasua kwenye eneo la kushuka daraja.

Kocha Lambert amekuwa katika wakati mgumu, ikiwa ni pamoja na kufungwa mechi mfululizo na kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la FA na Kombe la Ligi na timu ndogo.

Huu ni ushindi wa pili tu tangu kuanza mwaka huu 2013, ambapo Jumamosi hii walianza vibaya, kwa kutangulia kufungwa.

Beki wao, Nathan Baker alikuwa akimpatia pasi golikipa wake, Brad Guzan lakini mpira ukamzidi na kuzitikisa nyavu dakika ya 32.

Hata hivyo, mshambuliaji tegemeo wa Villa, Christian Benteke alijibu kwa kupachika bao la kusawazisha dakika moja tu baadaye, kisha Gabriel Agbonlahor akapachika bao la ushindi kwa fataki kali muda mfupi tu kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza.

Masahibu ya Reading yalikuwa makubwa, na ushindi wa Villa kupatikana ugenini Madjeski ni kielelezo cha dhamira ya Villa kubaki EPL.

Katika mechi iliyopita walicheza kufa na kupona dhidi ya mabingwa Manchester City katika Villa Park, Birmingham, lakini waliishia kufungwa kwa tabu bao 1-0.

Sherehe za Swansea kutwaa Kombe la Ligi baada ya miaka 100 zilihitimishwa kwa kipondo kutoka kwa West Bromwich Albion.

Romelu Lukaku (19) anayecheza kwa mkopo West Brom kutoka Chelsea alipachika moja ya magoli yao mawili na Swansea kupata moja, lakini pia alikosa penati.

Swansea waliwazawadia bao wapinzani wao, pale Jonathan De Guzman alipogongwa na mpira uliozama nyavuni, wakati Pablo Hernandez ‘Michu’ akiokoa kwenye mstari wa goli lake.

Swansea walikuwa wa kwanza kupata bao, lililofungwa na Luke Moore.

Ushindi huo umewafanya West Brom kuwapita Swansea na Liverpool ambao hawajacheza na kupanda hadi nafasi ya saba kwa kufikisha pointi 43.

Swansea waliomwongezea kocha wao, Michael Laudrup mkataba wa mwaka mmoja hadi 2015, wameshuka hadi nafasi ya tisa.

Mechi ilimalizika kwa utata, baada ya bao walilofunga Swansea kupitia Roland Lamah kukataliwa, ambapo hata kocha wa West Brom, Steve Clarke alisema mfungaji hakuwa ameotea, tofauti na waamuzi walivyoamua.

Uamuzi mwingine tata ulitokea Carrow Road, wenyeji Norwich walipopewa penati dakika za majeruhi lakini mkwaju wa Grant Holt uliokolewa na kipa wa Southampton, Artur Boruc na kufanya timu hizo kutoka suluhu.

Mwamuzi alikuwa Mark Clattenburg aliyelalamikiwa na Chelsea kwa lugha ya kibaguzi na pia na Arsenal kwa kuendeleza mchezo baada ya mchezaji wao kuumizwa.

Suluhu hiyo inawaacha Norwich na pointi 33 katika nafasi ya 13, huku Southampton wakiwa nafasi ya 16 kwa pointi 28.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version